RATIFA BARANYIKWA Na MASHIRIKA YA HABARIÂ
URUSI imeingia kwa mara nyingine tena kwenye vita ya kidiplomasia na mataifa ya magharibi baada ya mpinzani wa rais Vladimir Putin wa nchi hiyo, Alexey Navalny kudaiwa kupewa sumu kwenye chai akiwa uwanja wa ndege na kupoteza fahamu hadi sasa ikiwa ni wiki mbili.
Sumu hiyo inayofahamika kama Novichok ambayo inaathiri neva inaelezwa imekuwa ikitumiwa na Urusi tangu enzi za kisovieti kama moja ya silaha zake maangamizi.
Tangu wakati huo Urusi imekuwa katikati ya matukio na pengine visa vingi vinavyotajwa kuwa ni sumu dhidi ya yeyote anayeonekana kuwa adui yake.
Ingawa Urusi imekuwa ikikana lakini tukio la sasa dhidi ya Navalny limekumbusha orodha ya watu kadhaa wakiwamo majasusi wanaodaiwa kuwahi kupewa sumu na Serikali ya Urusi na wengi wao waliishia kupoteza maisha.
Alexander Litvinenko
Miongoni mwa waliowahi kukumbwa na dhahama hiyo ni Alexander Litvinenko, huyu aliwahi kuwa wakala wa Shirika la Kijasusi la Urusi linalofahamika kama Komitet Gosudarstvennoy Bezopasnosti, au Kamati ya Taifa ya Usalama zaidi inajulikana kama KGB na hapo kabla enzi za kisovieti akiwa Federal Security Service (FSB).
Ajenti huyo wa zamani wa KGB, Luteni Kanali Alexander Litvinenko alihitilafiana na Urusi mwaka 2000 na kukimbilia Uingereza, ambapo miaka sita baadae yaani 2006 aliugua vibaya baada ya kunywa chai iliyowekwa sumu kali ya Poloniamu-210.
Alexander Litvinenko ambaye kwa alijilinda vikali dhidi ya mashambulio yeyote tangu alipokosana na Urusi hadi pale alipokuja kujikwaa kwa kunywa chai alipoteza maisha baada ya wiki tatu.
Uchunguzi wa Uingereza ulibaini kuwa maajenti wa Urusi walikuwa wamemuua Litvinenko, labda kwa idhini ya Rais Vladimir Putin. Urusi ilikana kuhusika.
Kabla ya kifo chake, Litvinenko aliwaambia Waandishi wa habari kwamba FSB bado ilikuwa ikiendesha maabara ya siri ya sumu ya Urusi tangu enzi za Kisovieti.
Anna Politkovskaya
Mwingine aliyewahi kuingia kwenye rekodi za sumu ni Mwandishi wa habari za uchunguzi, Anna Politkovskaya ambaye alikuwa ameandika kwa kukosoa kuhusu unyanyasaji uliokuwa ukifanywa na Urusi pamoja na vikosi vya Chechenya vilivyokuwa vikiungwa mkono na Urusi vilivyokuwa vikipambana na wapiganaji wa Chechnya.
Ni andiko lake hilo ndilo lililomfanya ajikute akiingia kwenye vitisho vya kifo mara kwa mara.
Mwaka 2004, aliugua vibaya na kupoteza fahamu kwa namna na staili ile ile ya kunywa chai.
Alisema alikuwa amewekewa sumu kwa makusudi kumzuia kuripoti kutekwa kwa shule mwaka 2004 kusini mwa Urusi na wapiganaji wa Chechenya.
Miaka miwili baadae, Anna alipigwa risasi na kufa akiwa nyumbani kwake Moscow nchini Urusi.
Mauaji hayo yaliibua vita kali ya kidiplomasia kama ilivyo sasa kati ya Urusi na nchi za Magharibi.
Wanaume watano walihukumiwa kifungo jela kwa mauaji hayo lakini hakuna yeyote aliyekutwa na hatia kwa kuagiza mauaji hayo yafanyike
Vladimir Kara-Murza
Mwanaharakati wa upinzani Vladimir Kara-Murza Jr naye alilazwa kwa dalili za kupewa sumu mara mbili, mwaka 2015 na 2017.
Mwandishi wa habari na mshirika wa kiongozi wa upinzaji wa Urusi Boris Nemtsov, ambaye alipigwa risasi na kuuawa mwaka 2015 wakati akivuka daraja karibu na Kremlin, Mikhail Khodorkovsky, mpinzani huyo aliyegeuka mpingaji wa tukio hilo Kara-Murza alikaribia kufa kutokana na figo kutofanya kazi.
Ilishukiwa kuwa alipewa sumu kwa sababu madaktari hawakubaini sababu nyingine yeyote.
Alichukuliwa na kupelekwa hospitali kwa hali ile ile ya kuumwa mwaka 2017 na kukosa fahamu kwa maana nyingine akiwa mahututi.
Mke wake alisema madaktari walithibitisha kuwa alipewa sumu.
Kara-Murza alinusurika, na polisi walikataa wito wa kuchunguza tukio lake kwa mujibu wa mwanasheria wake.
Sergei na Yulia Skripal
Jasusi wa Urusi ambaye alikuwa akiifanyia kazi Uingereza (double agent), Sergei Skripal mwenye umri wa miaka 69 naye aliugua vibaya akiwa Uingereza katika jiji la Salisbury mwaka 2018.
Mamlaka zilisema kuwa Skripal na binti yake mkubwa, Yulia mwenye umri wa miaka 36, walipewa sumu hiyo inayoua mishipa ya fahamu Novichok. Binti huyo na baba yake walitumia majuma kadhaa wakiwa katika hali mbaya.
Uingereza ilipeleka lawama moja kwa moja kwa majajusi wa Urusi lakini nchi hiyo ilikana kuhusika kwa lolote.
Uingereza iliwahukumu wanaume wawili wa Kirusi kwa sumu hiyo, ilidai kuwa walitembelea Salisbury kama watalii ingawa wenyewe walikana kuhusika kwa shambilio lolote, tukio hilo lilikuja wakati nchi hiyo ikidaiwa kuhusika kuingilia kampeni za urais za Marekani mwaka 2016.
Pyotr Verzilov
Pyotr Verzilov, ambaye anatoka kundi la waandamanaji la Urusi la ‘Pussy Riot’ aliwekwa chumba cha uangalizi maalumu (UCU) baada ya kudaiwa kupewa sumu mwaka 2018 na alisafirishwa hadi Berlin, Ujerumani, kwa matibabu.
Madaktari wa Ujerumani waliokuwa wakimtibu walisema sumu alibainika dhahiri kwa bahati nzuri alipona.
Verzilov, na mpenzi wake pamoja na wafuasi wawili wa Pussy Riot walikuwa wamepelekwa jela hapo kabla kwa kosa la kuvuruga Kombe la Dunia lililofanyika Urusi.
Wenyewe walikuwa wakipinga nguvu kubwa iliyokuwa ikitumiwa na Polisi wakati huo wa Kombe la Dunia la Mpira wa Miguu.
Ametumikia kifungo kingine ambacho mwenyewe alikiita kwamba kilikuwa na shinikizo la kisiasa.
TUKIO LA ALEXEY NAVALNYÂ
Juzi Jumuiya ya Kujihami (NATO),ilikutana kwa ajili ya kujadili tukio la Navalny baada ya madaktari wa Ujerumani kuthibitisha kuwa amepewa sumu.
Nato imetoa msimamo mkali dhidi ya Urusi huku mataifa ya makubwa yakionekana kuchukizwa na kitendo hicho.
Katibu Mkuu wa Nato, Jenerali Jens Stoltenberg amesema kuna ushahidi usio na shaka kwamba mpinzani wa Urusi, Alexey Navalny amepewa sumu inayofahamika kama Novichok ambayo inaathiri neva.
Nato imeielekeza Urusi kushirikiana katika uchunguzi utakaoongozwa na taasisi ya kuzuia silaha za kemikali (OPCW).
“Matumizi yeyote ya silaha za kemikali ni yanaonyesha kutoheshimu maisha ya binadamu, na hayakubaliki,” Stoltenberg aliwaambia waandishi wa habari.
Awali Ujerumani ambako mwanasiasa huyo wa upinzani nchini Urusi, Alexei Navalny anatibiwa ilisema kuna ushahidi ulio dhahiri kuwa alipewa sumu ya Novichok.
Urusi kwa upande wake imejitetea ikisema nchi za magharibi hazipaswi kufanya pupa ya kuihukumu juu ya kutiliwa sumu mpinzani wa serikali ya nchi hiyo, Navalny.
Mazungumzo katika nchi za magharibi juu ya kuiadhibu Urusi yanapamba moto.
Urusi ilitoa kauli hiyo siku moja baada ya Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel kusema kuwa pamekuwapo na jaribio la kumuua Navalny kwa kumtilia sumu aina ya Novichok ambayo ilitengenezwa tangu enzi za kisovieti.
Sumu hiyo inaathiri mishipa ya fahamu na tangu tukio hilo dhidi ya Navalny takribani wiki mbili zilizopita hajaamka katika kitanda cha hospitali nchini Ujerumani hadi sasa.
Umoja wa Ulaya umesema unaweza kuweka vikwazo dhidi ya Urusi.
Nato iliitisha kikao cha haraka juzi kujadili uchunguzi wa madaktari wa Ujerumani uliothibitisha kwamba Navalny ametiliwa sumu.
Shirika la kudhibiti matumizi ya Silaha za Sumu OPCW limeelezea wasiwasi mkubwa baada ya Ujerumani kusema kiongozi huyo wa upinzani nchini Urusi, Navalny alipewa sumu hiyo aina ya Novichok.
Hata kabla ya kauli ya Nato, Mkuu wa OPCW, Fernando Arias amesema shirika hilo lenye makao yake mjini The Hague lilikuwa tayari kusaidia taifa lolote mwanachama atakayehitaji msaada wake.
Ikulu ya Urusi kupitia msemaji wake, Dmitry Peskov alisema Ujerumani haijatoa uthibitisho na kuongeza kuwa hakuna sababu ya kulituhumu taifa hilo, lakini pia akikataa mazungumzo kuhusiana na vikwazo vya kiuchumi huku akiyataka mataifa ya magharibi kutokimbilia kuwahukumu.
Ujerumani inasisitiza kuwa Navalny alipewa sumu ya jamii ya Novichok, sawa na ile iliyotumika dhidi ya jasusi wa zamani wa Urusi na Uingereza, Sergei Skripal pamoja na binti yake katika mji wa Salisbury nchini Uingereza miaka miwili iliyopita, hatua iliyoibua mivutano mikali na kushinikiza uchunguzi zaidi.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ameyarudia matamshi yake kwamba hatua yoyote itakayochukuliwa na Ujerumani ama Umoja wa Ulaya kuhusiana na ufichuzi huo, itategemeana na iwapo Urusi itasaidia kuondoa kiwingu kilichopo.
Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari pamoja na Waziri Mkuu wa Sweden, Stefan Loefven mjini Berlin, Merkel amesema hana la kuongeza baada ya taarifa aliyoitoa kuhusiana na jaribio hilo la kumuua Navalny.
” Bila shaka ninafuatilia kinachoelezwa, lakini ninapenda kusema kwamba siku ya jana nilitoa msimamo wa wazi kuhusu kile tutakachokifanya sasa na siku zijazo. Na kwa hakika, inategemea sana namna serikali ya Urusi itakavyojibu. Lakini sina cha kuongeza kwenye maneno yangu ya jana,” alisema Merkel.
Rais wa Belarus, Alexander Lukashenko amedai kwamba vikosi vyake vya usalama vimeingilia mazungumzo ya simu ya Ujerumani na kuonyesha kwamba madai hayo yalikuwa ni ya uongo.
Lukashenko amemwambia Waziri Mkuu wa Urusi, Mikhail Mishustin aliyeko ziarani mjini Minsk kwamba mawasiliano ya simu kati ya Berlin na Warsaw yalionyesha tukio hilo lilikuwa na kutunga.
Aliwanuukuu wazungumzaji aliodai walisema “Wamefanikisha, ili kumvunja moyo Rais Vladmir Putin wa Urusi ili asiendelee kujiingiza kwenye masuala ya Belarus. Hata hivyo hakufafanua zaidi.
Uingereza kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Dominic Raab, imesema Urusi ina swali zito la kujibu kuhusiana na madai hayo na ameahidi kuisaidia Ujerumani na washirika wengine wa kimataifa kuhusiana na suala hilo.
Uingereza ambayo imehusisha tukio la kupewa sumu mpinzani huyo na lile la jasusi wake nayo ilikutana kwaajili ya suala hilo.
Mgogoro wa sasa wa kidiplomasia unapamba moto ikiwa miezi kadhaa sasa tangu Urusi ikanushe madai ya kuhusishwa na shambulizi hilo dhidi ya Sergei Skripal pamoja na binti yake Yulia, kusini magharibi mwa Uingereza.
Skripal ofisa wa zamani wa kijasusi aliyewahi kufungwa jela kwa kuuza siri za Urusi kwa Uingereza, alihamia Uingereza mwaka 2010 na kuishi katika mji waSalsbury nchini humo.
Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, Theresa May alilieleza Bunge wakati huo kuwa inaelekea kwa kiwango kikubwa Urusi ilikuwa nyuma ya tukio hilo na kutaka ijibu haraka.
Wakati huo kama ilivyo sasa Marekani na Nato zote zilitoa taarifa kuiunga mkono Uingereza.
SUMU YA NOVICHOK
Sumu hii inaelezwa kuwa ilitengenezwa wakati wa Muungano wa Kisovieti
Kwa mujibu wa makala iliyochapishwa na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) Novichok maana yake ni “mgeni” kwa lugha ya Kirusi.
Ni jina linalotumiwa kurejelea kemikali za sumu ambazo hushambulia mfumo wa neva mwilini.
Kemikali hizo ziliundwa na Muungano wa Usovieti miaka ya 1970 na 1980.
Kwa mujibu wa BBC sumu hizo zilifahamika kama silaha za kemikali za kizazi cha nne na zilistawishwa chini ya mpango wa silaha za Muungano wa Usovieti uliofahamika kama “Foliant”.
Mwaka 1999, maofisa wa ulinzi kutoka Marekani walisafiri hadi Uzbekistan kusaidia kuvunja na kusafisha moja ya eneo kubwa zaidi lililotumiwa kufanyia majaribio silaha za kemikali na Muungano wa Usovieti.
Kwa mujibu wa ofisa mmoja wa ngazi za juu ambaye alitorokea Marekani, maofisa wa Usovieti walitumia kiwanda kilichokuwa eneo hilo kuunda na kufanyia majaribio sampuli za kemikali ya Novichok.
Kemikali hii iliundwa mahsusi kutoweza kugunduliwa na wakaguzi wa silaha na sumu katika mataifa mengine.
Sumu hiyo pia inatajwa kuwa yenye nguvu kuliko sumu nyingine
Moja ya kemikali hizi zinazofahamika kama Novichok – A-230 – inadaiwa kuwa na nguvu mara 5-8 zaidi ya sumu nyingine hatari inayofahamika kwa jina VX.
“Hii ni sumu hatari na changamano kushinda sumu aina ya sarin au VX na pia huwa vigumu zaidi kuitambua,” anasema Prof Gary Stephens, mtaalamu wa kemikali katika Chuo Kikuu cha Reading.
Sumu ya VX ndiyo iliyotumiwa kumuua ndugu wa kambo wa kiongozi wa Korea Kaskazini Kim Jong-un mwaka jana, kwa mujibu wa Marekani.
Aina mbalimbali za kemikali hii ya A-230 zimekuwa zikitengenezwa, na aina moja inadaiwa kuidhinishwa na jeshi la Urusi itumike kama silaha ya kemikali.
AINA MBALIMBALI ZA NOVICHOK
Inaelezwa ingawa baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok huwa majimaji, kuna aina nyingine ambazo ni yabisi (gumu au isiyokuwa majimaji).
Ni kemikali ambayo pia inaweza kugeuzwa kuwa poda laini.
Kwa mujibu wa andilo lililochapishwa na BBC, baadhi ya sumu hizi pia hudaiwa kutumiwa kama “silaha za ngazi mbili”.
Hii ina maana kwamba sumu hii huhifadhiwa mara nyingi kama kemikali aina mbili ambazo zikiwa kando kando si hatari. Zinapochanganywa, huingiliana na kutengeneza sumu.
Hii huifanya rahisi sana kwa viungo vya kemikali hii kusafirishwa kwani huwa sumu tu zikichanganywa.
“Moja ya sababu ambayo hufanya sumu hizi kuandaliwa ni kwa sababu viungo vyenyewe havijapigwa marufuku,” anasema Prof Stephens.
“Hii ina maana kwamba kemikali hizi ambazo huchanganywa huwa rahisi sana kusafirishwa bila kuwa hatari kwa anayezisafirisha.”
Kemikali hizo zikichanganywa inaelezwa zinaweza kuathiri mtu haraka sana
Inaelezwa mtu anapovuta sumu ya Novichok, au hata ikigusa ngozi yake, basi huanza kumuathiri upesi.
Dalili zake zinaweza kuanza kujionesha katika kipindi cha muda mfupi hivi, sekunde 30 hadi dakika mbili.
Dalili zake zinaelezwa kuwa ni sawa na za sumu nyingine za neva kwamba hata
Madhara yake ni sawa na ya sumu nyingine zenye kushambuliwa mfumo wa neva.
Hii ina maana kwamba huwa zinafanya kazi kwa kuzuia ujumbe au mawasiliano kati ya mfumo wa neva na misuli, na pia kusambaratisha shughuli nyingi muhimu za mifumo mwilini.
Dalili zake ni pamoja na macho kuwa na rangi nyeupe, huku mboni za macho zikisinyaa, na mtu kuonekana kupumbaa. Wakati mwingine, mtu hupoteza fahamu, kushindwa na kupumua na kufariki.
Sumu hizi kimsingi hufanya moyo kupunguza mapigo yake na kubana njia zinazotumiwa na mwili kupumua na mwishowe mtu kufariki kutokana na mtu kukosa hewa ya kutosha.
Baadhi ya aina za sumu hii ya Novichok zimeundwa mahsusi kuhakikisha dawa za kawaida za kupoza nguvu ya sumu haziwezi kufanikiwa.
HUDUMA YA KWANZA ALIYEPEWA NOVICHOK
Iwapo mtu amepewa sumu hii, inashauriwa avuliwe haraka mavazi yake na ngozi yake ioshwe maji na sabuni.
Macho yake pia yaoshwe kwa maji na apewe hewa ya oksijeni.