25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TUTAWASHANGAZA

Winfrida Mtoi -Dar es salaam

YANGA na Azam FC leo zinashuka dimbani katika nchini tofauti kucheza michezo yao ya marudiano  ya kimataifa inayoandaliwa na Shirikisho la Soka Afrika(Caf).

Yanga itakuwa dimbani Uwanja wa Levy Mwanawasa mjini Ndola nchini Zambia kuumana na Zesco United, katika mchezo wa marudiano wa raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Timu hizo zilipokutana Septemba 14, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Yanga ilibanwa mbavu na Zesco kwa kulazimishwa sare ya bao 1-1.

Ili kusonga mbele kutinga hatua ya makundi, vijana hao wa Jangwani wanatakiwa kuhakikisha wanapata ushindi au sare ya kuanzia mabao mawili na kuendelea.

Hata hivyo, vita hiyo haitakuwa nyepesi kwa Yanga kwa kuzingatia rekodi ya wapinzani wao Zesco ambao hawatawahi kupoteza mchezo kwenye uwanja wao huo, tangu walipoanza kuutumia mwaka 2012.

Timu hizo zina rekodi tofauti katika michuano hiyo,  mafanikio ya juu zaidi kwa Yanga ni kutinga hatua ya makundi mwaka 1998, wakati Zesco ilifika nusu fainali mwaka 2016.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera anajivunia uimara wa safu yake ya ulinzi na kiungo ambazo zimeonesha ukomavu wa hali ya juu.

Mabeki Kelvin Yondan na Lamine Moro aliyesajiliwa msimu huu, wamekuwa wakitengeneza ukuta mgumu kupenyeka.

Kwenye kiungo Papy Tshishimbi, Feisal Salum ‘Fei Toto’, Abdulazizi Makame, Mohammed Issa ‘Mo Banka,’ wamekuwa na uelewano mzuri.

Eneo ambao limekua likimuumiza kichwa Zahera ni ushambuliaji ambalo katika michezo  iliyopita lilionekana kukosa ubunifu wa kutupia mabao.

Hata hivyo, kocha huyo amekuwa akilifungia kazi  mazoezini ili kuhakikisha linakuwa na makali ya kutosha.

Eleo la ushambuliaji la Yanga limekuwa likiongozwa na Mganda Juma Balinya na raia wa Namibia, Sadney Urikhob.

Patrick Sibomana na Mrisho Ngassa ni wazi watacheza kama mawinga huku Ally Mtoni ‘Sonso’ na Mapinduzi Balama wakitarajiwa kucheza kama mabeki wa pembeni.

Upo  uwezekano mkubwa Zahera akafanya mabadiliko kutokana na makosa aliyoyaona katika mchezo uliopita hasa eneo la ushambuliaji, huenda Balinya akaanza pamoja na Sadney.

Pia kurejea kwa Issa Bigirimana ambaye aliukosa mchezo uliopita kutokana na majeraha kutampa Zahera wigo mkubwa wa kuchagua nani aanze katika safu yake ya ushambuliaji.

Yanga wanatakiwa kujipanga zaidi katika mchezo huo, kwani historia inaonyesha Zesco ni timu hatari zaidi inapokuwa katika dimba lake la nyumbani.

Wazambia hao wanaolewa na kocha wa zamani wa Wanajangwani hao, George Lwandamina  wametoka kushinda mechi zake tatu za Ligi Kuu nchini humo.

Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila, alisema wataingia uwanjani wakiwa na mtazamo chanya wa kupata ushindi, kwa sababu timu zote zina nafasi ya kusonga mbele.

“Dakika 90 ndio zitazungumza kama ilivyokuwa katika mchezo wetu wa Dar es Salaam, wachezaji wote wapo katika hali nzuri, kila mchezo una changamoto zake lakini sisi tumejipanga kwa hali yoyote tukiwa na nia moja ya kushinda,” alisema Mwandila.

Kwa upande wake wa nahodha wa Zesco, Jacob Banda alisema wana faida ya kutumia uwanja wa nyumbani na morali ya wachezaji ni kubwa,  wakiamini watashinda.

“Kucheza nyumbani mechi kama hii ni faida kwetu, tutacheza kwa kufuata muongozo tuliopewa na mwalimu wetu, tukilenga ushindi, licha ya kuwa wapinzani wetu nao wamejiandaa,” alisema Banda.

Ukiachana na mchezo huo, wawakilishi wengine wa Tanzania, Azam watakuwa nchini Zambabwe kuvaana na Triangle United,  katika mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo wa kwanza kati ya timu hizo uliopigwa Uwanja wa Azam Complex jijini Dar es Salaam na Azam kuchapwa bao 1-0.

Matokeo hayo yanailazimisha Azam kushinda mabao 2-0 au 3-1, ili kusonga mbele kwa kutinga hatua ya makundi ya michuano hiyo.

Akizungumza  kwa simu kutoka Zimbabwe, Kocha Mkuu wa Azam, Etienne Ndayiragije alisema kuna udhaifu aliuona katika mechi iliyopita,  ikiwamo umakini mdogo wa washambuliaji wake katika  kutumia nafasi wanazopata, lakini  tayari amepata mwarobaini.

Ndayiragije  alisema akili yao wameielekeza kutafuta namna gani watapata matokeo mazuri lakini si kufikiria kilichotokea Azam  Complex.

“Tuna changamoto ya hali ya hewa kwa sababu huku ni baridi, ila hiyo si tatizo , nimewaandaa wachezaji wangu na kuwaambia waondoe hofu, popote tunaweza kushinda, kinachotakiwa ni kupambana,” alisema Ndayiragije.

Timu nyingine ya Tanzania itakayokuwa dimbani leo ni  Malindi FC  ya visiwani Zanzibar.

Malindi itakuwa ugenini nchini Misri kukabiliana na Al Masry,  ukiwa ni mchezo wa marudiano wa Kombe la Shirikisho Afrika.

Mchezo wa kwanza ulipigwa Uwanja wa Amaan, Zanzibar ambapo Malindi ilitandikwa mabao 4-1.

Matokeo hayo ni wazi yameiweka Malindi katika mhitani mgumu wa kupindua ‘meza’ ugenini ili kutinga hatua ya makundi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles