Na CHRISTIAN BWAYA
KUNA uhusiano mkubwa kati ya kile unachokiamini na vile unavyojisikia. Kukata tamaa, kwa mfano, kunaanzia katika yale unayoyaamini. Huwezi kukata tamaa hivi hivi. Nikirejea mfano nilioutoa kwenye makala yaliyopita, mtu anayeamini lazima kila kitu kiende kama vile anavyopanga, anajiweka kwenye hatari ya msongo wa mawazo. Kwa nini? Maisha sivyo yalivyo. Si nyakati zote yale tunayotamani hutokea.
Mambo haya tunayoamini ambayo kwa kiasi kikubwa ndiyo yanayochangia kutunyang’anya furaha zetu, mara nyingi, huwa yameingizwa kwenye fahamu zetu bila sisi kujua kinachoendelea. Mfano, tangu tukiwa wadogo, tunakuwa na shinikizo kubwa la kufikia matarajio ya wazazi wetu. Tunapokosea tunapewa adhabu zinazotufanya tuamini mtu makini hakosei. Tunapojikuta tumekosea, tunajawa na hatia kubwa tukiamini kwa kule kukosea, basi tumekuwa waovu.
Imani hizi wakati mwingine zinaingizwa kwenye fahamu zetu kwa nia njema na watu wanaotuzunguka. Chukulia, mathalani, binti anapofika miaka 35 bila kumtambulisha mchumba wake, kwa kawaida wazazi, ndugu jamaa na marafiki huanza kuwa na wasiwasi. Kwa kuwa furaha yao ni kuona binti yao anaolewa, kuchelewa kuolewa kunaanza kutafsiriwa kama balaa kubwa katika maisha yake. Kwa kuelewa kuwa hivyo ndivyo watu wanavyomchukulia, binti huyu ‘anayechelewa’ kuolewa anaanza kukosa amani. Akijifikiria anajiona yeye si kama wanawake wengine wanaoolewa kwa wakati.
Hebu fikiria wanandoa waliojaribu kupata mtoto kwa miaka kadhaa bila mafanikio. Ingawa ni kweli wengi wetu tunatamani kuwa na watoto, mara nyingi ni unyanyapaa unaotokana na matarajio ya watu wanaowazunguka ndio unaotutesa pengine kuliko hata kule kukosa watoto. Mama asiye na mtoto, kwa mfano, anajisikia vibaya kunyanyaswa na ndugu wa mume, kudharauliwa na watu wanaomwita ‘tasa’ kuliko anavyoumia kwa kukosa mtoto wa kumzaa yeye. Katika makala haya ninajaribu kupendekeza mahali pa kuanzia ili kukabiliana na hali ya kukata tamaa unayokabiliana nayo.
Kwanza kabisa, kuna haja ya kuyatazama maisha katika mtazamo tofauti. Kama tulivyokwisha kuona, shida zetu nyingi zinaanzia kwenye kile tunachokiamini. Tunachokifikiri na kukiamini ndicho kinachotufanya ama tukose amani au tuwe na furaha. Maana yake ni kwamba ili kukabiliana na hali ya kukata tamaa lazima kubadili namna yetu ya kufikiri. Nitatoa mifano.
Nikuuleze mathalani, kwa nini unakosa amani kwa sababu tu ndoto ulizowahi kuwa nazo hazijatimia? Unajua kuwa si kila unachokipanga  hutokea? Kwa nini sasa unakata tamaa? Inawezekana ulitamani kuolewa na bado hujaolewa. Unakosa furaha na maisha. Lakini fikiria watu wengi walioolewa na watu wanaowasumbua. Wapo watu wengi waliofanikiwa kutimiza ndoto za kuolewa lakini wameishia kuishi maisha ya majuto. Kutimia kwa ndoto zao hakujawaletea furaha walioitarajia.
Namkumbuka dada mmoja aliyekataliwa na mchumba wake siku chache kabla ya harusi. Aliumia. Kilichomwuumiza zaidi, yule aliyepanga kufunga nae ndoa aliamua kumwoa rafiki yake siku chache baadae. Kama kuna mambo yanaweza kumwuumiza mtu, hili ni moja wapo. Lakini baada ya miezi kadhaa ya ndoa hiyo, iligundulika kumbe kijana yule alikuwa na familia nyingine ya siri. Wakati mwingine unaweza kupoteza amani kwa sababu tu hujui kwa nini ndoto yako haijatimia. Ungekuwa na uwezo wa kuelewa kwa nini ulichotamani kitokee hakijatokea ungeweza kuwa na furaha.
Labda kinachokunyima furaha ni vurugu kwenye ndoa au kuachika. Ulipokuwa kijana uliota kuwa na ndoa ya mfano. Unapowaona wenzako wakifurahia ndoa zao, unajikatia tamaa na kujihurumia. Unajiona kama mtu mwenye bahati mbaya kwenye maisha. Lakini fikiria, unayo mangapi mengine ambayo wengine wangetamani kuwa nayo lakini hawanayo? Wakati wewe shida yako ni ndoa, wapo wenye ndoa nzuri lakini hawana furaha kwa sababu wanatamani kuwa na kazi nzuri uliyonayo. Wakati wewe unatamani kupata watoto, wapo wengi wenye watoto wavuta bangi, walevi, wahuni, wasiosikia na wakati mwingine hao hao wamewasababisha matatizo makubwa wazazi wao.
Maana yangu ni kwamba tunahitaji kujifunza kuyakubali maisha katika uhalisia wake. Magumu uliyonayo ni sehemu ya maisha yako. Naam. Hata pale unapopita katika nyakati ngumu kiasi cha kuhisi unakanyaga kaa la moto, jipe moyo kuwa hayo ndiyo maisha. Kuna nyakati katika maisha tunafurahia. Inapotokea hivyo, tunamshukuru Mungu na kujiona tumebarikiwa. Lakini pia, zipo nyakati katika maisha zinakuwa nguvu. Inapotokea hivyo, tusikate tamaa. Nyakati hizi ngumu tusizozipenda mara nyingi hutufundisha mambo ambayo tusingepitia magumu hayo pengine tusingejifunza. Nitaeleza jambo hili kwa kirefu wiki ijayo panapo uzima.