24.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TUENDAKO: ABSALOM KIBANDA AMWASA JPM KUJIANDAA KWA KAZI NGUMU 2020

Rais Dk. John Magufuli

Na Absalom Kibanda


NIANZE makala yangu ya leo kwa kukiri mapema kwamba kama kuna jambo gumu kwa mwandishi wa aina yangu, ni kuandika uchambuzi unaogusa mamlaka ya ukuu wa nchi au kumzungumzia Rais wa zama hizi wa kariba ya John Magufuli.

Msingi mama wa ugumu upo katika kuchanganua na kuchagua maneno stahiki ya kutumia, ili hatimaye Rais mwenyewe, wasaidizi wake na watumishi waandamizi wa mamlaka nyeti za dola walazimike hata kwa shingo upande kuamini kwamba naandika ili kushiriki katika kuchagiza na kuchangia maendeleo ya taifa langu.

Ni rahisi sana kwa yeyote kati ya niliowataja hapo juu, kufikia hatua ya ama kupuuza ushauri au mawazo ya mwanahabari anayeandika kutoka mtaani na asiyejua kwa uhakika kile kinachoendelea ndani ya vyumba vya maamuzi mazito ya kisiasa, kiuongozi na pengine kiutawala.

Nilihitimisha makala yangu Jumatano ya wiki iliyopita kwa kuanza kudokeza pasipo kufafanua, ni kwa namna na sababu gani hasa nilikuwa nikifikiri na kuamini kuwa JPM alikuwa ana kila sababu ya kuanza kurejea na kujifunda mwenyewe kupitia katika safari ya uongozi yenye mafanikio na misukosuko mingi ya kiongozi aliyemwibua katika siasa na madaraka, Rais mstaafu Benjamin Mkapa (1995 -2005).

Tafakuri yangu ya juzi, jana na leo inanifanya niendelee kuamini kwamba ukimweka kando Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, basi Mkapa ndiye rais mstaafu anayeweza akasimama na kuongoza jahazi la mafanikio ya kisiasa na kiuongozi katika mizania ya weledi na umakini kwa rais aliye madarakani.

Sitaki na wala sina sababu ya kuanza kulifafanua hilo mapema kwa Rais Magufuli mwenyewe au wasomaji wa safu hii na badala yake rejea ya ushauri ambao nimeguswa kuudokeza japo kwa sehemu tu kwa viongozi na washauri wao, inaweza ikatoa majibu ya kile ambacho nimekuwa nikikitafakari kwa muda sasa.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya taifa hili, Tanzania ina rais ambaye makuzi na malezi yake ya kisiasa na kiuongozi hayajawahi kuguswa moja kwa moja na Mwalimu Nyerere.

Kwa sababu hiyo basi, tunaye rais ambaye hana sababu wala uwezo wa kutamba kama ilivyokuwa kwa watangulizi wake watatu, Jakaya Kikwete, Mkapa na Mzee Ali Hassan Mwinyi, ambao kwa nyakati tofauti waliishi na pengine kuteswa na kivuli cha Mwalimu Nyerere.

Pengine pia kwa mfanano kidogo na Kikwete, leo hii tunaye rais ambaye akiwa Ikulu hajawahi kulazimika au kulazimishwa kwenda Butiama au Msasani na kuchota hekima, maelekezo, nasaha na uzoefu wa urais kutoka kwa Mwalimu Nyerere.

Ingawa ni kweli kwamba Kikwete aliingia Ikulu wakati Mwalimu Nyerere akiwa ameshafariki dunia, tayari alishakuwa na ‘baraka za urais’ alizopata wakati alipokwenda kumtembelea na kumweleza dhamira yake ya kutamani kuwa Rais wa Tanzania mwaka 1995, akiwa na ‘pacha’ wake wa kisiasa wakati huo, Edward Lowassa.

Nusura ya JK kukaribia kuukwaa urais mwaka 1995, mbele ya macho ya Nyerere kabla hajapewa maelekezo ya kutakiwa asubiri akue, ni ushahidi bayana kwamba alishapata baraka zake miaka 10 kabla hajaingia Ikulu.

Kwa namna ile ile ambayo Kikwete aliingia serikalini mwaka 1988 wakati Mwinyi akiwa rais, akianzia na unaibu waziri, ndivyo ilivyo pia kwa Magufuli aliyeingia kilingeni zama zMkapa akiwa madarakani kwa namna ile ile.

‘Logic’ hiyo ambayo si lazima iwe sahihi kwa asilimia 100, inaweza ikatumika kuwa ni rejea inayopaswa kumwandaa kimkakati, kimalezi na kisaikolojia JPM wakati atakapomaliza urais mwaka 2020 au 2025 kukabidhi mikoba hiyo kwa vijana waliopita katika malezi ya kisiasa ya Kikwete.

Iwapo JPM atalizingatia hilo kwa namna walivyofanya watangulizi wake, basi anaweza akajikuta akilazimika au kulazimishwa kukubali mrithi wake akatoka ama ndani ya CCM au nje ambako mtangulizi wake JK alikuwa analea vijana wengi.

Kwa muktadha wa makala hii, nitakuwa nafanya makosa kuanza kulichambua hilo la ‘vijana wa JK’ ambalo naamini linahitaji mjadala unaojitegemea, hasa nyakati hizi unaposikia zile lugha za wana CCM, akiwamo JPM mwenyewe kudai ‘CCM itatawala milele’.

Nimelazimika kuanzia hapo kama tahadhari yangu kwa Rais Magufuli ambaye natambua akili na fikra zake wakati atakapokuwa ametimiza miaka mitatu ya urais Novemba mwaka huu, zitakuwa tayari zimeanza kuuona kwa karibu zaidi mwaka 2020.

Kwa sababu hiyo basi, litakuwa ni jambo la heri iwapo washauri wa masuala ya kisiasa wa JPM na CCM yake watapaswa kuyaangalia na kujifunza mapito adhimu na thabiti aliyopita Mkapa wakati akielekea kumaliza muhula wake wa kwanza Ikulu.

Ninasukumwa kufikiri hivyo kwa kuwa ninachokiona sasa kinanipa taswira hasi, ya shaka na pengine ngumu kwa JPM na CCM yake ninayoifananisha na ile iliyomkuta Kikwete wakati akielekea kukamilisha muhula wake wa kwanza Ikulu mwaka 2010.

Katika muktadha wa wasifu binafsi, Magufuli aliingia madarakani katika mazingira yanayofanana na yale aliyoingia nayo ‘mentor’ wake Mkapa mwaka 1995, akiwa mtu ambaye wachambuzi na hata wana CCM wenzake wakiwa hawalitaji sana jina lake au kumpa nafasi kubwa ya kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Magufuli mwenyewe amepata mara kadhaa kulisema hilo hadharani, akionyesha kujua pasipo kuyataja majina ya akina Lowassa, Bernard Membe, Mark Mwandosya, January Makamba, Asha Rose Migiro na wengine kadhaa kwamba ndio waliokuwa wakitajwatajwa zaidi kuliko yeye.

Wakati akilitambua hilo, Magufuli anapaswa sasa kujifunza kutoka kwa Kikwete na Mkapa namna rais aliye madarakani anavyopaswa kuwa makini na thabiti wakati anapojiandaa kushinda urais katika kipindi chake cha pili.

Watu wenye kumbukumbu nzuri wanaweza wakawa mashahidi wazuri kwamba Mkapa alishinda muhula wake wa pili mwaka 2000 akijiamini na kwa staha zaidi kuliko ilivyokuwa mwaka 1995, kwa sababu nyingi ambazo JPM anapaswa kuzijua na pengine kuzienzi.

Pamoja na kubebwa na CCM, taasisi za dola, Mwalimu Nyerere na makada wenye sifa lukuki na pengine vyombo mahususi vya habari, haikuwa rahisi kwa Mkapa kwenda Ikulu mwaka 1995.

Upinzani mkali alioupata kutoka kwa Augustine Mrema uliwatoa jasho kweli kweli Mwalimu Nyerere, akina Abdulrahman Kinana, Jaji Joseph Warioba, Mwinyi, Kikwete, Jenerali Ulimwengu na wengi wengine.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi ilipotangaza matokeo na kuonyesha kwamba Mkapa alishinda kwa asilimia 61 ya kura dhidi ya mpinzani wake mkubwa Mrema aliyepata asilimia 28, kulikuwa na miguno ya kutoamini.

Alipoingia Ikulu, Mkapa alifanya jambo moja kubwa. Kuwaaminisha Watanzania kwamba hakupata urais kwa bahati au kwa mbeleko ya Mwalimu Nyerere na CCM iliyokuwa ikibebwa na dola. Alifanya kazi kweli kweli.

Rekodi za kisiasa, kiuchumi na kijamii alizoweka katika muhula wake wa kwanza tu wa urais, zilitosha kumjengea imani kutoka kwa Watanzania wengi zaidi.

Ulipofika mwaka 2000, Mkapa katika hali ya kujiamini, alikataa katakata kubebwa na vyombo vya dola na hata viongozi wa Serikali katika kampeni zake na akaunda timu mahususi CCM kumbeba.

Alipiga marufuku wakuu wa wilaya, mikoa na hata magari yenye namba za Serikali kuandamana naye katika kampeni za urais, akifanya hivyo makusudi asionekane kubebwa na dola.

Wakuu wa taasisi za dola za ulinzi na usalama walipata kazi kubwa kumwelewa. Ilikuwa ni kazi kubwa kwa rais aliye madarakani kujipambanua kisiasa zaidi kuliko kiserikali.

Wakuu wa mikoa na wilaya hawakuruhusiwa kusogea katika majukwaa yake ya kampeni na wala hawakutakiwa kuukaribia msafara wake wakiwa na magari yenye namba za umma.

Mkapa ambaye aliingia kilingine safari ya pili akiwa mpweke bila ya Nyerere aliyekuwa amefariki dunia mwaka mmoja kabla ya uchaguzi mkuu huo na akiwa ameshakorofishana na akina Ulimwengu na kugusa masilahi kadha wa kadha ya watu fulani fulani, aliibuka mshindi akipata asilimia 71 ya kura.

Hilo lililofanyika kwa Mkapa mwaka 2000 silioni likielekea kufanywa wakati huu Rais Magufuli anapoelekea mwaka 2020 atakapokuwa akisaka kipindi chake cha pili cha urais.

Badala yake CCM na JPM nawaona wakichukua zaidi mkondo wa makosa na kuongeza yao mengine zaidi ambayo yanaelekea kuwapeleka kule alikopita JK wakati akijongea mwaka 2010 alipokuwa akisaka muhula wake wa pili Ikulu.

JPM anapaswa kuliona au kuonyeshwa hili mapema, kwamba akifanya mchezo na yakaendelea haya ya leo, anaweza akafika mwaka 2020 akiwa katika kipindi kigumu zaidi kuliko hata ilivyokuwa kwa JK mwaka 2010.

Katika hili pia, JPM anapaswa kutambua kwamba asilimia 80 ya kura ambazo Kikwete alivuna mwaka 2005 zilikuwa zina mkono wa mafanikio ya Mkapa na zile asilimia 61 zilizotangazwa na NEC mwaka 2010 na kuibua miguno, ndizo hasa zilibeba matokeo ya kazi yake ya miaka mitano.

JPM na washauri wake wanapaswa kujua na kuzingatia ukweli mchungu kwao kwamba ilimchukua Mkapa miaka mitatu tu tangu aingie madarakani, kuzitikisa kwa maana ya kuzishawishi taasisi za kiuchumi na kifedha za kimataifa zikiwamo Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Benki ya Dunia (WB) na kundi la mataifa 12 wafadhili (Paris Club).

Katika kipindi cha kati ya Novemba 1995 wakati akiingia madarakani na Februari 1997, Mkapa alikuwa amefanikiwa kushusha mfumuko wa bei kutoka kiwango cha asilimia 27 hadi kufikia asilimia 13.8 ambacho kilikuwa hakijapata kufikiwa kwa miaka 11 kabla.

Ilipofika mwaka wa fedha wa 1996/1997, tayari Mkapa alikuwa amefanikiwa kuongeza akiba ya taifa na kufikia Dola za Marekani milioni 450, kikiwa ndicho kiwango kikubwa kupata kufikiwa wakati huo tangu Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961 na Tanzania kuzaliwa miaka mitatu baadaye mwaka 1964 kwa muungano wa Tanganyika na Zanzibar.

Ni wakati huo wa 1995-1997 ambao Magufuli alikuwa Naibu Waziri wa Ujenzi, Serikali ya Mkapa ilifanikiwa kuongeza pato lililotokana na mauzo ya bidhaa za nje ya nchi kutoka wastani wa Dola za Marekani milioni 500 zilizodumu kwa miaka mitano kabla hadi kufikia dola milioni 762.

Mafanikio hayo makubwa yalikuja wakati huo wa kipindi cha kwanza cha Mkapa yalipofanyika mabadiliko na kuanza kufanya kazi kwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Ingawa Mkapa alilazimika kupunguza wafanyakazi serikalini ili kufikia malengo hayo, ikiwa ni pamoja na kukubali kuibinafsisha iliyokuwa Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) na kuunda benki nyingine tatu, uamuzi ambao ulipingwa hadi na Mwalimu Nyerere, hatua hizo za kimfumo ziliongeza tija na nidhamu ya kazi serikalini.

Pengine rejea ya rekodi za kati ya mwaka 2000 na 2005 zama zile zile za Mkapa akiwa rais na JPM waziri kamili, zinaweza zikasaidia kumfanya rais wetu akatafakari upya njia zake na kuchukua hatua mahususi kabla ya mwaka 2020 haujawa kama ule wa JK, mwaka 2010.

Naamini JPM anatambua kwamba Mkapa aliingia madarakni wakati taifa likiwa halina akiba ya kutosha kutokana na wafadhili waliokuwa wakiongozwa na IMF na WB kutokubaliana na mwenendo wa mambo ndani ya Serikali ya Mwinyi na hivyo kusababisha mzozo mkubwa wa kifedha na kiuchumi kitaifa.

Ingawa ni kweli hatua za mwanzo kuchukuliwa na Mkapa zilisababisha uhaba mkubwa wa fedha katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo hata kuibuka kwa jina maarufu la ‘ukapa’ linaloendana na hili la leo la ‘vyuma kukaza’, hatua kadha wa kadha za kitaasisi na kimaendeleo zilionekana.

Ninapomsikiliza JPM leo akisema kwamba analazimika kuchukua hatua ngumu na kali eti kwa sababu ‘nchi hii imeliwa sana’, huwa napata mawazo mchanganyiko juu ya uhalisia wa kile anachokisema.

Ingawa ni kweli kwamba kwa upande mmoja kuna ukweli katika hicho anachokisema, sehemu ya pili ya maelezo yake hayo anayoyarudia mara kadhaa yana ukakasi mwingi na pengine kutoa taswira isiyo sahihi.

Kauli za namna hiyo zina maana kubwa moja kwamba msingi uliojengwa na Mkapa kati ya mwaka 1995 na 2005, ulibomolewa na Serikali ya JK kwa kiwango cha leo JPM na Serikali yake kulazimika kuanza upya.

Pengine ni sahihi kuliacha hilo kwa muda na kurejea kwanza katika mstari na kujiuliza; Ni nini kingeikuta nchi hii iwapo tungepata rais wa aina ya JPM na si Mkapa mwaka 1995, ambaye angeingia madarakani na kukuta taifa likiwa lina jumla ya mashirika ya umma 330 tegemezi, ambayo yalikuwa yakiendeshwa kwa kupata ruzuku kutoka Wizara ya Fedha, uchumi ulioparaganyika, rushwa iliyokithiri na wafanyakazi ambao walishapoteza ari ya kazi kwa kiwango kikubwa?

Moja ya mambo bayana ambayo yangetokea, ni ukweli kwamba JPM wa mwaka 1995-2000 asingekuwa na jeuri aliyonayo leo ya kutumia fedha za ndani kununua ndege au kujenga reli ya kisasa (SGR).

Tutaliona hilo kwa marefu na mapana na pengine kutoa ushauri sahihi kwa Rais na wasaidizi wake iwapo tutashiriki kuchambua kwa namna ya kudadisi kile kilichotokea hadi mwaka 2005 zama za Mkapa na kisha kuanzia mwaka 2005 hadi 2015 ilipoanza safari ya JPM.

Pengine nitakuwa sahihi nikiandika ‘Msingi wa jeuri ya leo ni kazi kubwa iliyofanywa juzi na jana’.

Tutaendelea wiki ijayo…

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles