KLONG TOLEI, THAILAND
”KUNA uwezekano wa mimi kufa kwa njaa kuliko kwa virusi,” anasema Pantira Sutthi, muuza chakula anayeishi kwenye eneo la makazi duni ya Klong Toei nchini Thailand.
Eneo hilo lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1.5 huishi watu wenye vipato duni, nyumba zao ndogo zimejengwa kwa mbao zilizochakaa na rangi zilizofubaa.
Sutthi ni mama anayemlea mtoto wake pekee na mjukuu bila msaada wowote.
Huishi kwa kuuza kuku wa kukaanga na nyama katika shule moja iliyo karibu.
Lakini chanzo chake kikuu cha kipato kwa sasa kimetoweka kutokana na janga la corona, lililosababisha shule kufungwa.
Mara akawa ametoka kwenye kupata kiasi cha dola 30 kwa siku na hatimaye sasa hapati chochote.
Ameathirika kwa kiasi kikubwa na virusi, kama ilivyo kwa watu wengine 20,000 wanaoita eneo hili la Klong Toei nyumbani kwao.
Kwa Sutthi, kuhifadhi chakula ndani kwa ajili ya familia yake ni changamoto kuliko kununua vitakasa mikono au barakoa.
”Ni bahati kuwa hakuna hata mmoja kwenye jamii yetu aliyeathirika, hivyo sitaugua wala kufa kutokana na virusi. Lakini umasikini utatuua taratibu,” alisema na kuongeza;
”Nina matumaini tu kuwa hali itaimarika hivi karibuni, na nina matumaini serikali yetu itatusaidia.”
Katika hali ya kutokuwepo kwa watoto na wateja wengine kununua chakula anachopika, Sutthi hawezi kukidhi mahitaji yake.
Sutthi na familia yake sasa huishi kwa kutegemea chakula cha msaada
”Ninataka kweli kwenda nje kuuza chakula na kupata fedha,” anasema .
”Lakini sina pesa za kununua chakula changu mwenyewe- wapi nitaweza kupata fedha ya kununua kuku na nyama kwa ajili ya kuuza? ”
Anaishi kwa kupata msaada wa chakula kutoka ofisi za misaada na kwenye masinagogi.
”Kila ninaposikia kuhusu watu kutoa chakula bure kwenye eneo hili, ninakwenda na kujaribu kuchukua chakula cha kutosha kwa ajili ya familia yangu yote. Ninaogopa virusi, lakini kwa rasilimali chache na fedha hii ni njia pekee ya kuishi,” Sutthi anasema.
Mbali na dawa za kulevya na wizi, hakuna uchaguzi wa kazi walionao watu wanaoishi katika maeneo duni.
Kama ilivyo kwa wengine wengi, Thongrueng Thongphuen mwenye miaka 56 anayefanya kazi kama kibarua anahangaika kupata fedha za kujikimu hivi sasa.
Sambamba na mumewe huondoka kila siku kwenda mtaani karibu na makazi yao kwa ajili ya kutafuta kazi za kibarua.
Anafahamu kuhusu ushauri wa serikali wa kutotoka nje, lakini anahisi ni muhimu kutoka ili aweze kujipatia kipato kwa ajili ya kuishi.
”Watu masikini kama sisi hawana namna ya kufanya. Ninajua serikali inamtaka kila mmoja kusalia nyumbani. lakini kama sitatoka nje kujipatia fedha, hakuna atakayeweza kuishi ,” hongphuen alieleza.
”Hakuna aliyetupa kibarua, tuko hatarini kupata maambukizi ya virusi tunapokuwa nje na huenda tukavibeba kuvipeleka kwenye jamii yetu. Lakini tutafanya nini? Watoto wangu lazima wapate chakula na watu wanaonidai huja kuchukua fedha zao nilizokopa. Niko katika shinikizo kubwa. Wakati mwingine, sioni umuhimu wa kuishi,” alisema.
Watu wanaoishi katika makazi duni ya Klong Toei wanakisiwa kuwa 100,000
Klong Toei ni eneo kubwa zaidi la makazi duni nchini Thailand. Takribani watu 20,000 wanaishi eneo hili- ingawa idadi kamili inaaminika kuwa juu zaidi, labda karibu 100,000.
Nyumba katika eneo hilo zimejengwa katika mazingira ya msongamano, hali ambayo ni rahisi ugonjwa kusambaa.
Watu wengi katika makazi hayo wanafahamu kuhusu virusi vya Covid-19, lakini kwa rasilimali walizonazo, hakuna cha kufanya zaidi ya kusaidiana wenyewe.
”Watu wengi katika jamii hii ni watoto, wazee, na wagonjwa wasioweza kutembea. Iwapo itatokea hatari ya maambukizi kwa mtu mmoja tu, jamii yote itakuwa hatarini,” mkazi mwingine, Sanitmueanwai anaeleza.
Ladda Mangmeepol ana miaka 26 anaishi kwenye eneo la makazi duni. Anatengeneza barakoa na kuwapa watu bure.
”Mimi ni mmoja kati ya watu wenye bahati ambao wamekuwa wakizitunza familia zao. Lakini nimekuwa nikiwaona shangazi zangu, wajomba, na majirani wanavyohangaika kwenye hali hii.”
”Wote ni vibarua na hakuna kazi kwa ajili yao kwa sasa. Huu ni mwezi wa kwanza wa janga mjini Bangkok na watu tayari wanapata tabu. Siwezi kufikiri hali itakuwa vipi mwezi ujao.”
”Hali inaogopesha yalipo makazi yangu: kuna mtu mmoja aliye na maambukizi ya Covid-19,” anaongeza Mangmeepol.
”Nina wasiwasi kuwa watu wengi kwenye jamii yote wataambukizwa na kupoteza maisha kutokana na virusi hivi.”