Na Michael Sarungi, Dar es Salaam
WATANZANIA wametakiwa kujenga utamaduni wa kula vyakula vya asili katika kujikinga na ugonjwa wa saratani, ambao hivi sasa umekuwa tishio duniani.
Mbali na hilo, pia wametakiwa kuepuka uvutaji wa sigara, ulevi wa kupindukia na kubadili aina ya maisha kama njia ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana, daktari bingwa wa magonjwa ya saratani wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Dk. Harrison Chuwa, alisema katika kipindi cha mwaka mmoja hali ya ugonjwa huo imezidi kuwa mbaya.
“Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani leo, hali imekuwa ikibadilika na katika kipindi cha miaka mitatu, taasisi hiyo imekuwa ikipokea wagonjwa wa saratani 1,500 hadi 4,000 kwa mwaka,” alisema.
Alisema kati ya wagonjwa hao, wengi wao ni wale ambao ugonjwa huwa umefikia hatua za juu kiasi cha kusababisha matibabu yao kuwa ya gharama kubwa.
“Kwa kweli hata hali yetu ya maisha imekuwa ikichangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa ugonjwa huu hapa nchini. Kuacha kula vyakula vya asili na mboga za majani ni tatizo… badala yake vyakula vya kemikali nyingi vimechukua nafasi jambo ambalo si zuri kwa afya za Watanzania,” alisema Dk. Chuwa.
Alisema zipo njia nyingi za kuzuia saratani, ikiwamo kula vyakula vya asili, hasa ugali wa dona ulioandaliwa vizuri na kufanya mazoezi ya viungo.
Dk. Chuwa alisema kwa mujibu wa Taasisi ya Global Cane, hadi kufikia mwaka 2012, iliripotiwa kuwapo wagonjwa wapatao milioni 14.1 duniani, kati yao milioni 8.2 walifariki dunia.
“Unajua tatizo la nchi nyingi za Afrika ni elimu juu ya ugonjwa huu. Watu wengi bado wana uelewa mdogo juu ya ugojwa huu, ndiyo maana wengi wanakuja wakiwa wamechelewa,” alisema Dk. Chuwa.
Tezi dume kupimwa bure
Wakati huohuo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inaandaa kampeni ya kuwapima bure wananchi ugonjwa wa saratani ya tezi dume.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema upimaji huo utafanyika kama sehemu ya kukabiliana na ugonjwa huo.
Dk. Rashid alikuwa akizungumzia maadhimisho ya Siku ya Saratani Duniani ambayo hufanyika Februari 4 kila mwaka.
“Katika kuadhimisha Siku ya Saratani Duniani, wizara kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road ya Dar es Salaam, itatoa ujumbe uwafikie wananchi wote, ukieleza jinsi tunavyoweza kudhibiti saratani tutakaposhirikiana, na pia tutatoa elimu zaidi kwa umma kuhusu maradhi hayo.
“Pia, tutawapima wananchi saratani ya shingo ya kizazi na matiti, lakini pia wizara yetu inaandaa kampeni ya uchunguzi wa saratani ya tezi dume utakaofanyika mapema mwaka huu.
“Katika hili, tarehe kamili ya uchunguzi huu itatangazwa mipango itakapokamilika na upimaji huu utafanyika bure. Kwahiyo wananchi wote wanakaribishwa kwa ajili ya upimaji huo,” alisema Dk. Rashid.
Akizungumzia maradhi ya saratani kwa ujumla, alisema yamekuwa yakiongezeka kila siku duniani ingawa idadi kubwa ya wagonjwa iko katika nchi zinazoendelea.
“Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka wagonjwa wapya milioni 12.6 hugundulika duniani wakiwa na saratani.
“Hapa nchini idadi ya wagonjwa wapya wa saratani kila mwaka ni 34,000, lakini wengi wao hawafiki hospitalini kutokana na sababu mbalimbali,” alisema Dk. Rashid.