27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

TUNAMPONGEZA WAZIRI MKUU KWA RAI HII

HATIMAYE Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa rai kwa mawaziri na manaibu wao kuepuka kutoa matamko yasiyotekelezeka ili kuepusha mikanganyiko serikalini.

Waziri Mkuu Majaliwa ametoa rai hiyo kwa wasaidizi wake, mawaziri na manaibu waziri ikiwa tayari baadhi yao wameishatoa matamko yaliyoleta mkanganyiko katika jamii.

Katika rai yake hiyo aliyoitoa wakati akifungua mkutano wa mawaziri juzi mjini Dodoma,  Waziri Mkuu Majaliwa aliwataka mawaziri na manaibu waziri kujiridhisha na matamko wanayokusudia kuyatoa kwa wananchi kabla ya kusimama hadharani kuyatamka.

Rai hii tunakubaliana nayo kwa sababu tunaamini kiongozi wa ngazi ya waziri au naibu waziri anapaswa kujiridhisha na tamko lake kabla ya kulitoa kwa wananchi iwapo halina athari zozote mbaya za kisera au kibajeti.

Tunachukua fursa hii kumpongeza Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuiona dosari hii miongoni mwa wasaidizi wake na hatuna shaka hata kidogo kuwa itaimarisha mawasiliano ya kiutendaji na utoaji wa uamuzi katika kazi zao serikalini

Tunapompongeza Waziri Mkuu, tunawapenda kuwaasa viongozi wengine wakiwemo wakuu wa mikao na wilaya kuzingatia miongozo ya utendaji kazi wao na kuwatumia vizuri watendaji wanaowazunguka ili utekelezaji wa majukumu yao usiache maswali yasiyokuwa na majibu kwa wananchi wala kuibua mkanganyiko katika ofisi walizopewa dhamana ya kuziongoza..

 

Aidha, ni rai yetu kwa viongozi hawa waepuka kuchukua uamuzi unaweza kujenga hofu kwa walio chini yao ikiwemo kuamuru watiwe ndani, kuchapwa bakora au kuwafokea hadharani. Watambue kuwa kiongozi mzuri ni yule anayeelekeza na kuonyesha njia.

Kama alivyotoa rai Waziri Mkuu Majaliwa ambaye tumempongeza, sisi pia tumesukumwa kuungana naye kuwarai viongozi wetu baada ya kuona dosari hizi ndogo ndogo ambazo awali Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alizozitolea kauli ya maelekezo na maonyo.

Tunapenda viongozi wetu watambue kuwa maneno na vitendo vyao vina athari za moja kwa moja kwa wanaowaongoza ambao huvitafasiri kila mmoja kwa kadri ya uelewa wake.

Kwa sababu hiyo, tunawaomba viongozi wetu wazingatie ushauri na maelekezo ya Makamu wa Rais, |Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu Majaliwa kwa kufanya rejea za athari za tamko la Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) George Kakunda aliyekaririwa akieleza kuwa hakuna msichana atakayeolewa bila kuwa na cheti cha kidato cha nne na baada ya kuibua sintofahamu kwa jamii alilamizimika kuitolea ufafanuzi.

Sambamba na rejea hiyo, nyingine iyopaswa kuwasukuma viongozi wetu kuzingatia ushauri waliopewa na Makamu wa Rais na Waziri Mkuu ni kuhusu bomoa bomoa ya nchi nzima.

Kauli hii ilimfanya kwanza Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paulo Makonda kuizungumzia na baadaye Rais Dk. John Magufuli naye  aliizungumzie kwa kutoa ufafanuzi kabla ya kumtaka waziri naye kuitolea ufafanuzi wa kina.

Tanzania inabadilika kwa kasi, watanzania wanayakubali mabadiliko wanayoyapitia na wanawaunga mkono viongozi wao hivyo tamko lolote la kiongozi wanalichukua kwa uzito mkubwa.

Inapotokea tamko hilo linaacha maswali yasiyokuwa na majibu kwa wananchi usumbufu unaojitokeza kwao ni mkubwa na ndani ya serikali kunakuwa na mkanganyiko unaowalazimu viongozi wakuu wa kitaifa kusimama kutoa kauli za kurekebisha mkanganyiko.

Hatupendi mikanganyiko ya aina hii iendelee kuwaandama viongozi wetu na hatupendi wananchi waendelee kubaki na maswali yasiyokuwa na majibu kwa kauli zinazotolewa na viongozi wetu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles