Na NATHANIEL LIMU - SINGIDA -
VITENDO vya ukeketaji na ukatili wa jinsia vimeendelea mkoani hapa kutokana na kinachodaiwa kuwa wazazi kuamua kumaliza matatizo hayo kwa njia ya majadiliano na upande wa wahalifu.
Hayo yamesemwa juzi na Mkuu wa Dawati la Jinsia, Mkaguzi wa Polisi, Iddah John, wakati wa kilele cha maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili duniani yaliyofanyika katika Kijiji cha Ilongero wilayani Singida.
Alisema wanafunzi wa kile wanapopata mimba, wazazi wa binti husika humalizana kwa mazungumzo na wazazi wa mwanaume aliyesababisha hali hiyo.
“Wazazi wa mwanafunzi huyo wa kike huficha kwa makusudi tukio hilo lisijulikane kabisa, wao watafanya mazungumzo na upande uliomfanyia binti ukatili wa kijinsia.
“Kwa ujumla katika mazungumzo hayo hufanyika makubaliano ya upande ulioathirika kupata ‘kitu kidogo’, kisha kitakachofuata ni kunywa supu ya mbuzi,” alisema.
Akifafanua zaidi, Iddah alisema ni ukweli usiopingika kwamba wazazi hao, watakuwa wamemfanyia ukatili wa kijinsia binti yao kwa vile atakuwa amekatishwa masomo yake.
Mratibu huyo alisema maadhimisho hayo yanalenga kuhimiza jamii mkoani hapa kutoa ushirikiano kusaidia kutokomeza vitendo hivyo pamoja na ukeketaji.
Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Singida, Veronica Mure, alisema ukatili wa kijinsia unafanywa na kila mtu kwa kujua au kutokujua.
“Kwa hali hiyo, vitendo hivi ambavyo vipo kinyume na haki za binadamu, ni jukumu letu sisi sote kuvitokomeza, tujitambue na tuamue kwa dhati kushiriki kuvitokomeza vitendo hivyo kupitia Serikali, asasi na mashirika ya kiraia,” alisema.
Aidha mkurugenzi huyo, alisema jamii ina upungufu katika mapambano hayo, ikiwamo kushindwa au kukataa kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola katika kuvitokomeza.
“Kitendo cha ukatili wa kijinsia au ukeketaji kikitolewa taarifa polisi au mahakamani, kwanza mhanga wa tukio atafichwa na mbaya zaidi hakuna mtu au watu watakaokuwa tayari kushirikiana na polisi au kutoa ushahidi mahakamani,” alisema.