Serikali imesema hali ya upatikanaji dawa nchini imeimarika kutoka asilimia 45 hadi kufikia asilimia 86.3 Julai, mwaka huu.
Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amesema hayo leo wakati akifungua Kongamano la 49 la Afya lililoandaliwa na Chama cha Madaktari Tanzania (MAT).
Mama Samia amewataka waganga wakuu wa mikoa na wilaya kutoa taarifa za hali ya upatikanaji wa dawa kwa wananchi katika maeneo yao.
“Lakini pia mnatakiwa kuanzisha mifuko ya dawa katika maeneo yenu ili kuimarisha hali ya upatikanaji dawa,” amesema.
Hata hivyo, wakizungumzia wagonjwa wanaopelekewa nje ya nchi kwa matibabu amesema idadi yao kwa ufadhili wa serikali imepungua kutoka wagonjwa 423 mwaka 2015/16 hadi 203 mwaka 2016 /17 sawa na asilimia 47.9.
Amesema hali hiyo inatokana na hatua zilizochukuliwa na Serikali kuboresha na kuanzisha baadhi ya huduma za upasuaji ambazo awali hazikuwapo nchini.