27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

VIGOGO MBARONI KWA RUSHWA YA MIL 43/-

Na BENJAMIN MASESE-GEITA

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (Takukuru) Mkoa wa Geita, imewaburuza mahakamani vigogo wawili wa kusimamia upimaji ardhi mkoani humo kwa makosa manne ya kuomba rushwa.

Vigogo hao ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Ardhi na Maliasili Halmashauri ya Wilaya ya Geita, Salu Ndongo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Inland Surveyors Ltd ya Dar es Salaam ambayo ilishinda zabuni ya upimaji viwanja katika mradi wa Cadastral Survey.

Watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani juzi mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Geita, Ushindi Swallo na kusomewa mashtaka na waendesha mashtaka wa Takukuru, Kelvin Mrusuri, Augustino Mtaki, Felister Chamba na Husna Kiboko.

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa washtakiwa walitumia nyaraka mbalimbali za udanganyifu katika kuomba malipo ya kazi ya upimaji wa viwanja 2,000 katika eneo la Magogo na kuisababishia Serikali hasara ya Sh milioni 43.23.

Hata hivyo, baada ya kusomewa mashtaka hayo, washtakiwa walikana mashtaka yote matatu ya kumdanganya mwajiri na moja la kuisababishia hasara Serikali.

Upande wa mashtaka uliieleza mahakama kuwa uchunguzi wa kesi umekamilika na kuiomba mahakama   kupanga tarehe ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali na kwamba haukuwa na pingamizi la dhamana kwa washtakiwa.

Hakimu Swallo, aliwataka washtakiwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja alitakiwa kusaini bondi ya Sh milioni 20 pamoja na kuwa na hati ya mali isiyohamishika.

Washtakiwa wote walitimiza masharti ya dhamana waliyopewa na wako nje kwa dhamana. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Aprili 4, mwaka huu itakapotajwa kwa ajili ya washtakiwa kusomewa maelezo ya awali.

Mkuu wa Takukuru wa mkoa huo, Thobias Ndaro, aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles