Na Nora Damian, Mtanzania Digital
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Mkoa wa Njombe, Scolastica Kevela amepongeza juhudi zinazoonyeshwa na Rais Samia Suluhu Hassan na kuwataka Watanzania kumuunga mkono ili aendelee kuiongoza Tanzania katika kipindi kingine.
Kevela ameyasema hayo Februari 5,2024 wakati akizungumzia maadhimisho ya miaka 47 ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Amesema miongoni mwa mambo mengi ya kupongezwa ni katika ujenzi wa demokrasia nchini na kusema Rais Samia amekuwa akitumia busara na hekima katika uongozi wake.
“Amekuwa ‘role model’ katika uongozi kitaifa na kimataifa, sisi wanawake wa Mkoa wa Njombe tunasema 2025 kuelekea 2030 ni Dokta Samia Suluhu Hassan, tunamuunga mkono kwa sababu tunaona anayoyafanya…tuna amani, utulivu, nchi imetulia.
“Kupitia Rais Samia sisi wanawake katupaisha, katupatia makatibu tawala, wakuu wa wilaya, wakurugenzi, wabunge na anaelekea kutupeleka kwenye 50 kwa 50. Tunamuombea aendelee kufanya kazi vizuri na sisi tuko nyuma yake kuhakikisha tunafanya kazi kwa bidii,” amesema Kevela.
Amewataka Watanzania waendelee kukiunga mkono CCM ili kiendelee kushika dola kwa sababu yapo ya kujivunia chini ya utawala wake.
“Miaka 47 ya Chama Cha Mapinduzi inaonyesha namna gani chama kilivyo imara na kitaendelea kushika hatamu kwa sababu lengo letu ni kuisogeza Tanzania mbele.
“Mama kaleta Royal Tour inatuletea watalii wengi, sasa Tanzania inajulikana kitaifa na kimataifa, miaka ya nyuma watu walikuwa wanasema Mlima Kilimanjaro uko Kenya lakini sasa hivi wanatoka huko wanajua uko Tanzania.
“Mikopo ya elimu ya juu hadi wanaosoma diploma wanapata, elimu bure inatolewa hadi kidato cha sita…haya ni maendeleo makubwa,” amesema.
Amesema wanaendelea kushiriki kwa vitendo katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia na kuongeza idadi ya wanachama wapya.