Na Faraja Masinde, Mtanzania Digital
Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA) umebainisha kuwa utalii wa picha ni moja ya eneo linalovutia watalii wengi kwasasa na huku ikibainisha kuwa idadi ya watalii imekuw aikiongezeka mwaka hadi mwaka.
Kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa na Kaimu Kamishna wa Hifadhi wa Wakala wa Usimamizi wa Wanyamapori (TAWA), Mabula Misungwi Nyanda, kwa Wahariri wa vyompbo vya habari waliotembelea Pori la Akiba la Pande liliko Mabwepande jijini Dar es Salaam, imebainisha kuwa kupitia aina hiyo ya utalii hata mapato yamekuwa yakiongezeka.
Kwa mujibu wa Nyanda, kwa mwaka wa Fedha 2021/22, kumekuwa na ongegezeko la asilimia 76.2 la watalii ikilinganishwa na mwaka uliopita.
“Kutokana na jitihada zinazoendelea kuchukuliwa na serikali ikiwemo utoaji wa chanjo
ya Uviko-19 na utangazaji wa utalii na kuvutia uwekezaji kupitia programu maalum ya
“Tanzania – The Royal Tour” mwenendo wa utalii wa picha umeanza kuimarika. Katika mwaka wa fedha 2021/22, jumla ya watalii wa picha 158,108 walitembelea katika
maeneo yanayosimamiwa na TAWA.
“Idadi hiyo ni ongezeko la asilimia 76.2 ikilinganishwa na watalii wa picha 37,684 waliotembelea katika maeneo yanayosimamiwa na TAWA kwa mwaka 2020/21.
“Sambamba na hayo kutokana shughuli za utalii (utalii wa picha na uwindaji) Mamlaka imekuwa ikitoa gawio kwa Halmashauri za Wilaya, Vijiji na maeneo ya Jumuiya za Hifadhi ya WanyamaporiWMAs. Kati ya mwaka 2016/17 – 2021/22, Mamlaka imetoa jumla ya Sh bilioni 37.79 kwa wanufaika hao,” amesema Nyanda.
Aidha, amefafanua kuwa kanuni za uwindaji wa kitalii zinaelekeza kampuni zilizokodishwa vitalu vya uwindaji kuchangia shughuli za maendeleo kwa walau dola za Marekani 5,000 kwa kila kitalu kwa mwaka.
“Lengo la Tawa ni kuhakikisha kuwa wananchi na watalii wanafurahia aina mbalimbali ya utalii lakini pia jamii ikinufaika,” amesema.
Upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa TAWA, Meja Jenerali mstaafu Hamis Semfuko, akizungumza kwenye warsha hiyo ya wanahabari alibainisha sababu ya kuja na aina hiyo ya utalii kuwa ni kuvutia Watanzania na wageni ambao wakati mwingine kwao wamekuwa wakiwaona wanyama mara kwa mara.
“Mfano kuna watu wanaishi wanawaona Twiga, Tembo kwenye hifadhi zetu za mikumi, Serengeti na kwingine sasa mtu kama huyu ili uweze kumshawishi kufanya utalii basi unatakiwa umpe kitu cha tofauti mbali na wanyama.
“Hivyo uwepo wa vivutio vingine tofauti kutachangia kuwepo kwa uchaguzi tofauti na kuongeza vyanzo vya mapato kupitia utalii nchini ukiwemo utalii huo wa picha, utalii wa malikali, utalii wa baharini sambamba na ule wa pikniki na kutembea kwenye misuti kama msitu wa Pande unaotoa fursa mbalimbali za utalii jijini Dar es Salaam,” amesema Meja Jen mstaafu Semfuko .