TANGU aajiriwe kama konstebo Januari 1979, amewatumikia watu wa Jimbo la magharibi la Madhya Pradesh kwa umahiri na uadilifu mkubwa.
Amejikusanyia karibu tuzo 200 katika safari yake hiyo ya kiaskari na kupandishwa cheo mara nne.
Ameongoza vituo vya polisi tangu akiwa msaidizi tu wa inspekta na ripoti yake ya mwisho ya siri ya mwaka inampatia daraja ‘A’.
Tuzo alizopata ni pamoja na zilizotokana na operesheni kali dhidi ya dawa za kulevya na kuzuia uhalifu dhidi ya wanawake.
Lakini akifahamika kwa ushujaa, ushupavu na ujasiri, kejeli aliyopata kutoka kwa mwanahabari mmoja kidogo imtibue nyongo.
Ushujapu na ujasiri wake wote ulikuwa kama umetoweka kufuatia simu anazopokea kutoka kwa maofisa wenzake, marafiki na namna vyombo vya habari vinavyomchukulia.
Mkewe akahangaika kumtuliza na kuzua hofu picha zake zilizosambazwa isivyo zikimkejeli kwa unene wake huenda zikasababisha astaafu mapema kabla ya wakati yaani Novemba, 2020.
Taarifa ya Twitter iliyotumwa na mwandishi maarufu nchini India Shobhaa De ndiyo iliyomuaibisha na kumvuruga polisi huyo anayeijua kazi yake vyema, ijapokuwa ikaleta matokeo chanya, ambayo hayakutarajiwa.
Ni baada ya kuweza kupata ofa ya kutibiwa bure kwa upasuaji ili kupunguza uzito wake mjini Mumbai.
De, alituma ujumbe katika mtandao wa Twitter wenye picha ya ofisa huyo wa polisi Daulatram Jogawat hivi majuzi.
Katika ujumbe wake huo alisema polisi huyo aliyeko Mumbai alikuwa na mpango wa ‘kuweka usalama mzito’ kwa ajili ya uchaguzi wa serikali ya mitaa.
Hata hivyo, mwandishi huyo wa kike, alikosea kutaja kituo cha kazi cha askari huyo akitaja Mumbai badala ya Madhya Pradesh.
Ujumbe huo wa dhihaka ulisambazwa katika mitandao ya jamii ikiwamo magroup ya Whatsap kiasi kwamba Hospitali ya Saifee baada ya kuguswa ikajitolea kulipia gharama za matibabu ya upasuaji wake.
Wakati akiitikia ujumbe huo wa tweeter, Jogawat alieleza kutofurahishwa akisema unene wake umetokana na matatizo ya kiafya si ulaji vyakula, huku akisisitiza haukuwahi kuwa na tatizo katika utendaji wake wa kazi.
“Nimeumizwa mno na post ya Shobhaa De ikinidhihaki. Nimepata unene kutokana na matatizo ya kiafya kufuatia operesheni ya kibofu mwaka 1993,” Inspekta Jogewat akiviambia baadhi ya vyombo vya habari vilivyomfuata kupata maoni yake baada ya taarifa hiyo kusambaa.
Kufuatia utata kuhusu tweet ya De, hospitali kadhaa zikajitokeza kutoa ofa ya kumpatia tiba bure inspekta huyo.
Dk. Muffazal Lakdawala, Mmwenyekiti wa Kituo cha Sayansi ya Upasuaji na Utafiti alitegemea Daulatram atapoteza uzito taratibu ndani ya mwaka na kurejea katika maisha ya kawaida.”
Baada ya kusikia hali yake kupitia taarifa hiyo, Dk. Lakdawala alimtafuta na kumpa ofa ya kumtibu.
“Rafiki yangu nahisi unahitaji msaada wa kimatibabu na nadhani upasuaji wa bariatric utakusaidia, niamini tafadhali,” Dk. Lakdawala alitweet.
Katika taarifa yake rasmi, mtaalamu huyo wa afya alisema; “nikiwa daktari nahisi kuwa ni wajibu wangu kumsaidia mgonjwa aliye katika shida hasa iwapo inaweza kuimarisha afya yake na kuokoa maisha.”
Wakati niliposikia kuhusu masaibu ya Daulatram Jogawats nilihisi naweza kumsaidia kumrudisha katika hali ya kawaida na hivyo nilimtafuta,” Lakdawala alisema.
Hospitali hiyo ilisema kuwa Inspekta Jogawat anaendelea vyema baada ya upasuaji, na uzito wa mwili wake unaweza kupungua hadi karibu kilo 80 mwaka ujao.
Awali kabla ya upasuaji huo alikuwa na uzito wa kilo 180.
Upasuaji huo kwa lugha ya kitaalam -Bariatric surgery, hutumiwa kama tiba ya mwisho kwa mtu mwenye unene wa kupindukia unaoweza kumsababishia madhara ya kiafya.
Awali pia Hospitali ya Saifee iligonga vichwa vya habari Januari mwaka huu, ilipoanza shughuli zake kwa kumtibu mwanamke mmoja raia wa Misri, ambaye aliaminika kuwa mtu mwenye uzito mkubwa zaidi duniani akiwa na uzito wa mwili wa kilo 500.
Jogawat aliliambia gazeti la Hindustan Times kwamba alipata ‘fursa ya kwenda Mumbai kwa mara ya kwanza kwa ajili ya matibabu, kwa sababu ya ujumbe huo wa Twitter.
Aliongeza kwa kusema kuwa uzito wa mwili ulianza kuongezeka kutokana na matatizo ya kiafya na si kwa sababu ya kula sana kama inavyodhaniwa.
“Kusema ukweli, uzito wangu haukuja kutokana na kazi yangu kwa sababu nilikuwa mwenye nguvu na mkakamavu kimwili na nilikuwa na akili ya kutatua uhalifu. Nilikuwa nalipwa vyema na kazi yangu,” alisema Jogawat.
Baadaye mwandishi wa habari Shobhaa De baadae alitetea ujumbe wake wa Twitter, akisema kuwa azma yake haikuwa kumuudhi yeyote.