Nora Damian – Dar es Salaam
WAHANGA wa ukatili wa kijinsia 116,899 wametambuliwa kupitia madawati 420 ya jinsia na watoto yaliyopo katika vituo mbalimbali vya polisi nchini.
Walipata huduma katika madawati hayo katika kipindi cha mwaka 2016 hadi 2018 na kati yao 78,400 ni watu wazima na 38,499 ni watoto.
Takwimu hizo zilitolewa jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, wakati wa mkutano na waasisi wa Jumuiya ya Wanawake katika Nchi Huru za Afrika (Pawo) Tawi la Tanzania.
Mkutano huo ulikuwa na lengo la kupitia na kutoa maoni kwenye rasimu ya sera ya wanawake na jinsia ambayo inafanyiwa mapitio hivi sasa.
“Inakuwaje mtoto analawitiwa mara ya kwanza, ya pili, ya tatu mama na baba mko nyumbani. Je, tunakosea wapi? Napata kesi nyingi, mtu anakuja mtoto ameshaharibiwa.
“Kuasiwa haitatusaidia, miaka 30 jela bado ni adhabu kubwa sana, lakini watu hawaachi. Ni jukumu letu kwa pamoja kuzuia vitendo vya ulawiti na ubakaji hivyo kila mmoja atimize wajibu wake,” alisema Ummy.
Alisema madawati ya jinsia yameongeza mwamko wa wananchi katika kujiamini na kutoa taarifa za ukatili pale unapotokea kwenye maeneo yao.
Ummy alisema pia vituo vya mkono kwa mkono vya kutoa huduma kwa wahanga wa ukatili wa kijinsia vimeongezeka kutoka 10 mwaka 2017 na kufikia 13 mwaka jana.
Kwa mujibu wa Ummy, vituo hivyo vinawezesha utoaji huduma rafiki na za haraka kwa waatirika wa vitendo vya ukatili na vinahusisha wataalamu mbalimbali wakiwamo Jeshi la Polisi, ustawi wa jamii, wanasheria na madaktari.
Alisema pia watoto 6,927 wametambuliwa kupitia huduma ya simu bila malipo, yaani namba 116 kwa watoto wanaofanyiwa vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
Kuhusu sera hiyo, alisema wanawake hao waasisi wamehusishwa kutoa maoni yao kwa kuzingatia uzoefu wao katika masuala ya kukuza usawa wa jinsia.
“Serikali imetoa kipaumbele katika masuala ya kukuza usawa wa kijinsia kuyaweka kuwa ni miongoni mwa ajenda muhimu za maendeleo za kitaifa na utekelezaji wake unagusa nyanja mbalimbali,” alisema Ummy.
Katibu wa tawi la Pawo nchini, Maria Shaba, alisema utitiri wa asasi zisizo za kiserikali umesababisha wanawake kukosa chombo kimoja cha kuwasiliana na wanawake wengine wa Kiafrika duniani.
Pawo ilianzishwa Julai 31, 1962 nchini kwa lengo la kutoa msukumo wa kuwashirikisha wanawake wa Bara la Afrika katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.