Mwandishi Wetu -Zanzibar
HEKAHEKA za kupata mrithi wa Rais wa Zanzibar wa awamu ya nane, zimepamba moto baada ya makada wa chama hicho wanaowania nafasi hiyo kufikia 29, huku Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM, Pereira Ame Silima, akijitosa kwenye kinyang’anyiro hicho na kuzidi kupandisha joto.
Hatua hiyo sasa inaelekea kufikia rekodi ya waliokuwa wanaomba kuteuliwa na CCM kuwania urais mwaka 2015 kwa chama hicho upande wa Jamhuri ya Muungano, ambayo ilifikia 42.
Jana Peirera Ame Silima alikuwa mgombea wa 27 kuchukua fomu ya kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya CCM.
Mbali na Silima, wengine waliochukua fomu ya kuwania urais kupitia CCM jana ni Iddi Hamad Idd na Shaame Silima Mcha.
Kuchukua fomu kwa Silima ambaye amewahi kushika nafasi mbalimbali katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) pamoja na ya muungano, kumepandisha upya joto la kutafuta mtu atakayepeperusha bendera ya CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.
Nafasi ambazo Silima amewahi kushika ndani ya SMZ ni Katibu Mkuu wa Wizara za Biashara Masoko na Utalii, Kilimo, Mifugo na Maliasili na tangu Machi 2017 hadi sasa amekuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM. Kwa sasa ni Katibu wa Oganaizesheni ambayo ndiyo idara inayoratibu masuala yote ya uchaguzi.
Akizungumza mara baada ya kukabidhiwa fomu ndani ya Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar, Silima alisema kikubwa kilichomsukuma kugombea ni nia yake thabiti ya kukuza uchumi wa wananchi wa Zanzibar.
Alisema kuwa licha ya viongozi waliopo na waliotangulia kufanya kazi nzuri, ameona kuna changamoto katika ukusanyaji mapato ya ndani na kwamba kasi yake haiendani na uwezo wa kuzalisha.
“Nchi inahitaji maendeleo ya kiuchumi yatakayochagiza ukuaji kipato cha taifa na mwananchi mmojammoja, lakini sasa kipato cha wananchi ni kidogo na hivyo wengi kuangukia kwenye umaskini. Nikipata ridhaa ya kuongoza nitahakikisha taifa linapiga hatua kimaendeleo,” alisema Silima.
Kuhusu kuongeza wigo wa ukusanyaji kodi, Silima ambaye pia ni mtaalam wa masuala ya usimamizi wa fedha na biashara za kimataifa alisema Zanzibar kwa sasa inategemea sekta za utalii na bahari kukuza mapato jambo ambalo linahitaji kufanyiwa maboresho zaidi.
“Uchumi wa Zanzibar unategemea sekta chache ikiwamo utalii na uchumi wa bahari ambao haujawekezwa ipasavyo, hivyo kama nitachaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar jukumu langu la kwanza litakuwa kuhakikisha kunakuwa na miundombinu ya kutosha ya kukuza uchumi,” alisema.
Akizungumzia umoja wa kitaifa alisema kwa sasa Zanzibar inahitaji jamii yenye umoja kuliko iliyopo sasa katika upatikanaji wa huduma muhimu kama elimu bora, afya na maji, yaani asiwepo wa kumwogopa mwenzake kwa sababu yoyote ile.
“Baadhi ya wanasiasa walitugawa Wanzanzibari kutokana tu na itikadi za kisiasa hadi kufikia watu kuogopana, katika zama zangu kila mtu atakuwa huru kufanya vile atakavyo katika misingi ya kisiasa au kidini ili mradi tu havunji sheria za nchi,” alisema Silima.
Kwa upande wa ustawi wa jamii Ame Silima alisema atatumia uzoefu wake kuhakikisha Zanzibar inakuwa na mkakati maalum wa kukomesha vitendo vya unyanyasaji wa watoto na wanawake.
Pereira Ame Silima aliyezaliwa miaka 61 iliyopita. Aliwahi kutunukiwa tuzo ya mwanafunzi bora wa shahada ya kwanza ya misitu kwa miaka mitatu mfululilizo. Pia ana shahada ya uzamili (MSC) ya mipango ya usimamizi wa misitu (1991) kutoka Chuo Kikuu cha Helsinki, Finland.
Makada ambao wamekwisha kurejesha fomu zao ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Hussein Mwinyi, Balozi Ali Karume, Mohammed Hija Mohammed, Mbwana Bakari Juma, Abdulhalim Mohammed Ali na Hamis Mussa Omari, ambapo sasa wanasubiria hatua inayofuata ya uchujaji ili kupata idhini ya kuingia katika mchakato wa kumrithi Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, anayemaliza kipindi cha uongozi wake wa miaka 10 tangu achaguliwe mwaka 2010.
Juni 15 mwaka huu ndiyo ilikuwa siku ya kwanza ya uchukuaji fomu ya kuomba kuteuliwa kuwa mgombea wa CCM katika uchaguzi wa mwaka huu. Waliofungua dimba ni mtoto wa Rais wa Kwanza wa Zanzibar, Balozi Karume na Bakari Juma.
Waliochukua fomu mpaka sasa ni Mbwana Bakari Juma, Ali Abeid Karume, Mbwana Yahya Mwinyi, Omar Sheha Mussa, Dk. Hussein Ali Mwinyi, Shamsi Vuai Nahodha, Mohammed Jaffar Jumanne, Mohammed Hijja Mohammed, Meja Jenerali Issa Suleiman Nassor na Prof. Makame Mnyaa Mabarawa.
Wengine ni Mwatum Mussa Sultan, Haji Rashid Pandu, Abdulhalim Mohammed Ali, Jecha Salum Jecha, Dk Khalid Salum Mohammed, Rashid Ali Juma, Khamis Mussa Omar, Mmanga Mjengo Mjawiri, Hamad Yussuf Masauni, Mohammed Aboud, Bakar Rashid Bakari, Hussein Ibrahim Makungu, Ayoub Mohammed Mahmoud, Hashim Salum Hashim pamoja na Hasna Attai Masoud.
Hata hivyo, pamoja na kuwa na wingi wa wagombea ambao wanavunja rekodi ya mwaka 2010 ambapo kulikuwa na wagombea 11 pekee waliokuwa wakitaka kumrithi Aman Abeid Karume, safari hii kumekuwa na mwamko mkubwa wa makada wa CCM kuomba nafasi ya uteuzi wa CCM ili kuwania urais wa Zanzibar.
URAIS BARA 2015
Mwaka 2015 makada wa CCM walikuwa kwenye sintofahamu kama inayotokea sasa kwa upande wa Zanzibar, ambapo waliochukua fomu walikuwa makada 42.
Kati ya wanachama hao, 38 ndiyo waliorudisha fomu ya kuwania nafasi hiyo waliomba kupeperusha bendera ya chama hicho.
Miongoni mwao makada waliowania urais CCM mwaka 2015, lakini walijikuta wakikwaa kisiki kwenye uteuzi wa kupata mtu mmoja ni pamoja Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ambaye sasa amevuliwa uanachama CCM, Bernard Membe na marehemu Samuel Sitta.
Aliyekuwa Waziri wa Ujenzi, Dk John Pombe Magufuli alifanikiwa kuteuliwa na vikao vya chama hicho kuwa mgombea urais.
Ikulu kuna biashara gani huko? Mbona wanapakimbilia?