WIKI hii tumeshuhudia kwa mara nyingine tasnia ya habari ikitikiswa.
Hii si mara ya kwanza, tumepata kusikia kauli na kuona matendo ya baadhi ya viongozi yanayotoa taswira ya kutisha uhuru wa habari.
Matukio mawili ambayo wiki hii yametoa ishara ya kile tunachokiita kutikiswa kwa tasnia ya habari, ni kitendo cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kuvamia kituo cha redio na televisheni cha Clouds akiwa na askari wenye silaha za moto.
Tukio la pili ni uamuzi wa Rais, Dk. John Magufuli, kumwondoa kwenye nafasi yake aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, ikiwa ni siku moja tu tangu kiongozi huyo akemee na kuchukua hatua dhidi ya tukio la kuvamiwa kwa Clouds.
Kutokana na msingi huo, sisi kama chombo cha habari chenye wajibu mkubwa katika jamii wa si tu kuhabarisha, bali pia kuonya, kutengeneza ajenda kwa ajili ya mustakabali mwema wa Taifa nk., tunadhani ni vizuri viongozi wetu wakazingatia utawala wa sheria.
Kwa ufupi, utawala wa sheria ni mahusiano kati ya wale wanaotawaliwa na wale wanaotawala.
Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, utawala wa sheria umewekewa misingi katika ibara ya 3, 4, 13.
Kwa mfano, Ibara ya 12 imefafanua kwa kina juu ya usawa mbele ya sheria na kuelezea kama ni moja ya nguzo muhimu katika utawala.
Ibara hizo zinafafanua kuwa, pasipo kubagua, kila mtu ana haki ya kulindwa na kupata haki sawa na yeyote mbele ya sheria.
Kwa mujibu wa ibara hizo, bila kujali asili, dini, rangi, jinsia wala kabila, kila mtu anapaswa kutendewa kadri ambavyo sheria inaelekeza.
Katika misingi kama hiyo, mmoja wa wanasheria alipata kuandika kuwa, sheria zinazohusu mabavu hazina nafasi katika dhana ya utawala wa sheria.
Utawala wa sheria unaaminiwa kila mahali kuwa ndiyo kiini cha mifumo ya kitaifa ya kisiasa na kisheria, inaaminika vile vile kuwa, ni sehemu muhimu ya uhusiano wa kimataifa.
Katika Waraka wa Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Dunia wa 2005, wakuu hao walikubaliana juu ya uwepo wa haja kwa dunia nzima kuheshimu na kutekeleza utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa.
Mwaka mmoja baadaye, Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa ulipitisha azimio juu ya utawala wa sheria katika ngazi za kitaifa na kimataifa na umeendelea kufanya hivyo katika mikutano yake ya kila mwaka baada ya hapo.
Kwa sababu hiyo, tunadhani ipo haja ya viongozi kutenda na kutoa kauli ambazo hazipingani na sheria wala Katiba yetu.