Na MWANDISHI WETU
HIVI majuzi Tasisi ya Utafiti ya Twaweza kupitia mradi wake wa ‘Uwezo Tanzania’ ilitoa mafunzo kwa watu watakaojitolea kuwahoji wanafunzi ili kupima uwezo wa watoto katika KKK yaani Kusoma, Kuandika na Kuhesabu.
Mradi huo una lengo la kusaidia Serikali na jamii kufahamu changamoto katika uelewa wa watoto na kuzitafutia ufumbuzi.
Zaidi ya wanafunzi 40,000 wenye umri kati ya miaka sita hadi 16 wanatarajiwa kupimwa uwezo wao na wahojaji zaidi ya 3,300 kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Meneja wa Mradi huo, Zaida Mgalla anasema upimaji huo utasaidia kupata njia bora za kutatua matatizo ya watoto katika masuala ya elimu.
“Tathmini hii ina tija kubwa kwa Taifa, baadaye tutaandaa ripoti na kuikabidhi kwa serikali ili hatua za haraka zichukuliwe kuhakikisha sekta ya elimu inakuwa nzuri na kuwezesha kupata wataalamu mahiri,” anasema.
Wakati tathmini hiyo ikifanyika maeneo mbalimbali nchini, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, wahojaji 60 wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kufahamu namna ya kutathmini kikamilifu ili kupata taarifa sahihi na kwa wakati.
Mratibu wa Uwezo wa wilaya hiyo, Yonah Mahuli anasema tathmini kama hiyo ina umuhimu mkubwa hasa ikizingatiwa inaangazia elimu ambayo ni moja ya silaha ya kupambana na adui ujinga.
Mahuli anasema katika wilaya hiyo kila kitongoji kitakuwa na kaya 20 zitakazofanyiwa tathmini.
Akizungumzia changamoto zinazoikabili wilaya hiyo katika suala la elimu, anasema umbali wa shule zilipo ni jambo linalowaumiza mno.
Anasema umbali ni miongoni mwa vikwazo kwa wanafunzi kuhakikisha wanajifunza vema na wanapata kile wanachostahili.
“Wako watoto ambao wanatoka zaidi ya kilomita 15 kwa miguu kuifikia shule ilipo, atawezaje kukaa darasani na kufanya kazi zake vizuri wakati akiwa amechoka?” anahoji Mahuli.
Changamoto hiyo inaungwa mkono na mmoja ya wahojaji wa kujitolea, Wilson James anayetokea Kijiji cha Sale wilayani Ngorongoro.
James anasema: “Vuta picha mtoto anatoka umbali wa kilomita 20 kuifikia shule, hivi atawezaje kusoma? Mtoto kama huyo unamsaidiaje ili aweze kufikia lengo lake kama ambavyo wengine walivyofanya hadi kufanikiwa.” Akizungumzia suala la elimu linavyopewa kipaumbele katika kijiji anachotoka, anasema wazazi wengi hawana mwamko na elimu, jambo ambalo linasababisha kuwapo kwa vijana wengi wasiosoma.
“Mtoto anaambiwa akachunge ng’ombe muda wa shule, au wakati wa kilimo analazimishwa aende shambani akalime huku masomo yakimpita. Hii ni changamoto kubwa ambayo kwa namna moja au nyingine inahitaji utatuzi wa haraka ili kuikomboa jamii,” anasema James.
Anasema wakazi wa kijijini hapo hawana mwitikio wa kuhudhuria vikao vya shule ikilinganishwa na baadhi ya maeneo nchini, jambo linalosababisha mateso kwa watoto wengi.
James anasema ni muhimu kufanya tathmini kwa sababu itawaamsha wazazi wanaodhani kuwa elimu haina manufaa kwao.
Kwa upande wake Mariana John ambaye ni miongoni mwa mahojaji wa kujitolea, anasema tathmini hiyo itawaamsha wazazi kuwahimiza watoto wao kwenda shuleni.
Anasema pia itamwezesha mzazi kukagua madaftari ya watoto, kumtafutia cheti cha kuzaliwa na kumhamamisha zaidi, kama ambavyo maswali ya Uwezo yanavyouliza katika madodoso.
Anasema: “Uwezo inauliza swali rahisi tu je, watoto wetu wanajifunza? Swali hilo linajibiwa na taarifa ya tathmini ambayo Uwezo inasambaza kwa kuangazia viwango vya kujifunza ili kujenga uelewa na kuwahamasisha wale wanaojali kuhusu kujifunza kwa watoto na kuchukua hatua za kuboresha elimu.”
Naye Ofisa Elimu wa wilaya hiyo, Emanuel Sukums anasema suala la elimu ndani ya wilaya hiyo ni gumu hasa kwa jamii ya wafugaji ambao muda mwingi wanataka kuona watoto wao wakichunga.
“Tunajitahidi kuboresha elimu na kupambana na wazazi kama hao kwa kuwapa ushauri, pia tuko katika mchakato wa kujenga mabweni katika shule zilizo mbali na makazi ya wanafunzii ili iwe rahisi kwao kuhudhuria mazomo,” anasema Sukums.