25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

UNAJISIKIA VIZURI KULA KIYOYOZI, UMEFIKIRIA MWISHO WAKO?

Na ATHUMANI MOHAMED

KWA kawaida binadamu hutaka kujisikia vizuri. Ndivyo binadamu walivyoumbwa. Hupenda kufanya mambo yanayofurahisha mioyo zaidi.

Hata hivyo katika kusaka mafanikio, kanuni zinasema ni lazima ukatae mambo yanayokufanya ujisikie vizuri kwa muda fulani ili baadaye ufanikiwe.

Hii inamaanisha kwamba lazima ukubali maisha ya mateso kwa wakati fulani katika maisha yako, wakati ukitafuta maisha mazuri huko mbeleni.

Kwanini washauri wa mambo ya mafanikio na maisha wanashauri kwa hoja hii? Ni kwa sababu ni ukweli kwamba asilimia kubwa, mambo yanayofurahisha huhitaji fedha.

Fedha ambazo ukizitumia kwa wakati huo ambao unazo, kuna siku utakwama na hapo utarudi kwenye maisha magumu. Kwamba, unaweza kuwa mgumu kwa wakati fulani ambao una uhakika wa kupata kiasi fulani cha fedha kwa lengo la kujijenga ili baadaye uishi kwa ufahari.

Hiyo ndiyo kanuni ya maisha ambayo wengi huwashinda. Wanaoishinda kanuni hii, wanaishi maisha mazuri. Wengine ambao wanaishinda kanuni hii sasa wanajiandaa kwa maisha mazuri baadaye.

Hakuna uchawi katika hilo, ni suala la kanuni. Kwamba ukiweza kuitii basi tarajia mafanikio, lakini ukishindwa, ujue unaandaa bomu la maisha ya chini siku za usoni.

Bomu hili la kijasiriamali, huanzia mashuleni. Kwa bahati mbaya sana, mfumo wa elimu wa hapa kwetu upo katika mtindo wa kukariri zaidi. Mwanafunzi anasoma ili afaulu mitihani.

Lakini wakati akifanya hivyo, watoa elimu wanawaeleza wanafunzi wao kwamba wanatakiwa kusoma kwa bidii ili wafaulu mitihani na baadaye wapate kazi.

Hivyo basi, vizazi kwa vizazi wanafanya kazi kwa matazamio ya kupata ajira nzuri ofisini. Kijana yupo chuo, lakini akilini mwake anawaza kuvaa mashati ya vitenge, suti na tai shingoni, huku akifanya kazi kwenye ofisi nzuri inayopuliza viyoyozi kila kona baada ya kumaliza masomo.

Ndivyo maisha mazuri kwa Mwafrika. Hizo ni fikra mfu. Na kwa hakika kuwaza kuajiriwa maisha yako yote, maana yake ni kukubali kuwa masikini maisha yako yote.

Hata siku moja mshahara haujawahi kutosha. Lazima akili yako ipanuke, uone kitu kikubwa kilicho ndani yako ili uweze kupambana kwa kufanya ujasiriamali kwa ajili ya kutengeneza utajiri wa baadaye.

 

AJIRA NI MBAYA?

Ajira haijawahi kuwa mbaya hata siku moja. Ilivyo ni kwamba maisha ya binadamu yeyote yanategemea mtu mwingine. Maana yake ni kwamba lazima mtu akubali kutoa nguvu au akili zake kwa ajili ya kufanya kazi ili apate ujira.

Lakini kuajiriwa hakukufungi kufanya shughuli za ujasiriamali. Umeajiriwa serikalini kwa mfano, ambapo mfumo wa kazi ni mapumziko kuanzia Ijumaa (nusu siku), Jumamosi na Jumapili.

Siku hizi mbili nzima na nusu unaweza kusimamia mradi wako na ukajiongezea kipato. Mfano umeamua kuwa mfugaji wa kuku nyumbani kwako; ni kazi ambayo haikuhitaji muda wote uwe hapo.

Utakuwa kazini kwako, lakini kuna mtu anaangalia mifugo yako. Baada ya siku kadhaa unaweza kuwa na kuku wengi ambao watakuongezea utajiri.

 

BUNI ZAIDI NA ZAIDI

Sumbua ubongo wako kubuni miradi mingi kadiri uwezavyo. Mfumo wa maisha ya utajiri, unamtaka mtu kuajiriwa kwa ajili ya kupata fedha, kisha kubuni miradi ambayo ataisimamia wakati akiendelea na kazi, kisha baadaye kusimamia kazi zako, baada ya kukua kwa biashara zako.

Hii inakufanya utambue kuwa ajira ni muhimu sana kwako, lakini unatakiwa uitumie kama daraja la kukusogeza kwenye utajiri hapo baadaye. Ukibweteka na viyoyozi, nguo nzuri, gari na nyumba unayolipiwa na ofisi, kuna siku kazi itaisha, maana yake na wewe utakuwa umeishia hapo.

Unaweza kujiuliza kivipi? Jibu ni rahisi. Unaweza kupata ulemavu wa maisha na mkataba wako wa ajira ukaishia hapo. Ni kweli utalipwa mafao yako, lakini hayatakidhi mahitaji yako ya msingi kwa maisha yako yote yaliyobaki.

Aliyewekeza, anaweza kuendelea kuishi bila hofu, maana muda huo nguvu na akili yake si muhimu sana kwenye biashara yake, kwani anaweza kuajiri watu wakaendelea kufanya kazi, wakati akikabiliana na maisha yake mapya ya ulemavu.

Siyo jambo la kuombea, lakini lazima tukubali kwamba kwenye maisha dharura zipo. Marehemu Mzee Gurumo (mwanamuziki) alipata kuimba akisema, sote tu walemavu watarajiwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles