Mwandishi Wetu, Pangani
Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega ameahidi kununua jokofu la kusindika samaki lenye thamani ya Sh milioni 20 katika Soko la Samaki Pangani Mashariki, wilayani Pangani.
Ulega ametoa ahadi hiyo leo Jumatano Septemba 26, alipofanya ziara ya siku moja wilayani Pangani na kukagua miradi mbalimbali wilayani humo.
Katika ziara hiyo Ulega pia ametembelea Chama cha Wafugaji wa Ng’ombe wa Maziwa (Wwawapa) ambao kwa siku wanazalisha zaidi ya lita 10,000 ambapo amewaahidi kuleta josho la kuogeshea mifugo kwa  kuzungumza na Benki ya Kilimo ili wafugaji hao wapatiwe mkopo nafuu na kuwaunganisha wafugaji hao na Taasisi ya Uzalishaji na Utafiti wa Mifugo (Taliri) ili waweze kupatiwa ufumbuzi wa magonjwa ya mifugo yao.
Ulega akiwa katika Chuo cha Uvuvi (KIM), amewataka kufika wizarani kwake kabla ya Oktoba 10, wakiwa na mikakati ya kukifanya chuo hicho kiwe na manufaa kwa wavuvi wa Pangani.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya, Zainab Abdallah, amemshukuru Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina na Naibu Waziri huyo kwa kufanikisha maombi yao na kuwatembelea ili kujua changamoto zinazowakabili katika sekta ya uvuvi.