Na Leonard Mihafu, Lilongwe.
KUMEKUWA na maswali kadhaa niliyowahi kutafakari kuhusiana na demokrasia. Maswali hayo naweza kuyaita pacha kwa mfanano wake kimuundo na kimtizamo.
Swali la kwanza, je, tunahitaji demokrasia ama maendeleo? La pili tunahitaji demokrasia ili kuendelea ama tunahitaji maendeleo ili kuelekea demokrasia?
Maswali hayo ndiyo msingi wa hoja. Niliyatafakari nikinuia kugusa kiini cha demokrasia yenyewe, yaani demokrasia kuanzia kwa wayunani na baadaye kupokelewa na mataifa ya magharibi, mwishowe kubambikiziwa Waafrika na huo ndio msingi wa maswali hayo.
Demokrasia kama mfumo wa kiutawala licha ya kutofautiana kulingana na taifa hadi taifa, bara hadi bara bado viungo vya msingi ni haki, usawa na uhuru. Kutoka katika viungo hivyo vitatu demokrasia imejipambanua kusimamia haki itolewayo na watawala ama mahakama kwa raia wa sehemu husika kwa uhuru na usawa stahiki.
Demokrasia kwa wayunani ilifikiwa kama tunda la siasa iliyokomaa na fikara pevu. Hivyo hadi kufikia demokrasia wayunani iliwabidi kufikiri, kupambanua na kufikicha akili zao ili kufikia namna ya utawala ambayo itatenda haki katika pande mbili, watawala na watawaliwa.
Wayunani walipitia kashikashi za utawala wa Kifalme ambao baadaye ulisababisha taifa hilo kutawaliwa kiimla kwani mtawala alikuwa na nguvu kubwa za kimaamuzi na hivyo haikuwa rahisi kwa wananchi na wanafalsafa wa kipindi hicho kukubaliana na namna hiyo ya kiutawala. Wakaangukia katika demokrasia ambayo ilionekana ndiyo namna bora sana ya utawala kupita hizo zote zilizotangulia.
Hivyo kwao kila hatua ya kifikra ilitawaliwa na fikra kinzani juu ya ubora na uhakika wa namna hiyo ya utawala. Licha ya wengi kuona demokrasia ni njia sahihi ya utawala mwanafalsafa Plato yeye alikuwa na maoni ya tofauti sana.
Plato alitoa kauli yake maarufu ikisema ‘Democracy is the government of the fools’ yaani kwa Kiswahili kisicho rasmi demokrasia ni utawala wa wapumbavu.
Demokrasia hiyo hiyo ilipasua anga na kuangukia katika mataifa mbali mbali. Taifa linaloonekana kuongoza kidemokrasia duniani ni Marekani. Rais wa zamani wa Marekani, Abraham Lincoln anasimama katika historia kama nguzo ya utawala wa kidemokrasia.
Katika Bara la Afrika demokrasia ililetwa, ilipandikizwa ama iliamuliwa kama suala la lazima na si pendekezo wala ombi. Hivyo vikawekwa vigezo vya nchi za Afrika kupokea misaada ya kibinadamu na kiuchumi kutoka Benki ya Dunia ni lazima nchi hizo ziipokee demokrasia kama njia yao ya kiutawala.
Nchi hizo za Afrika zikiwa changa kiuchumi hazikuwa na mbadala wa kiuchumi bali kukubaliana na vigezo hivyo. Kwa sababu hii mwandishi wa siasa Gerardo Munk anasema “Democracy in Africa was an order from above”, yaani kwa tafsiri isiyo rasmi “demokrasia kwa Afrika ilikuwa ni amri kutoka juu”.
Hoja hiyo ya Munk ndiyo inayosababisha demokrasia kwa Afrika kuwa na sura tofauti kulingana na nani anatawala na nini anataka kufanikisha. Katika kutaja nchi chache, ukiangalia Zimbabwe, Togo, Uganda, Burundi, Kongo ambayo inaitwa Jamhuri ya Kidemokrasia unaona ukweli usio na shaka kuwa demokrasia yetu ina sura ya upekee, upekee wake ni kwanza, katika uanzishwaji wake na pili, namna tunavyoifanyia kazi kwenye ulingo wa siasa.
Ipi hoja juu ya maendeleo?
Demokrasia kwa wayunani ilikuwa ni tunda la fikra pevu na siasa zilizokomaa kwa hoja. Hivyo demokrasia ilikuwa ni mojawapo ya maendeleo waliyoyapata kupitia siasa na fikra. Hii inafanya demokrasia kwa wao kuwa mojawapo ya hatua walizoipiga.
Kwa Afrika demokrasia tuliaminishwa ili kupewa misaada ya kiuchumi na baadaye kuendeleza mataifa yetu ni lazima tuwe na demokrasia yao. Kwa lugha nyepesi ili tuendelee tulihitaji demokrasia.
Ukiangalia kiundani juu ya ujio wa demokrasia Afrika unaona hata ujio wake haukuwa wa kidemokrasia. Waafrika hatukuwa na chaguo tofauti na la kukubali kwani kuikataa demokrasia ilionekana ni sawa na kulipiga teke bakuli la dhahabu.
Baadhi ya watawala wa nchi za Afrika wanaamini demokrasia ndio inakwamisha maendeleo huku wengine wakiwa na msimamo wa vuguvugu juu ya suala hilo.
Kimsingi tunapaswa kujiuliza je; tatizo lipo kwenye demokrasia yenyewe ama mtazamo wetu juu ya demokrasia? Au tunahitaji demokrasia ya kuletewa ama tufikiri kivyetu na kuona namna ya utawala yenye kuendana na Afrika ya sasa na ya baadaye?