HAKUNA ubishi kuwa mapenzi yanachukua nafasi kubwa sana katika maisha ya binadamu, ipo dhahiri kwamba mapenzi yanaweza kuleta furaha maishani mwako lakini wakati huohuo  maumivu, mateso na karaha.
Watu wengi bado wanalizwa na mapenzi na hii ni kwa sababu hawafuati kanuni sahihi za mapenzi. Ndiyo… mapenzi yana kanuni zake.
Kwa bahati mbaya kabisa, kwa sasa mapenzi yamegeuzwa na kuwa kama kitu cha kujaribu au kufanyia biashara ndiyo maana yanawatesa wengi.
Lakini ni kwa nini mapenzi yaendelee kututesa? Au ni kwa sababu hatujui maana halisi ya mapenzi? Hebu tuyaangalie mapenzi kwa jicho la tatu, kisha tuchukue hatua.
MAPENZI NI NINI?
Katika hali ya kawaida, mapenzi hayaelezeki kuwa ni nini. Ni vigumu sana mtu kukueleza maana ya mapenzi ndiyo maana kila mtu ana uelewa tofauti juu ya suala hilo.
Mtaalamu mmoja wa masuala ya mapenzi kutoka Colombia, aliwahi kuyaelezea mapenzi ndani ya kitabu chake cha More About Love, akisema; ‘Love is natural feelings, which take place from the deepest part of your heart upon somebody or something else’.
Kwa tafisiri isiyo rasmi alimaanisha kuwa mapenzi ni hisia za asili ambazo huchukua nafasi kutoka sehemu ya ndani kabisa ya moyo juu ya mtu au kitu chochote. Tena bila kuwa na visingizio au masharti ya aina yoyote.
HISIA NI NINI?
Huu ni msukumo wa vichochezi katika homoni za ndani ya mwili ambazo hutokea kutokana na mazingira. Lakini huwa tofauti kati ya mtu na mtu na ndiyo maana watu hutofautiana madaraja ya kupenda.
Mfano halisi ni kwamba, utakuta mtu anapenda sana wanawake weupe, lakini mwingine hataki hata kuwaona. Lakini mapenzi siyo mawazo au uamuzi wa mtu, bali hisia ambazo hutokea pasipo uamuzi wa mtu.
Kutokana na hali hiyo, utasikia mtu akisema: ‘Sijui nimempendea nini huyu mwanaume!’ ni kweli yeye hajaamua lakini hisia zimefanya awe hivyo.
USIRUHUSU MAPENZI YAKUTESE
Kwa nini mapenzi yakuumize? Unakosea wapi? Kwa nini ukataliwe kila mara? Haya ni baadhi ya maswali ya kujiuliza kuhusu mateso ya mapenzi.
Kamwe katika maisha yako usiruhusu mapenzi yakutese, najua yawezekana kila mpenzi unayempata haudumu naye, wewe ni mtu wa kulia kila siku, hujawahi kufurahia maisha hata siku moja, jipange upya.
Thamini na jali zaidi maisha yako kwanza, fikiria kipi ni bora kati ya mapenzi na maisha yako, ni kipi kilitangulia? Kama maisha ndiyo yalitangulia kwa nini usijijenge kwanza kimaisha ndipo mengine yafuate?
Hata kama unateswa na mtu unayempenda kwa dhati, hata kama ni mzuri kwa kiwango gani, kwani bila yeye maisha hayaendi? Si kweli na kama unaweza kuishi bila yeye kwa nini akutese namna hiyo?
Usikubali hisia zako zichezewe, mwamuzi wa mwisho wa maisha yako ni wewe mwenyewe. Ni vyema kuchuja mambo na kuwa katika uhusiano na mtu sahihi ambaye mnagongana kihisia.
Kama hisia zako na zake ni tofauti, kwa nini uendelee kumng’ang’ania? Ni bora kufanya maamuzi magumu ambayo yanaweza kukuumiza mara moja, lakini ukawa na furaha katika maisha yako yote.
Usidanganyike, mapenzi ni kufurahi. Kama upo kwenye uhusiano ambao unahisi unateseka, basi huna sababu ya kuendelea nao.
Usikose sehemu ya mwisho ya mada hii wiki ijayo.
Kama unapenda kupata mafunzo haya zaidi kupitia kundi letu la WhatsApp, tafadhali wasiliana nasi inbox.
Pia jiandae kupata kitabu changu kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachotoka hivi karibuni.