26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

UN, TEF WATEMBELEA MIRADI YA MAENDELEO ARUSHA

Na JANETH MUSHI,ARUSHA



Umoja wa Mataifa(UN) na Jukwaa la Wahariri (TEF), wametembelea miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO), jijini hapa na kuridhishwa na utekelezwaji wake hususani inayopunguza ukosefu wa ajira kwa vijana.

Miradi hiyo ni Chuo cha Taifa cha Utalii na Hoteli ya Arusha, ambazo ni baadhi ya taasisi zinazoshirikiana na ILO, katika kutekeleza Programu ya Ubora ya Uanagenzi inayofadhiliwa na Serikali ya Norway, hadi sasa zaidi ya wahitimu 150 wa elimu ya sekondari wamepitia programu hiyo ya kuwajenga uwezo katika sekta ya utalii na hoteli.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo,Afisa Habari na Mawasiliano wa ILO, Magnus Minja, amesema lengo la kutembelea miradi hiyo ni kuangalia utekelezaji wa malengo endelevu ya maendeleo ya Dunia,yanayotekelezwa katika nyanja mbalimbali.

Amesema kuwapa vijana mafunzo bora ya wanagenzi inawaongezea nafasi ya kuajiriwa na kuweza kupambana katika soko la ajira na kuwa hadi sasa kuna wanagenzi zaidi ya 150 kwenye programu zinazoendelea Tanzania Bara na Zanzibar.

“UN nchini hapa inaendelea kushirikiana na Serikali na ukweli ni kwamba viwango vya ukosefu wa ajira nchini kiujumla ni asilimia 10.3, na kwa vijana ni asilimia 11.7,ikilinganishwa na kiwango cha dunia cha asilimia 5.8,”amesema Minja.

Aidha ujumbe huo umetembelea Taasisi ya Uhandisi na Usanifu Mitambo Tanzania (TEMDO), kujionea mradi wa kilimo cha mbogamboga unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) kwa lengo la kuwezesha wajasiriamali wadogo kuboresha mazao yao ili yapate soko la ndani na nje.

Naye Mratibu Msaidizi wa TEF, Anita Mendoza,amesema kesho Jukwaa hilo kwa kushirikiana na UN watatoa mafunzo kwa waandishi wa habari wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara, kuhusu namna ya kuandika habari za maendeleo zinazotekelezwa na umoja huo na Serikali, katika utekelezaji wa Malengo endelevu ya dunia.

Kwa upande wake Msaidizi wa UNIDO, Alusaria Nkya,amesema mradi wa Kiliflora ni miongoni mwa miradi minne iliyokamilishwa ya kusaidia ufuaji umeme kutoka katika vinu vidogovidogo.

Amesema maeneo hayo manne yanazalisha jumla ya 1640 kW, za umeme ambazo zimewanufaisha zaidi ya watu 3,000 kupitia ajira za viwanda vidogovidogo na kuzipa umeme kaya zaidi ya 4000 mbali na vituo vya jamii,shule,hospitali na nyumba za watoto yatima.

Awali Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ushauri wa ndani kutoka TEMDO, Mhandisi Alexander Komba alishukuru ujumbe huo kuwatembelea na kuwafadhili vifaa vilivyosaidia kuboresha bidhaa za kilimo za wajasiriamali wadogowadogo na kuomba mradi huo uwe endelevu kwa sababu mahitaji makubwa kwa kundi hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles