Na Patricia Kimelemeta, Dar es Salaam
JOPO la mawakili 11 wakiongozwa na Michael Ngallo na Peter Kibatala jana walijitokeza katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa ajili ya kumtetea Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema).
Lissu alipandishwa kizimbani jana katika mahakama hiyo na kusomewa shtaka moja la kutoa maneno ya uchochezi kinyume na kifungu namba 32(1)(b) cha sheria ya magazeti iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mawakili wengine wanaomtetea Lissu ni pamoja na John Mallya, Nehemia Mtobesya, Fredrick Kihwelo, Omary Msemo na Juma Nassoro, wakati upande wa jamhuri ulikuwa na mawakili, Salum Mohamed na Nassoro Katuga.
Katika kesi hiyo, upande wa Jamhuri ulikua na mawakili watatu ambao wameongozwa na Wakili Mkuu wa Serikali, Bernard Kongola na kusoma hati ya mashtaka mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Dk. Yohana Yongolo.
Wakili Kongola, alidai mahakamani hapo kuwa, mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo jipya mnamo Julai 28, mwaka huu katika eneo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyopo Ilala jijini Dar es Salaam.
Alidai kuwa kwa nia ya kushawishi na kudharaulisha wananchi wa Tanzania dhidi ya mamlaka halali ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mshtakiwa huyo alitoa maneno ya uchochezi yaliyosomeka.
“Mamlaka ya Serikali mbivu ya kidikteta uchwara inahitaji kupingwa na kila Mtanzania kwa nguvu zote.
“Huyu dikteta uchwara lazima apingwe kila sehemu kama uongozi utafanywa na utawala wa kijinga nchi itaingia ndani ya giza nene”.
Alidai kuwa, upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba mahakama hiyo kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kusomewa maelezo ya awali(PH).
Hata hivyo, Lissu alikana shtaka hilo na Wakili Kongola aliiomba mahakama hiyo kutoa masharti magumu ya dhamana kwa sababu mshtakiwa huyo ni mtuhumiwa mzoefu.
Wakili Kongola, alidai kuwa mahakama hiyo inapaswa kutoa angalizo kwa mshtakiwa huyo kabla ya kumpa dhamana kwa sababu , siku aliyotenda kosa hilo alitoka kupandishwa kizimbani kwenye kesi nyingine iliyokua inamkabili yeye na wenzake watatu lakini alidhaminiwa.
Alidai kuwa, alipotoka mahakamani hapo, alitoa lugha ya uchochezi iliyosababisha kupandishwa tena kizimbani kwa mara nyingine, hali inayoonyesha wazi kuwa, mshtakiwa huyo hana hofu na mahakama.
“Mshtakiwa anaonekana hana hofu na mahakama, ndiyo maana alipotoka mahakamani kwenye kesi nyingine akarudia kutenda kosa lile lile, kwa sababu anaiona mahakama ni kitu cha kawaida na ni mzoefu wa mahakama ninaiomba mahakama yako kuweka masharti magumu ambayo yatamfanya awe na hofu na mahakama,”alidai Kongola.
Hata hivyo, upande wa utetezi ukiwakilishwa na Kibatala ambaye alidai kuwa, hoja zilizotolewa na upande wa Jamhuri hazina mashiko kwa kuwa mshtakiwa huyo ni mtiifu na kwamba ameweza kwenda mwenyewe kituo cha polisi kati baada ya kuitwa.
Baada ya kujitokeza kwa hoja za pande zote mbili, Dk. Yongolo alisema kuwa, hati ya dhamana kwa mshtakiwa huyo ipo wazi na kuwataka kuwa na wadhamini wawili ambao kila mmoja atasaini bondi ya Sh milioni 2.
Hata hivyo, mshtakiwa huyo alikidhi masharti ya dhamana na Dk. Yongolo, alitoa masharti mengine ikiwa ni pamoja na kumtaka kutosafiri nje ya nchi bila kibali cha mahakama hiyo.
Kesi hiyo imehairishwa hadi Agosti 2, mwaka huu itakapoanza kusomewa maelezo ya awali, ambapo tangu saa tatu asubuhi, Jeshi la Polisi liliimarisha ulinzi katika maeneo hayo huku kukiwa na polisi wenye silaha wakitanda kila kona.
Alivyowasili
Tundu Lissu aliwasili majira ya 6:55 katika viwanja ya mahakama hiyo akiwa kwenye gari la polisi la wazi lenye namba za usajili T 671 BEQ na kusindikizwa na polisi wawili waliovaa kiraia.
Baada ya kuwasili, wanachama wa chama hicho walijitokeza karibu na gari hilo na kuanza kupiga kelele za ‘Peoples Power’ huku wengi wao wakiwa wamevalia sare za Chadema ambapo ilipofika saa 7:30 mbunge huyo alipandishwa kizimbani.
Baada ya kuachiwa kwa mbunge huyo ambaye pia ni Mwanasheria Mkuu wa Chadema, wafusi wa chama hicho walitoa mabango yao na kuyaonesha juu ambapo wafuasi watatu walijikuta wakiishia katika mikono ya polisi.
Kwa upande wake Lissu, alisema kuwa alitegemea Serikali ingekua na busara na kuamua kukaa kimya baada ya kuzungumza suala hilo, lakini kilichofanyika ni kumkamata na kumpandisha kizimbani.
Maisha ya selo
Alisema alipokuwa ndani mahabusu katika Kituo cha Polisi Kati, alishuhudia unyanyasaji wa mahabusu unaofanywa na vyombo vya ulinzi na usalama.
“Nimelazwa chumba cha mahabusu ya kawaida kama wanavyolazwa watuhumiwa wengine wanaofikishwa kituo cha kati cha polisi,” alisema.