NA OSCAR ASSENGA, KOROGWE.
TATIZO la uhaba wa nyumba za walimu wilayani Korogwe mkoani Tanga, limesababisha walimu kushindwa kuishi kwenye shule wanazopangiwa kutokana na miundombinu kutokuwa rafiki.
Hayo yalisemwa juzi na Kaimu Ofisa Elimu Sekondari wa Halmashauri ya Korogwe, Martha Kusare, wakati wa upokeaji majengo matatu ya maabara yaliyojengwa na Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Vuga Development Initiative ya mkoani Arusha, ikishirikiana na A Better World kutoka nchini Canada kwa Shule ya Sekondari ya Patema iliyopo Kata ya Mpale.
Alisema hali hiyo imekuwa kikwazo kikubwa cha wanafunzi kushindwa kufikia malengo yao ya kitaaluma na kuiomba Serikali kuona namna bora ya kuanzisha ujenzi wa nyumba za walimu kwenye maeneo ya vijijini, kwani kuna uhaba mkubwa kutokana na kukosekana hata nyumba za kupangisha.
Alisema kitendo cha kukosekana kwa nyumba za walimu kwenye maeneo ya shuleni kumechangia hata kuwapo kwa tatizo la utoro wa wanafunzi wao na hivyo kama halmashauri wamejipanga kukabiliana nalo kwa vitendo ili kulimaliza.
“Ukiangalie hivi sasa walimu wanaopangiwa maeneo ya vijijini wanafika kuripoti na kukaa kwa miezi kadhaa na wanapoona hakuna mazingira mazuri, wanalazimika kuhamia maeneo mengine, kitendo ambacho ni hatari kwa maendeleo ya sekta ya elimu,” alisema.
Hata hivyo, alisema wanaishukuru watu wa Canada kwa kushirikiana na Vuga kusaidia kumaliza nyumba ya mwalimu shuleni hapo.
Naye Mkurugenzi wa taasisi hiyo, Azidu Kaoneka, alisema umaliziaji wa maabara hizo, nyumba moja ya walimu na kuwawekea kifaa cha kuzalisha umeme kupitia jua (mobisol), vimegharimu Sh milioni 75.