TUNIS-TUNISIA
MAELFU ya raia wa Tunisia wanajiandaa kwa uchaguzi wa mapema unaotarajiwa kufanyika Septemba 15 baada ya rais wa kwanza wa taifa hilo la Afrika ya Kaskazini, Beji Caid Essebsi kufariki dunia, na kuzikwa juzi katika maziko yaliyohudhuriwa na wengi.
Essebsi, aliyechaguliwa kwa njia ya kidemokrasia, alifariki dunia akiwa na miaka 92 katika hospitali ya kijeshi baada ya kuugua. Kifo chake kinatishia mgogoro wa kisiasa katika taifa linaloonekana kutokuwa na mafanikio ya kisiasa kufuatia maandamano yaliyokumba ulimwengu wa kiarabu.
Rais wa Ufaransa, Emmanuel Macron na viongozi wengine wa kigeni walisafiri nchini Tunisia kutoa heshima zao za mwisho kwa kiongozi huyo mkongwe. Spika wa Bunge la Tunisia, Mohamed Ennaceur, aliyeapishwa kuwa rais wa mpito, alimtaja Essebsi kama mwasisi wa maridhiano ya kitaifa.