SHABANI MATUTU NA VERONICA ROMWALD, DAR ES SALAAM
WABUNGE wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), wanakusudia kupeleka hoja binafsi bungeni ili kumng’oa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia kwa kusababisha vurugu katika uchaguzi na siku za kuapishwa wenyeviti wa Serikali za Mitaa.
Akizungumzia kusudio hilo Dar es Salaam jana alipozungumza na waandishi wa habari, Naibu Katibu Mkuu Bara wa Chama cha Wananchi (CUF), Magdalena Sakaya, alisema wanachukua njia hiyo kutokana na Ghasia kugoma kung’oka kwa hiyari yake na Rais Jakaya Kikwete kushindwa kumuwajibisha kutokana na kushindwa kusimamia uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa haki na utulivu.
Alisema leo viongozi wa Ukawa wanatarajia kukutana jijini Dar es Salaam na kujadili mikakati watakayotumia katika kufanikisha jambo hilo kwa pamoja.
“Tulimtaka Ghasia kujiuzulu wakati zilipotokea vurugu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa na hata matokeo yalichakachuliwa kwa baadhi ya maeneo lakini hakutaka kufanya hivyo kwa hiyari yake.
“Leo hii tunaendelea kushuhudia makosa yakiendelea kujitokeza katika uapishwaji wa wenyeviti wa mitaa na imeshuhudiwa mahali waliposhinda wapinzani wametangazwa wanachama wa CCM na sehemu nyingine ambako uchaguzi haukufanyika nako wametangazwa wagombea wa CCM kushinda,” alisema Sakaya.
Alisema hali hiyo ya kubadilishwa kwa matokeo, imesababisha kuibuka kwa vurugu katika baadhi ya maeneo ambayo kama hatua hazitachukuliwa mapema zitasababisha Taifa kuelekea kubaya na kukumbwa na machafuko.
Alisema ukimya ambao umeendelea kwa Serikali kutotoa kauli kuhusu unyongwaji huo wa demokrasia, unatoa taswira kwamba CCM itakuwa inahusika kwa kutoa shinikizo kwa wakurugenzi kubadilisha matokeo ya wenyeviti hao.
“Kwa mfano katika Mtaa wa Ukwawani Kata ya Kawe, mgombea wa CUF alishinda lakini wamembadilisha na kumuweka wa CCM, Mtaa wa Msisiri A, Mwananyamala, msimamizi msaidizi alimtangaza mgombea wa CUF kushinda lakini kesho yake akabandika matokeo yakionesha aliyeshinda ni mgombea wa CCM.
“Mtaa wa Mwinyimkuu, Kata ya Mzimuni Kinondoni mgombea aliyeshinda alikuwa wa CUF lakini msimamizi akatangaza kurudiwa kwa uchaguzi huo Desemba 17 lakini wananchi waligoma kupiga kura na siku ya kuapishwa ameapishwa wa CCM.
“Katika Mtaa wa Kiwalani Kata ya Migombani, uchaguzi ulivurugika na masanduku yakaharibiwa na kesi hadi leo ipo Polisi Buguruni na masanduku hayo yapo hapo lakini cha kushangaza mgombea wa CCM ameapishwa,” alisema Sakaya.
Alisema yapo maeneo mengine ambayo matokeo hayakutangazwa kutokana na kutokea kwa vurugu lakini wagombea wa CCM walipewa barua za kwenda kuapishwa na katika Mtaa wa Malapa mshindi wa CUF jina lake lilionekana katika mtaa mwingine wa Liwiti.
“Maeneo mengine yaliyokumbwa na hali kama hiyo ni Kinyerezi, Migombani, Bunda (Mara) na kwingine ambako inaonyesha kwamba ni mikakati inayoandaliwa na CCM na wanajiandaa kuitumia katika Uchaguzi Mkuu ambao utafanyika mwaka huu,” alisema Sakaya.
Alisema CUF wamebaini kuwa CCM kwa sasa wamejiandaa kupora ushindi wa vyama vya upinzani kwa kutumia vyombo vya dola.
“Lakini tunataka kuwaonya kwamba, moto tuliouwasha katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa ni sawa na fukuto, tumejipanga vizuri zaidi ya tulivyodhibiti katika uchaguzi huu na uapishwaji.
“CUF tunataka CCM na Serikali yake itambue kwamba nguvu ya umma waliyokutana nayo katika uchaguzi huo itaongezeka maradufu kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu,” alisema Sakaya.