Grace Shitundu na Leonard Mang`oha- Dar Es Salaam
SAFARI ya mwanasiasa Bernard Membe ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ilihitimishwa jana na Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya chama hicho baada ya kufukuzwa uanachama kwa makosa ya kimaadili.
Kamati Kuu imefukuza uanachama wa CCM, Membe ambaye pia amepata kuwa Waziri wa Mambo ya Nje katika serikali ya awamu ya Nne na kulitumikia Jimbo la Mtama kama mbunge kwa muda wa miaka 15 baada ya kuonekana kushindwa kujirekebisha katika adhabu alizopewa kipindi cha nyuma.
Muda mfupi baada ya CCM kutangaza kumfukuza, Membe aliandika kwenye mtandao kwa Twitter kwamba; “Watanzania wenzangu nimepata habari ya kufukuzwa kwangu kutoka kwenye chama changu cha CCM, Simu zinamiminika hadi nashindwa kuzijibu, Tulieni! Nitapata muda wa kuongea na wote, muda si mrefu!”.
Mbali na Membe kufukuzwa, Kamati kuu ya chama hicho imempa karipio na kifungo cha kutokugombea nafasi yoyote ndani ya chama hicho, Katibu Mkuu mstaafu Abdulrahman Kinana na pia kumsamehe Katibu Mkuu mstaafu, Yusuph Makamba ambaye ameomba msamaha kwa barua.
Makada hao wa CCM walifikishwa katika Kamati ya Maadili inayoongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula kwa makosa ya ukiukwaji wa kimaadili.
Maazimio ya kuwaita makada hao yalifanywa Disemba 13 mwaka jana na Halmasharui Kuu ya CCM iliyokutana jijini Mwanza chini ya Mwenyekiti wake Rais Dk. John Magufuli.
Chanzo cha kuitwa kwa makada hao ni baada ya sauti zao kusambaa katika mitandao ya kijamii zikimsema vibaya Rais Magufuli ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM.
Lakini pia Membe binafsi aliwahi kutuhumiwa hadharani na Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk. Bashiru Ally kwa kuandaa mipango ya kumkwamisha Rais Dk. John Magufuli katika uchaguzi wa 2020.
Wakati Membe na Kinana wakikumbana na adhabu hiyo sasa, katika sakata hilo walikuwepo pia Mbunge wa Mtama Nape Nnauye, Mbunge wa Bumbuli January Makamba na Mbunge wa Sengerema William Ngereja ambao waliomba radhi mapema na kusamehewa na Rais Magufuli.
UAMUZI WA KAMATI KUU
Akizungumza na vyombo vya habari jana katika Ofisi ndogo za CCM Lumumba, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole alisema Kamati Kuu baada ya kupokea maelezo ya makada hao iliyajadili na kutoka na maazimio hayo.
Alisema Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imeazimia kwa kauli moja kwamba Membe afukuzwe uanachama wa Chama Cha Mapinduzi.
“Uamuzi huu umekuja baada ya kuja taarifa zake ndani ya chama zikionyesha mwenendo wake kutoka mwaka 2014 katika chama ambapo amewahi kupata adhabu nyingine ambazo zingeweza kumrekebisha, lakini imeonekana sivyo.
“Adhabu kwenye Chama cha Mapinduzi zipo ambazo zinaweza kuwa za siri akaambiwa mhusika, na adhabu ya karipio inasomwa hadharani, adhabu ya kufukuzwa inasomwa hadharani.
Aliongeza kusema; “Jambo moja tu ninaloweza kusema kuwa kujiunga uanachama wa Chama Cha Mapinduzi ni mchakato, kujitoa pia kuna utaratibu na kufukuzwa uanachama upo utaratibu wake, ”.
Alisema Kamati Kuu imepokea maelezo ya Katibu Mkuu mstaafu wa CCM Abdulrahman Kinana na imeaziamia apewe adhabu ya karipio kwa mujibu wa kanuni za uongozi na maadili toleo la 2017.
“Adhabu ya karipio imeainishwa katika kanuni na inasema mwanachama anayefanya kosa linalokipaka matope chama na bila ya kuonyesha nia ya kujirekebisha, basi Kamati Kuu ya Halmashauri kuu ya Taifa inaweza ikampa mwanachama huyo adhabu ya karipio.
“Mwanachama aliyepewa adhabu ya karipio atakuwa katika matazamio kwa muda usiopungua miezi 18 kutoka tarehe ya jana ili kumsaidia mwanachama huyo katika jitihada za kujirekebisha” alisema Polepole.
Alisema mwanachama anapokuwa katika kipindi hicho hatakuwa na haki ya kugombea nafasi yoyote ya uongozi katika chama lakini atakuwa na haki ya kupiga kura kuwachagua viongozi wake wa chama kama ana dhamana hiyo.
Kwa upande wa Katibu Mkuu mstaafu Yusuph Makamba, Polepole alisema Kamati Kuu ya NEC imeazimia mwanachama huyo asamehewe makosa yake kwa kuwa ameomba msamaha kwa barua.
“Kamati Kuu imetoa msamaha huu kwa msingi kwamba Makamba wakati wote tangu aliposomewa mashtaka yake amekuwa ni mtu muungwana, mnyenyekevu na mtii kwa mamlaka ya chama na kubwa kuliko yote Makamba ameomba asamehewe makosa yake kwa barua,” alisema Polepole.
ADHABU YA MEMBE 2014
Mwaka 2014 Membe wakati huo akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, pamoja na mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowassa na Frederick Sumaye na wabunge Steven Wasira, William Ngeleja na January Makamba waliitwa mbele ya Kamati ya Maadili ya CCM kuhojiwa kwa tuhuma za kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2015 kabla ya wakati kinyume cha utaratibu wa chama hicho.
Katika tuhuma hizo Membe na wenzake walitiwa hatiani kwa kosa la kuanza kampeni mapema ambapo walizuiwa kujihusisha na shughuli za chama hicho, ikiwa ni pamoja na kugombea nafasi za uongozi kwa kipindi cha miezi 12.
TUHUMA ZAO
Itakumbukwa Desemba 1, 2018
Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally ndiye aliyekuwa wa kwanza kumtuhumu Membe hadharani na alimtaka afike ofisini kwake ili kutoa ufafanuzi wa tuhuma za kuandaa mpango wa kumkwamisha Rais Magufuli.
Dk Bashiriu alitoa agizo wakati akiwa mkoani Geita ambapo alisema Membe anatuhumiwa kuandaa
mipango hiyo kimyakimya na tangu ameteuliwa kushika wadhifa
huo hajawahi kuonana naye.
“Kati ya wagombea wote wa CCM ni Membe peke yake ambaye sijakutana naye, namkaribisha ofisini, aje anieleze ninayoyasikia ni kweli au si kweli.”
“Kwani haya yanayozungumzwa nyie hamyasikii? nasema peke
yangu? Mimi ndiyo Katibu Mkuu wa CCM aje ajitetee kwamba
yeye si kikwazo,” alisema Dk. Bashiru
“Iweje watu waseme kwamba wewe (Membe) unafanya vikao
vya kutafuta kura za 2020, kwamba unataka kumkomesha Rais
Magufuli, halafu unakaa kimya tu, sasa mimi nakualika uje
ofisini kama ni mwanachama wa kweli aliyetoa ahadi ya
uanachama wa CCM ya kusema kweli daima fitina mwiko.
MAJIBU YA MEMBE
Januari 17 mwaka huu katika mahojiano yake na gazeti dada la hili la RAI, Membe alizungumzia mwaliko huo wa Dk. Bashiru ambapo alimshangaa kwa kukalia kimya barua yake ya wito.
Akizungumza na RAI nyumbani kwake, Membe alisema: “Nilituhumiwa na Katibu Mkuu Dk. Bashiru Ally kuwa ninaihujumu Serikali ya Awamu ya Tano na kunitaka nifike ofisini kwake kujibu tuhuma baada ya kudai hana namba yangu ya simu.
“Na mimi kwa kumheshimu Katibu wangu wa chama tarehe 7, Desemba mwaka jana nilimpelekea barua kwa dispatch (ushahidi) na kusainiwa nikimuomba kunipangia siku, muda na tarehe ya kufika kwake lakini cha kushangaza ameendelea kukaa kimya.”
Aidha, Mwanadiplomasia huyo alidai kushangaa kusikia kauli ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa chama hicho Humphrey Polepole kuwa mjadala huo umefungwa rasmi.
“Nimemsikia Polepole kupitia Radio Clouds akisema ‘mjadala wa Membe umefungwa rasmi.’ Sasa ninamhoji ni yeye aliyeuanzisha mjadala huo hadi aufunge? Lakini pia kulikuwa kuna mjadala rasmi wa Membe?”
Akizungumza katika kipindi cha ‘Power Breakfast’ cha kituo cha Radio Clouds cha jijini Dar es salaam, Polepole akizungumzia masuala mbalimbali ya chama hicho alipoulizwa sakata la Membe na Bashiru limefikia wapi alijibu kwa msisitizo, “naomba niwaambie Watanzania na wana CCM kuwa mjadala wa Membe umefungwa rasmi.”
Membe aliendelea kusema: “Nilitegemea baada ya Katibu Mkuu kunitaka nifike kwake angefanya hivyo maana hata nilipotaka mtuhumu wangu mkubwa (Cyprian) naye awepo Katibu Mkuu alinitaka nisimuwekee masharti, nikakubali kukutana naye bila huyo ili nijibu mapigo.
“Hata hivyo, huyo mtuhumu wangu tayari nimemfungulia kesi Mahakama Kuu nikimtaka athibitishe kauli yake dhidi yangu kupitia gazeti lake au anilipe sh 10 Bilioni kama fidia ya kunichafua.”
Ni wakati huo huo wa mvutano wa maneno kati ya Membe na CCM, Julai mwaka jana zilisambazwa vipande vya sauti zilizoonekana kunyofolewa kutoka katika simu za akina January, Nape na makatibu wakuu wastaafu hao wa CCM, Makamba na Kinana na Membe.
Katika sauti hizo zilizovujishwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwa upande wao January, Nape, Kinana na Makamba pamoja na mambo mengine walisikika wakizungumzia kuandaa taarifa kwa vyombo vya habari kuhusu tuhuma zilizoelekezwa kwa makatibu wakuu hao wastaafu na zaidi baadhi yao wakimsema vibaya Rais Magufuli.
Siku chache baadaye ikasambaa sauti nyingine ya mawasiliano yanayodaiwa kuwa ni ya Nape na Ngeleja kisha kufuatiwa sauti inayodaiwa kuwa ni ya Membe na Katibu Kata cha Rondo mkoani Lindi.
Membe alipoulizwa na vyombo vya habari kuhusu sauti hiyo alikiri kuwa ni yeye.
WARAKA WA KINANA, MAKAMBA
Kusambaa kwa sauti hizo kulitanguliwa na tukio la Julai 14 mwaka jana ambapo Kinana na Makamba waliandika taarifa kwa Baraza la Wazee wa CCM wakilalamikia mambo mbalimbali ikiwamo kudhalilishwa kwa mambo ya uongo na mtu anayejitambulisha kama mwanaharakati na mtetezi wa Serikali.
Waraka huo unaodaiwa kuandaliwa kwa ushirikiano wa Nape na January pia ulisambazwa katika mitandao ya kijamii.
Katika taarifa hiyo viongozi hao walidai kuwa wamezingatia Katiba ya CCM toleo la mwaka 2017 ibara ya 122, na kwamba waliwasilisha maombi yao wakiwasihi wazee hao wa chama watumie busara zao kushughulikia jambo hilo ambalo walidai kuwa linaelekea kuhatarisha umoja, mshikamano na utulivu ndani na nje ya chama.
Pia walidai kuwa wametafakari kwa kina kabla ya kutoa taarifa kuhusu kile walichodai kuwa ni uzushi na kwamba mara kwa mara Watanzania wamekuwa wakijiuliza kwamba mtu huyo anatumwa na nani.
“Pili anakingiwa kifua na nani? Tatu anatumika kwa malengo gani? Na nne nini hatima ya mikakati yote hii.
“Tafakari yetu inatupeleka kupata majibu yafuatayo; kwanza kwa ushahidi wa kimazingira mtu huyu anatumwa na kutumiwa na watu wenye uwezo wa kumlinda na kumkingia kifua bila kuhojiwa na taasisi yoyote wala mtu yeyote.
“Pili zipo ishara kwamba watu hawa wanaomkingia kifua wana mamlaka, baraka na kinga ambazo wamepewa ili kutekeleza majukumu maalumu kwa watu maalumu na kwa malengo maovu,” ilieleza taarifa yao hiyo.
Katika hoja nyingine walidai kuwa mtu huyo anatumika kwa malengo ya kuwazushia, kuwakejeli, kuwavunjia heshima, kuwatia hofu na kuwanyamazisha viongozi, taasisi na watu ambao ni walengwa waliokusudiwa.
Jingine ni kwamba kuna kila dalili kuwa lengo na hatima ya mkakati huo ni kuandaa tufani ya kuwahusisha walengwa, wastaafu na walio kazini katika nafasi mbalimbali na matendo ya kihalifu, kimaadili na kihaini ili kuhalalisha hayo wanayokusudia kuyafanya.
“Tumeamua kutochukua hatua za kisheria kwa sasa kwa sababu kwanza jambo hili lina taswira ya kimkakati na lina mtandao wenye malengo ya kisiasa. Kwa hiyo linapaswa kushughulikiwa kisiasa. Pili, unapochafuliwa, unachokwenda kudai mahakamani ni fidia. Kwetu sisi, heshima yetu haiwezi kuthaminishwa na fidia,” walieleza kupitia taarifa hiyo.
Kuhusu tuhuma zilizokuwa zikielekezwa kwao na mwanaharakati huyo walisema wanaamini kuna sehemu zinatoka na kwamba anatumwa kutekeleza maagizo na kutumika kama kipaza sauti tu.
Waraka huo ulidai kuwa mara ya kwanza walizushiwa kuwa wanamkwamisha Rais Dk. Magufuli kutekeleza majukumu yake jambo ambalo walilipuuza kwa imani kwamba viongozi wao watayaona kwa namna yalivyo kuwa haiwezekani washiriki kuihujumu Serikali ya chama walichokitumikia maisha yao yote.
Uliongeza kuwa mara ya pili walizushiwa kuwa wanataka kumhujumu Rais ili asipitishwe na CCM kutetea urais mwaka 2020.
“Katika utumishi wetu, tumesimamia michakato ya kupitisha wagombea wa nafasi ya urais na nyinginezo tuhuma hizo ni uzushi uliosukwa kwa malengo maalumu na kwamba msingi wa tuhuma zote mbili ni hofu.
Pamoja na hayo yote Desemba 13 mwaka jana kikao cha halmashauri Kuu wa CCM (NEC) kilichofanyika Mwanza kiliagiza Kamati ya Madili ya chama hicho kuwahoji Membe na wenzake, jambo ambalo ambalo lilifanyika baada ya kuitwa na kuhojiwa Februari 6 mwaka huu.
Baada ya kuhojiwa Membe aliwaeleza waandishi wa habari kuwa amekuwa mtu mwenye furaha kubwa ajabu huku akionesha kufurahia safari yake huko jijini Dodoma.
“…lakini niwaambie tu, safari hii ya kuja Dodoma ilikuwa ni ya manufaa makubwa sana sana sana, kwangu kwa chama na kwa taifa letu.”
Alipotakiwa kueleza mwenendo wa mahojiano na hatima yake baada ya kuhojiwa alisema mambo mengine yatakuja kidogo kidogo huku akiahidi kuwa anakwenda kula chakula kizuri na mkewe katika hoteli moja ya kifahari.
“Mijadala ilikuwa mizuri, mikubwa na ya kitaifa inayohusu chama chetu cha mapinduzi, inayohusu nchi yetu. Nimepata nafasi nzuri ya kujadili masuala ya kitaifa na ya kimataifa, nimepata nafasi nzuri ya kufafanua mambo kadhaa ambayo chama changu walitaka kuyajua,” alisema.
Siku moja baadaye kupitia ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa Twitter alieleza kuwa anamshukuru Mungu kwa ujasiri aliompa wa kwenda mbele ya Kamati ya Maadili na Nidhamu na kujibu hoja mbalimbali bila woga, bila kuyumba wala kuyumbishwa.
“Naamini wameupokea ushauri nilioutoa kuhusu uhuru, haki, uchaguzi na uhusiano wa kimataifa,” alieleza Membe kupitia ujumbe wake huo.
Baada ya Membe kuhojiwa ilizuka sintofahamu kuhusu kuhojiwa kwa Kinana na Makamba ambao hata hivyo walionekana katika ofisi za CCM Dar es Salaam na si Dodoma ambapo taarifa zinadai kuwa waliwasilisha malalamiko yao kwa barua.