27.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 22, 2024

Contact us: [email protected]

UNDANI MAUAJI YA ASKARI WANANE WABAINIKA

Na Mwandishi Wetu – pwani

TABIA ya usiri, hofu na itikadi kali za kidini vimehusishwa kuwa nyuma ya pazia la mauaji ya askari wa Jeshi la Polisi na viongozi wa Serikali za Mitaa na Vijiji mkoani Pwani.

Taarifa zilizokusanywa na MTANZANIA Jumapili kutoka vyanzo vya ndani ya Jeshi la Polisi na katika maeneo ambayo matukio ya mauaji yanayotokea mara kwa mara, zinadai kuwa ukatili huo wa kutisha unaendeshwa na mtandao mpana wa kihalifu uliojikita zaidi katika wilaya za Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Mtandao huo unadaiwa kusheheni wataalamu wenye ujuzi wa kutumia silaha nzito waliopatiwa mafunzo katika moja ya nchi za Afrika na Mashariki ya Kati.

Inaelezwa kuwa mtandao huo unaendesha mauaji hayo kwa nia ya kukusanya silaha ili kutanua magenge yao ya uhalifu.

Tukio la wiki iliyopita la kuuawa kwa askari wanane, ambalo linaelezwa kufanywa kwa misingi ya kulipa kisasi, linafanya jumla ya idadi ya askari na raia waliouwa katika kipindi kisichozidi mwaka mmoja kufikia 18.  

Inaelezwa kuwa mtandao unaotekeleza mauaji hayo mbali na kuwa na intelijensia kali, pia una mizizi iliyokomaa ndani ya jamii, hatua inayosababisha kushindwa kuufichua kwa hofu ya kuuawa.

Kuwapo kwa mazingira hayo, kunawafanya wakazi wa maeneo husika kuwa wasiri wakubwa wa wahalifu.

Hilo linaweza kuthibitishwa kwa kiasi fulani na mazingira ambayo MTANZANIA Jumapili limeyashuhudia katika vijiji vya Mwalusembe, Kimanzichana na Bungu.

Tofauti kabisa na dhana iliyozoeleka ya ukarimu wa Watanzania, baadhi ya watu wa maeneo hayo hukwepa wageni na hawataki kuzungumza nao.

Askari mmoja aliyeko katika ngome ya Polisi ya Bungu wilayani Kibiti, aliliambia gazeti hili kuwa changamoto inayoikumba operesheni ya kutokomeza uhalifu, ni wananchi kukwepa kutoa ushirikiano wa kutosha wa kufichua wahalifu mahali walipo.

Alisema hali hiyo inasababishwa na hofu ya kuuawa na wahalifu hao, hivyo mazingira hayo yanawafanya kukwepa kuzungumza na wageni wanaotembelea katika vijiji vya wilaya hizo.

Askari mwingine aliliambia MTANZANIA Jumapili kuwa wahalifu wanaowakamata kila wanapowahoji wengi wao hawatoi ushirikiano.

“Tumewakamata wengi tu, lakini tukiwabana kwa taarifa zaidi hawatujibu. Baadhi hugeuka bubu, wengine tukiwapa kibano huishia kutamka lugha isiyoeleweka, lakini wapo wanaotuambia wamefunzwa uhalifu wa aina hii nje ya nchi,” alisema.

Aliongeza kuwa katika operesheni za kuwasaka wahalifu hao, wamegundua wengi wanaishi msituni wakijifanya wanafanya biashara ya kuchoma mkaa na wengine hupendelea kuuza matunda pembezoni mwa barabara kubwa.

Alisema mara nyingi wahalifu wanaojifanya kuuza matunda pembezoni mwa barabara huwa na jukumu la kukusanya taarifa na kupeleka kwenye vikao vyao vya mikakati.

“Tukiwakamata wahalifu hawa na tukienda kukagua makazi yao tunakuta kuna ‘line’ za simu nyingi, tukiwabana wanakwambia kuna mawasiliano mengine wanaongea mara moja tu kisha wanateketeza ‘line’, na hawapendi kutumia simu za kisasa ‘smartphone’,” alisema askari mwingine.

MAFUNZO

Mmoja wa maofisa wa juu wa Serikali ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa kuwa si msemaji, alilithibitishia gazeti hili kuwa miongoni mwa watu wanaounda mtandao huo na ambao wanashikiliwa kwa tuhuma za mauaji ya askari, raia na viongozi wa vijiji katika Mkoa wa Pwani ni wale waliopatiwa mafunzo katika nchi za nje ikiwamo Mashariki ya Kati.

Taarifa ambazo gazeti hili limedokezwa kutoka katika mifumo ya jeshi hilo mkoani Pwani, zinaeleza kuwa baadhi ya wahalifu hao waliokamatwa na kuhojiwa wamesema kuwa walipelekwa kwenye nchi hizo kupata mafunzo tangu wakiwa watoto wadogo.

“Vijana hawa waliondoka nchini wakati wa utawala wa awamu ya pili, ukiwauliza wanakwambia walikuwa watoto sana, hivyo hawakujua wanakwenda kufanya nini, lakini baada ya kufika huko wakakutana na elimu ya uhalifu, wamefundishwa nchi mbalimbali na sasa wamerudi nchini kuendesha mafunzo kwa vijana wetu na lengo lao wanataka kuimarisha magenge yao ya uhalifu,” kimeeleza chanzo chetu.

Inaelezwa mtandao huo kabla ya kuwaua askari wanane katika tukio la wiki iliyopita wilayani Kibiti, walipanga kushambulia ngome ya Jeshi la Polisi inayoendesha operesheni ya kuwasaka wahalifu katika eneo la Mkuranga, Kibiti na Rufiji.

Chanzo chetu kilidai kuwa tukio hilo la ushambulizi lilikuwa la ulipaji kisasi baada ya kupata taarifa kuwa kuna wenzao wameuawa katika majibizano ya risasi na polisi.

“Kabla ya kuua askari wenzetu, nasikia walibishana sana, wengine walitaka kuja kushambulia ngome yetu ila baadhi wakakataa,” alidokeza mmoja wa askari.

Gazeti hili limeelezwa kuwa mtandao wa wahalifu hao una intelijensia ya hali ya juu na katika maeneo mengine wanatumia hata watoto kukusanya taarifa.

MTANZANIA Jumapili lilipomuuliza Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Ernest Mangu juu ya taarifa za kuwako kwa mtandao huo wa wahalifu, alisema hana taarifa hiyo na hawezi kuthibitisha chochote juu ya hilo.

Alipoulizwa juu ya kukamatwa kwa watuhumiwa wanaohusishwa na mtandao wa mauaji, alisema taarifa za namna hiyo lazima zitolewe na polisi, na kwamba hakuna raia ambaye ana uwezo wa kujua polisi walimkamata wapi mtu.

“Sasa basi kazi ya upelelezi hauwezi kuipeleka kwenye magazeti… haiwezekani ukaambiwa matokeo ya mahojiano kutoka kwa raia, kwa hiyo hicho chanzo chako cha habari hakina ukweli wowote labda uwe na chanzo cha habari kamili ambacho hutaki kukitaja.

“Sisi hatuwezi kuanza kuingilia shughuli za upelelezi, vinginevyo tutakuwa tunalishinda kusudio la uchunguzi,” alisema IGP Mangu.

MTANZANIA Jumapili lilipomtafuta Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Evarist Ndikilo kwa simu ili atoe ufafanuzi wa uwapo wa mtandao huo, alijibu kwa ujumbe mfupi wa maandishi kuwa yuko kikaoni na akaomba awasiliane kwa kuandikiwa meseji, hata hivyo alipoandikiwa hakujibu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles