Na Jamila Shemni, Dar es Salaam
SERIKALI na kampuni mbalimbali, zimeombwa kuhamasishwa ili kuwekeza zaidi katika ulinzi wa masuala ya usalama wa mitandao kama nyenzo kuu ya kuepukana na athari za uhalifu wa mitandao, kwani inarudisha nyuma mendeleo ya nchi na mataifa mengine.
Akizungumza na MTANZANIA mwishoni mwa wiki, mtaalamu wa masuala ya usalama mitandaoni, Yusuph Kileo, alisema mataifa mbalimbali duniani yameanza kujipanga kikamilifu kukabiliana na tatizo la uhalifu mitandaoni kwani linachukua taswira mpya na kuathiri nchi mbalimbali.
“Mwaka huu uhalifu wa mitandao unategemewa kuchukua taswira nyingine ambapo vita vya mitandao kati ya mataifa na kampuni vinategemewa kukua na hivyo kuhamasisha mataifa mbalimbali duniani kuanza kujipanga kukabiliana na hali hii,” alisema.
Aliongeza kwamba, sambasamba na ukuaji wa teknolojia, uhalifu wa mitandao umeongezeka huku wizi wa fedha katika mitandao ukishika kasi zaidi.
“Mataifa kadhaa yameanza kuchukua hatua stahiki kukabiliana na hali hii, huku ujuzi wa kukabiliana na hali hii ukihimizwa kufikishwa katika mataifa mbalimbali kuweza kupunguza matukio ya wizi wa fedha mitandaoni,” alisema Kileo.
Alitolea mfano ujenzi wa miundombinu ya barabara unaondelea sasa ambapo alishauri wajenzi kutafakari kutengeneza njia stahiki zitakazoweza kupitisha mifumo ya kimtandao katika barabara hizo wakati ujenzi ukiwa unaendelea.
Kileo ameitaka jamii katika kila ngazi kuhakikisha kuna umakini katika matumizi salama ya mitandao kwani athari zinazosababishwa na uhalifu wa mitandao ni kubwa na husababisha kudorora kwa uchumi wa mataifa mengi.
Hivi karibuni, Rais wa Ufaransa kupitia Jukwaa la Uchumi wa dunia jijini Davos, alihimiza mataifa kuwekeza zaidi katika masuala ya ulinzi katika mitandao.