27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

USIKUBALI KUDANGANYIKA KIRAHISI HIVYO! – 2

WAKATI fulani mwaka 2014, nikiwa kwenye semina yangu ya JS Love Talk iliyofanyika Sinza, jijini Dar es Salaam,  dada mmoja alisimama na kuuliza swali.

Alikuwa akizungumza kwa uchungu huku akimwaga machozi. Alikuwa kwenye maumivu makali ya kuachwa na mpenzi wake wa muda mrefu. Ni mwanaume ambaye alikuwa naye mapenzini kwa muda wa miaka mitatu.

Walifahamiana kwenye mtandao (Facebook), kila mmoja akajieleza kwa mwenzake na wote wakakubaliana kuwa wapenzi.

Anasema mpenzi wake huyo anaishi na kufanya kazi mjini Iringa, wakati yeye akiwa hapa jijini Dar es Salaam. Walifanyiana mengi kwenye mapenzi yao. Wakawa na ahadi kedekede.

Tatizo ni siku au tuseme wiki waliyokaa pamoja na kufahamiana. Dada huyo alikwenda Iringa kumuona mpenzi wake huyo kwa mara ya kwanza, lakini hakujua kuonana kwao ndiyo ilikuwa mwisho wa penzi lao.

Anasema: “Alinipokea vizuri sana. Akanipeleka nyumbani kwake Kihesa. Lakini hakuonekana kufurahia sana ujio wangu.

“Nililala naye na ilikuwa siku yangu ya kwanza kukutana naye kimwili. Akawa anaondoka asubuhi sana na kwenda kazini, kisha anarudi usiku wa saa tano wakati mwingine mpaka sita.

“Sikupata muda mwingi wa kuwa naye, baada ya siku tano nilirudi Dar nikiwa sijamjua vizuri yule bwana. Kutokea hapo, kila nikimpigia simu hapokei, nikimtumia meseji hajibu.

“Baadaye akanijibu kwa kifupi; kama hujui kusoma, hata picha huwezi kutazama? Sitaki mazoea tena na wewe, maana wewe siyo type yangu. Tangu hapo akawa hapokei tena simu yangu.

“Najua hanitaki tena, lakini bado nampenda sana, nashindwa kumuondoa kichwani mwangu, nimechanganyikiwa sana. Naomba msaada wako mwalimu.”

Nilizungumza naye pale, lakini pia baadaye nilizungumza naye zaidi chemba. Lakini kifupi niseme tu, mwanzo wa matatizo yote ni mapenzi ya kudanganyana kabla ya kuonana.

Wakati naanza mada hii wiki iliyopita, nilieleza kwa kifupi namna hali inavyokuwa wakati wa kuanzisha uhusiano wa kabla ya kuonana.

Hebu sasa tumalizie mada yetu, nikiamini kuwa mfano nilioanza nao hapo juu umekusaidia kukuongezea ufahamu.

 

MAPENZI YA HISIA

Kimsingi sababu ya haya yote ni hisia tu. Njia ya mawasiliano inaweza kukoleza au kuimarisha uhusiano ambao tayari upo. Mfano kama unaishi Moshi na mpenzi wako yupo Mwanza, mnaweza kuboresha uhusiano wenu kwa kuwasiliana kwa njia ya simu, waraka pepe na mitandao ya kijamii.

Kinachotokea kwa marafiki wapya ambao wanahisi tayari ni wapenzi na wanapendana ni zile hisia za ndani zinazowaingia wakati wa mawasiliano yao. Pengine walianza kuzungumzia mambo ya mapenzi na kujikuta wakitamani kuwa karibu.

Jambo kubwa zaidi ni kwamba mhusika hutawaliwa zaidi na hisia, maana kwa sababu hawafahamiani, watakuwa wanauliza; ‘Wewe ukoje? Mrefu, mfupi, mwembamba, mnene au?’ halafu mwenzake atamjibu, ‘mrefu kiasi, si mnene sana, kifupi nina umbo namba nane…navutia na ni maji ya kunde’.

Kifupi mtu anaweza kujielezea vyovyote atakavyo, hivyo kumfanya mwenzake amtengeneze ajuavyo kichwani mwake na kujihakikishia kwamba anampenda kwa dhati mwenzake kumbe anajidanganya! 

 

TABIA BANDIA

Mbaya zaidi ni kwamba, wakati wapenzi hawa wanaojidanganya wakiendelea kuwasiliana si rahisi kujuana vizuri kitabia kwa sababu wengi huonesha tabia bandia. Mambo yao ya ndani wanayaficha kwa nguvu na kuonesha mema tu.

Hapo ndipo mwanzo wa penzi feki kwa kudanganyika na tabia za kutengeneza.

 

HULKA MBAYA

Kuna wengine ni tabia zao za asili. Amezoea kupata wapenzi kwa kupitia kwenye simu na mitandao ya kijamii. Usishangae kuna wengine wanapiga namba hata wasizozijua, akikutana na mtu wa jinsia tofauti na yake, anaanza mambo yake. Akimaliza haja zake anakuacha!

 

ACHA KUJIDANGANYA

Ni vizuri sasa ukatoka kwenye ulimwengu wa giza na kurudi kwenye ulimwengu unaonekana. Kwa hakika ni vigumu sana kumpenda mtu ambaye hujamuona, labda kama unataka kucheza na muda wako.

Wako anakuja, vuta subira ukifanya mambo yako kwa usahihi. Usijidanganye na matapeli wa mapenzi. Wapo ambao baadhi ambao wanafanikiwa kuingia kwenye mapenzi lakini mwisho wao hauwi wenye mafanikio.

Penzi la dhati hubebwa na vitu vingi sana, ukiachana na UPENDO kuna suala la tabia na mengine mengi ambayo huwezi kuyajua kwa njia ya kuwasiliana pekee.

Utajihakikisha umempenda kwa kumtengeneza kichwani mwako, mwisho wa siku unakutana na mtu ambaye yupo tofauti na mawazo yako, itakuwaje hapo? Fikiri zaidi.

Je, unapenda kujifunza masomo haya zaidi kupitia group la WhatsApp la Love Moment? Kama ndivyo karibu inbox, andika ujumbe wako ukitaka kujiunga na kundi hilo, nasi tutakuunganisha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles