26.4 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

Ukawa wamchokoza Rais Magufuli

Rais John Magufuli
Rais John Magufuli

NA AZIZA MASOUD, DODOMA

WABUNGE walio katika Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) jana walimtuhumu Rais John Magufuli kuwa analiendesha Bunge kutokea Ikulu kwa kumtumia Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.

Wakizungumza na waandishi wa habari katika ofisi ya habari ya Bunge, wabunge hao walisema wanachokiona bungeni ni Rais Magufuli akiwa kama Spika wa Bunge huku viongozi wengine wa Bunge wakiwa ni matawi yake.

Wa kwanza kutoa tuhuma hizo katika mkutano huo uliohudhuriwa na wabunge wengi wa Ukawa alikuwa Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara ambaye alisema Bunge la 11 haliko huru kwa sababu maamuzi yake yanatolewa na Rais Magufuli kutoka Ikulu kupitia Naibu Spika, Dk. Ackson.

“Bunge linaongozwa na Magufuli (Rais John) kutoka Ikulu moja kwa moja kupitia Dk. Tulia, Rais ndiye Spika wengine ni matawi tu, mfano tukiangalia mwongozo wa posho za wabunge wa upinzani uliotolewa juzi, umetolewa uamuzi mara mbili, haiwezekani kitu kimoja kikatolewa maelezo mawili tofauti ni wazi kuwa anafuata maagizo kutoka juu,” alisema Waitara.

Alisema hivi sasa kuna mhimili mmoja wa dola ambao ni Serikali Kuu kwa sababu maamuzi yote yanatolewa na chombo hicho huku akilitaja Bunge kuwa tawi la Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Alisema Naibu Spika, Dk. Tulia hakupaswa kutoa uamuzi wa wabunge wa Ukawa kutolipwa posho kwa sababu ni mtuhumiwa wa jambo hilo.

“Kutomwita mheshimiwa tunamaanisha  na tungekuwa na jina baya zaidi tungemwita, nina wasiwasi na PhD yake ya sheria, sijawahi kuona mtu anayelalamikiwa anatoa hukumu sijawahi kuona, yeye ni mtuhumiwa anatoaje uamuzi. Bora Spika Job Ndugai arudi,” alisema Waitara.

Katika mwendelezo wa tuhuma zake hizo, alisema Naibu Spika, Dk. Tulia aliteuliwa kimkakati na Rais Magufuli na amekuwa akiongoza matukio mbalimbali yanayogharimu wananchi.

“Naibu Spika ni Mbunge wa ‘Voda Faster’, aligombea uspika CCM wakamkataa, baada ya kuona amekataliwa Rais akaamua kumpa ubunge ili aje kugombea nafasi ya Naibu Spika ambayo nayo ameilazimisha hata CCM walikuwa hawamtaki,” alituhumu Waitara.

Waitara alienda mbali zaidi kwa kumtuhumu Dk. Tulia kuwa miongoni mwa watu waliovuruga mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya kwa kushiriki kukata maoni ya wananchi na kubakiza yaliyotolewa na CCM.

Katika mlolongo huo wa tuhuma, Waitara aliendelea kutuhumu kuwa Dk. Tulia alishiriki kuwanyima haki ya kulinda matokeo ya kura kwa kuwataka wananchi kukaa umbali wa mita 200 kutoka kituo cha kupigia kura wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Aliendelea kusema kuwa pia alishiriki kurudisha Sh bilioni 12 Ikulu bila kumshirikisha Spika Ndugai.

Kwa upande wa Mbunge wa Vunjo, James Mbatia, alisema Serikali haiheshimu maamuzi wabunge na kwa mara kadhaa Rais Magufuli amekuwa akitoa uamuzi bila kuwashirikisha.

“Bunge linakaa na kujadili bajeti na kupitisha lakini Serikali haiheshimu na  haitekelezi, kuna haja gani ya kuwa na mhimili wa Bunge? Dk. Magufuli (Rais John) amekuwa akifanya maamuzi yake mwenyewe ya kuchukua fedha na kuzigawa katika taasisi mbalimbali bila kupitishwa na Bunge jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Kinachotushangaza ni fedha zinazobaki katika taasisi mbalimbali kupelekwa Ikulu wakati zinapaswa kurudi Hazina, anapelekewa yeye ndiye Hazina? Rais hapaswi kuzipangia fedha kazi kabla ya kupitishwa na Bunge, hakuna haja ya kuwa na huu mhimili kama unaingiliwa kiasi hiki,” alisema Mbatia.

Mbatia alisema msimamo wa Ukawa ni kufutwa kwa posho na endapo Serikali itapitisha hoja ya kukatwa kwa kodi mafao ya wabunge inapaswa iwakate viongozi wa ngazi zote waliotajwa katika sheria hiyo.

“Sheria mafao ya wabunge inahusu viongozi wote wa kisiasa, pia inaenda sambamba na pensheni ya Rais, Makamu wa Rais, mawaziri, Spika, Naibu Spika, wakuu wa mikoa na wilaya, iweje wachague wabunge tu kuwakata kodi kama ni hivyo wawakate viongozi wote waliotajwa ndiyo watakuwa wametenda haki,” alisema Mbatia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles