Na VERONICA ROMWALD – DAR ES SALAAM
OKTOBA 12, kila mwaka huwa ni Siku ya Macho Duniani, Tanzania iliungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha siku hiyo ambayo kwa mwaka huu ilipewa kauli mbiu isemayo: ‘Afya ya Macho kwa Wote, Thamini Uoni wa Jicho.’
Lengo la maadhimisho ya siku hiyo ni kuhamasisha jitihada za kutokomeza upofu unaozuilika duniani. Uamuzi wa kuadhimisha siku hiyo ulifikiwa na Lions Club International Foundation mwaka 1998.
Baadae yaliungwa mkono na wadau wengine likiwamo Shirika la Afya Duniani (WHO), Muungano wa Mashirika ya Kimataifa yanayojihusisha na Huduma za Macho (IAPB), Serikali za nchi mbalimbali, wataalamu wa afya na watu binafsi.
Ni maadhimisho mahususi yenye lengo la kuhamasisha utekelezaji wa Dira ya Kimataifa ya Kutokomeza Upofu unaozuilikaDuniani ifikapo mwaka 2020 kwa kuthamini haki ya kuona kwa wote.
Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu anasema Serikali iliridhia na kuungana na mataifa mengine duniani katika kutekeleza azimio hilo Mei 23, 2003.
Kwa mujibu wa Ummy, inakadiriwa kuwa takribani watu milioni 285 duniani wana matatizo ya kutokuona na kwamba kuna ongezeko kubwa la matatizo ya kutokuona duniani ambayo asilimia 80 ya hayo yangeweza kuzuilika.
Daktari
Asha Mweke ni Mtaalam wa Macho (Optometria) katika Taasisi ya Letasi Eye and Optical Center iliyopo jijini hapa, anasema ni kweli kwamba matatizo ya macho yanaweza kuzilika iwapo watu wajajenga utamaduni wa kupima mara kwa mara.
“Tatizo tunaona kuna changamoto, wengi hawana mwamko wa kujitokeza mapema kufanya uchunguzi wa afya ya macho, kutokana na hali hiyo wengi huja hospitalini wakati tatizo likiwa limeshakuwa kubwa, wamechelewa,” anabainisha.
Kundi la wanafunzi
Mweke anasema kundi la wanafunzi ndilo ambalo linaonekana kuathiriwa zaidi na hali hiyo, huku akitolea mfano namna walivyoweza kuwabaini wengi baada ya kufanya upimaji bila malipo katika kituo chao.
“Tuliwaalika kituoni kwetu hivi karibuni wakati shule zilipokuwa zimefungwa na tukawafanyia uchunguzi bila malipo, tuliwapima wanafunzi 120 kati ya hao 90 tuliwakuta na matatizo mbalimbali hasa ya uoni hafifu,” anabainisha.
Anaongeza: “Wengi hawakuwa wanajitambua kama wana matatizo ya macho, kila tuliyemuhoji alisema alijua kule kuwasha washa, wekundu kwenye macho na au kutoka tongo tongo ni hali ya kawaida.
“Zile ni ishara au dalili zinazokuonesha kwamba macho yako yana tatizo kwa hiyo unapoona ishara yoyote kati ya hizo ni muhimu ukawahi hospitalini na kuwasiliana na mtaalamu wa macho ili ufanyiwe uchunguzi mapema,” anasema.
Undani wa tatizo
Mtaalamu huyo anasema kitaalamu tatizo la uoni hafifu limegawanyika katika aina kuu tatu.
“Kuna ambao wanasumbuliwa na tatizo la uono hafifu wanapokaa kwa karibu, wapo wenye uono hafifu pindi wanapokaa kwa mbali na kuna ambao wana huoni hafifu wa kutokuona pindi wanapokaa mbali na hata karibu.
“Lakini tatizo hili linatibika na mara nyingi ni kwa kuvaa miwani, kwa wale ambao wamechelewa kupata tiba,” anabainisha.
Anasema watu wenye tatizo la uoni hafifu kwa karibu mara nyingi huwa wanapata maumivu makali ya kichwa na wengi hulalamika wanapopita kwenye eneo lenye mwanga hudai unawaumiza.
“Kutokana na hali hiyo utaona mtu mwenye tatizo anapofika kwenye mwanga mkali anakuwa anafinya macho yake kwa sababu huhisi maumivu makali,” anasema.
Lishe ni tiba mbadala
Anasema pamoja na matibabu wanayotoa ikiwamo kutumia miwani kutibu tatizo, lakini pia linaweza kutibika iwapo mtu atapata lishe bora.
“Wapo wanafunzi ambao wanakuja hospitalini kwetu wakilalamika macho yao yanauma, lakini tunapowafanyia vipimo tunakuta hawana tatizo lolote, kumbe hali hiyo inawapata kutokana na kukosa lishe bora,” anasema.
Wengi wanapenda maharagwe
Mtaalamu huyo anasema kwa kawaida watoto wengi hupendelea kula mboga ya maharagwe ambayo kimsingi ina protin kwa wingi.
“Maharagwe si mboga mbaya, ni nzuri kwani ina protin kwa wingi ambayo huhitajika mwilini lakini tunahamasisha waanze kupenda kula mboga mboga (za majani) zile zina virutubishi vingi vya Vitamin A ambavyo ni muhimu kwani husaidia kulinda afya ya macho,” anasema na kuongeza:
“Mwili unapokosa virutubisho vya vitamin A mtu huwa kwenye uwezekano mkubwa wa kupata tatizo la uoni hafifu na matokeo yake hujikuta akipata upofu katika maisha yake hapo baadae.
Uoni hafifu na ufaulu duni
Juma Faustine ni mwanafunzi wa darasa la pili katika Shule ya Msingi Bunju A, anasema kwa muda mrefu amekuwa akisumbuliwa na tatizo la macho.
“Huwa nikikaa mbali na ubaoni siwezi kuona vizuri, nilimweleza mwalimu wangu juu ya jambo hilo akanihamishia katika dawati la mbele lakini bado siwezi kuona sawa sawa,” anabainisha.
Mwalimu Mkuu Msaidizi wa shule hiyo, Diana Felix anasema tatizo la uoni hafifu huchangia kwa namna moja au nyingine kushusha kiwango cha ufaulu kwa mwanafunzi husika.
“Kwa mfano mwaka jana jumla ya wanafunzi 400 waliandikishwa kuanza darasa la kwanza, ambao tumewagawa katika madarasa manne kila moja likichukua takribani wanafunzi 90,” anasema.
Anasema katika hali ya kawaida ikiwa mtoto anakabiliwa na tatizo la uoni hafifu halafu akakaa umbali mrefu kutoka usawa wa ubao ni dhahiri hataweza kuona kile ambacho mwalimu ameandika ubaoni.
“Wapo ambao huwa wawazi kwa walimu na kueleza kwamba hawaoni basi hapo mwalimu husika huchukua hatua ama ya kumuhamisha kuja kukaa mbele jirani na ubao.
“Changamoto ni kwamba si wote ambao husema, wengi huwa waoga hivyo huamua kunakili kwa wenzao, sasa ikiwa mwenzake hajanakili vizuri ubaoni maana yake ni kwamba wananakili makosa ya wenzao,” anasema.
Anasema kutokana na hali hiyo, wanapopatiwa mtihani hujikuta wakifanya vibaya kwani walinakili kitu ambacho si sahihi.
“Pamoja na idadi kubwa ya wanafunzi kwani inakuwa vigumu mwalimu kumfikia kila mmoja na kujua iwapo ana tatizo au la,” anasema.
Ushiriki wa wazazi kikwazo
Mwalimu huyo anasema changamoto nyingine ni ushirikiano mdogo wa wazazi.
Anasema: “Wengi ni wazito kufuatilia maendeleo ya mtoto, hatuwaoni kuja kuuliza maendeleo ya watoto wao na hata inapotokea mtoto mmebaini ana tatizo tunapowaita huwa hawaji, inakuwa inatupa wakati mgumu mno.
“Hapa kuna watoto wanaishi na Virusi vya Ukimwi lakini wazazi hawapo wazi, hata kutudokeza walimu wakuu, wazazi wanasema tu mtoto anaumwa lakini hasemi anaumwa nini lakini walimu tunaelewa tunapowaangalia tunajua watoto wana matatizo.
“Kwenye suala la afya ni changamoto nyingine, mtoto unamuona ana afya duni, labda analalamika ana maumivu ya kichwa hata wiki nzima lakini anakuja na kukueleza amepatiwa dawa ya kutuliza maumivu basi, hakupelekwa hospitalini kuchunguzwa afya yake. Kwa kweli ushirikiano ni mdogo mno.”
Anasema hiyo inachangia kushusha kiwango cha maendeleo mazuri ya mwanafunzi.
“Yupo mwanafunzi hapa (anamtaja) afya yake si nzuri kwa sasa hata shule hawezi kuja, wenzake walienda kumtembelea hivi karibuni, anasema ameenda hospitalini amepewa dawa ambazo anazitumia lakini hata yeye mwenyewe hajui ni za nini zaidi ya mama yake,” anasema.
Mwalimu huyo anaishukuru taasisi hiyo kwa kufanya upimaji bila malipo shuleni hapo kwani itasaidia kuwatambua wanafunzi wenye matatizo na hivyo kupata matibabu mapema.
“Wamewafanyia upimaji wanafunzi 1,350 wa darasa la kwanza, pili na tatu, kabla ya upimaji huu tuliwashirikisha wazazi, kwa hiyo wale ambao watakutwa na tatizo pia tutawashirikisha wazazi ili waendelee kufuatilia matibabu ya watoto wao,” anasema.
Hali halisi
Waziri Ummy anasema idadi kubwa ya watu wenye matatizo ya kutokuona asilimia 90 wanaishi katika nchi zinazoendelea.
Anasema asilimia 65 ya watu wasioona ni wale wenye umri wa zaidi ya miaka 50 na kwamba kundi hilo linachangia asilimia 20 ya watu wote duniani.
“Ongezeko la watu wenye umri mkubwa katika nchi nyingi kunamaanisha ongezeko la watu watakaokuwa hatarini kupoteza uwezo wao wa kuona kutokana na matatizo ya macho.
“Watoto milioni 19 duniani wanakabiliwa na matatizo hayo na kulingana na kwa mujibu wa takwimu za WHO takriban Watanzania 573,000 hawaoni kabisa.
“Kwa ujumla watu wote wenye matatizo ya kuona kwa viwango mbalimbali nchini wanakadiriwa kuwa mara tatu ya watu wasioona ambao ni takriban watu milioni 1,73,000,” anabainisha.