Na JUSTIN DAMIAN -DAR ES SALAAM
TUME ya Ushindani (FCC) imekataa kuridhia muungano wa Kampuni ya AB InBev, inayotaka kuinunua Kampuni ya SABMiller inayomiliki Kampuni ya Bia Tanzania, (TBL Group) yaliyowasilishwa kwake kwa mujibu wa Sheria ya Ushindani.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Dk. Frederick Ringo, maombi ya muungano huo yaliwasilishwa kwa mujibu wa wa Sheria ya Ushindani Namba 8 ya mwaka 2003 pamoja na kanuni zake na kuongeza kuwa, tayari wamechapisha tangazo katika magazeti.
Lengo la matangazo hayo ni kuwaalika wale wote wenye pingamizi au maoni tofauti kuhusiana na maombi ya kuidhinishwa kwa muungano huo, wawasilishe maoni yao ili yaweze kuwa sehemu ya tathmini kabla ya uidhinishaji wa maombi ya muungano husika.
“Ikiwa ni sehemu ya utaratibu wake wa kiuchunguzi (inquisitorial process) na ikiwa ni sehemu ya utaratibu wa kisheria unaoongoza shughuli za tume, bado inaendelea kuchunguza masuala mbalimbali kuhusu ombi la muungano huo,” alisema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari.
Aidha katika taarifa hiyo, Dk. Ringo alieleza kuwa, taratibu hizo zinahusisha pia tathmini za taarifa mbalimbali na kuwapa fursa wadau kusikilizwa pingamizi zao na maoni yao kuhusiana na muungano huo na kuzitolea maamuzi kabla ya kufikia uamuzi wa mwisho kuhusiana na kuidhinisha muungano husika.
Taarifa hiyo ilitolewa kufuatia taarifa zilizochapishwa na gazeti moja la wiki linaloandika kwa lugha ya Kiingereza, likisema FCC imekamilisha mchakato wa uidhinishaji wa muungano huo na kwamba imekwisha kuuidhinisha, jambo ambalo si sahihi kwa mujibu wa Tume ya Ushindani.
“Kwa mantiki hiyo, Tume haijafikia hitimisho la tathmini ya maombi ya muungano huo na bado haijayaidhinisha.
“Tume inaviasa vyombo vya habari kuepuka kuchapisha taarifa zilizoegemea upande mmoja na ambazo hazikuthibitishwa na upande wa pili kwa kuwa zinawe za kusababisha misuguano isiyo kuwa na ulazima.