WATU wengi kwa kadiri ya uwezo wao hupenda kula mayai karibu kila siku, wakiamini ni mazuri kiafya hasa kile kiini cha kati.
Ni kwa vile kwa miaka mingi wamehakikishiwa na wataalamu wa afya juu ya manufaa ya mayai mwilini.
Wengi wanaofahamu umuhimu huo wa yai hupendelea kula angalau yai moja kila siku wakati wa kifungua kinywa na tafiti za nyuma zimeshauri hivyo.
Miongoni mwa faida zinazoelezwa ni kwamba protini zilizoko ndani ya mayai hukufanya kutohisi njaa mapema.
Ina maana kuwa ukila mayai unaweza kukaa muda marefu zaidi bila kula ikilinganishwa na mikate au vyakula vingine vya ngano.
Kadhalika, inaelezwa kwamba ulaji wa mayai husaidia kupunguza uzito wa mwili. Baadhi ya tafiti zinasema watu wanaokula mayai wamefanikiwa kupunguza uzito wa miili yao kwa kiasi kikubwa ikilinganishwa na wasiokula.
Kadhalika inaelezwa ukilinganisha na vyakula vingine vya protini kama vile nyama, mayai ni bei rahisi zaidi. Hivyo basi, mayai yanaweza kupatikana na kuandaliwa kwa urahisi wakati wa kifungua kinywa kuliko vyakula vingine.
Lakini pia licha ya kwamba kuwa mayai yana kiwango fulani cha lehemu (cholesterol). Lakini utafiti uliofanyika huko nyuma ulibaini lehemu iliyoko katika mayai inapoliwa haina athari kwenye kiwango cha lehemu kwenye damu. Hivyo hakuna haja ya kuhofia juu ya magonjwa ya moyo yatokanayo na lehemu.
Hali kadhalika tafiti za nyuma zilieleza kirutubisho kinachoitwa ‘Choline’ kinachopatikana kwenye mayai ni muhimu katika ukuaji na maendeleo ya ubongo. Pia kinahusishwa katika kuongeza uwezo wa ubongo wa kutunza kumbukumbu.
Pia inaelezwa kuwa kemikali za leutin na zeaxanthin zinazopatikana kwenye mayai zinaaminika kulinda macho dhidi ya madhara ya mionzi mibaya. Pia inaaminika kuwa zinazuia kutokea kwa tatizo la mtoto wa jicho uzeeni.
Lakini wataalamu wamekuwa na shaka kuhusu uhakika wa hayo baada ya kubaini kuwapo kwa visababishi vya maradhi ya moyo pamoja na vifo vya mapema katika yai iwapo yataliwa kwa wingi.
Hivyo, kwa miaka kadhaa wataalamu wa afya wamekuwa wakiumiza kichwa iwapo ulaji wa mayai ni mzuri au mbaya kwa afya ya mwanadamu.
Na hivyo, tafiti zimefanyika ukiwamo huu mkubwa uliofanyika hivi karibuni, ambao umehitimisha kwamba jibu la swali hilo linategemeana na kiwango cha mayai unayokula kwa wiki.
Kwa mujibu wa utafiti mpya uliochapishwa kwenye jarida la Jumuiya ya Tiba Marekani (JAMA), kula mayai mawili tu kwa siku kunaweza kusababisha maradhi ya moyo na hata kifo cha mapema.
Hilo linatokana na kiwango kikubwa cha lehemu kinachopatikana kwenye kiini cha yai, matokeo ambayo kama tulivyoona yanahitilafiana na tafiti za nyuma.
Kwa mujibu wa Idara ya Kilimo ya Marekani yai kubwa moja lina hadi miligramu 300 za lehemu, kikiwa ni zaidi ya nusu ya kiwango cha lehemu, ambacho Shirika la Afya Duniani (WHO) linashauri mtu ale kwa siku miligramu 185.
Utafiti wa JAMA ulichakata taarifa kutoka katika majaribio sita yaliyohusisha zaidi ya watu 30,000 katika kipindi cha miaka 17.
Watafiti wamefikia hitimisho kuwa kula miligramu zaidi ya 300 za lehemu kwa siku kunaongeza hatari ya kupata maradhi ya moyo kwa asilimia 17 na vifo vya mapema kwa asilimia 18.
Uwiano huo wa hatari huongezeka zaidi kwenye ulaji wa mayai na wanasayansi wamebaini kuwa kula mayai matatu au manne kwa siku kunaongeza hatari ya kupata maradhi ya moyo kwa asilimia sita na vifo vya mapema kwa asilimia nane.
Kwa mujibu wa utafiti huo, madhara hayo ya mayai hayaathiriwi na umri, nguvu ya mwili, matumizi ya tumbaku na historia ya kuwa na shinikizo la damu.
“Utafiti wetu umebaini kuwa endapo watu wawili watafuata aina moja ya mlo na tofauti pekee ikawa ni ulaji wa mayai, basi yule ambaye mwenye kula mayai mengi ana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa ya moyo kuliko yule asiyekula,” anasema Norrina Allen, Profesa Mshiriki wa Dawa za Kinga katika Chuo Kikuu cha Northwestern ambaye pia ameshiriki kuandika utafiti huo.
Utafiti mpya unatofautiana na kazi za tafiti za awali, ambazo zilibaini kuwa hakuna uhusiano kati ya ulaji wa yai na uwezekano mkubwa wa kupata maradhi ya moyo.
Lakini, Allen anasema kwamba kulikuwa na sampuli tofauti chache na zilikuwa na muda mfupi wa kufuatilia walaji wa mayai.
Hata hivyo, watafiti wanakiri kuwa huenda kuna makosa katika uchunguzi wao.
Data kuhusu ulaji wa yai zilikusanywa kwa njia ya maswali, ambapo ilibidi walioulizwa kukumbuka chakula chao katika kipindi cha miezi na miaka kadhaa.
Watafiti wengine pia wanasema kuwa matokeo hayo ni ya kuchunguzwa zaidi na ingawa walieleza uhusiano kati ya ulaji wa yai na kuongezeka kwa hatari ya ugonjwa wa moyo na kifo cha mapema, hawawezi kuthibitisha sababu ya hali hiyo.
“Umuhimu wa utafiti huu ni kwamba uliwakilisha jamii tofauti za watu wa Marekani na chakula kinacholiwa na Wamarekani wa kawaida,” anasema Tom Sanders, Profesa wa Masuala ya Lishe katika Taasisi ya King’s College mjini London.
“Ukomo wake unategemea kipimo cha ulaji wa lishe moja,” alisema.
Mwandishi mwenza wa utafiti huo, Allen anapendekeza kutokula mayai zaidi ya matatu kwa wiki.
Pia anatoa ushauri kwa wanaopenda kula mayai, kula hasa sehemu nyeupe ya yai.
“Siwaambii watu wayaondoe kabisa mayai kwenye mlo wao, bali ninapendekeza tu kwamba watu wayale kwa kiasi,” anasema.
Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2015 wa Tume ya Kimataifa ya Mayai (IEC), nchi zinazoongoza duniani kupenda kula mayai kwa kuzingatia kiwango cha mayai yaliyoliwa kwa mwaka ni:
Mexico wastani wa mtu kula mayai ni 352 kwa mwaka, Malaysia 342, Japan 329, Urusi 285, Argentina 256, China 254.8, Marekani 252, Denmark 245.
“Wastani wa kiwango cha cholesterol kinacholiwa na Wamarekani kinaweza kufikia karibu mayai 600, hiki kikiwa ni kiwango cha wastani wa juu kuliko kile kinacholiwa nchini Uingereza, ambacho ni miligramu 225 kwa siku,” Tom Sanders anaeleza.
Katika takwimu za hivi karibuni kutoka IEC, kuanzia mwaka 2015, inaonyesha kuwa Marekani ni nchi ya tano kwa ulaji zaidi wa mayai duniani – huku kila mtu akila mayai 252 kwa mwaka.
Lakini nchi hiyo ina matatizo ya moyo ambayo husababisha asilimia 20 ya vifo.
Japan, ambako ulaji wa mayai unafikia kiwango cha mayai 328 kwa mtu, ilirekodi asilimia 11 pekee ya vifo.
“Ulaji wa mayai walau matatu hadi manne kwa wiki ni sawa,” Wanasema wataalamu nchini Uingereza.