25.4 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TUCTA WAKERWA KUHISHWA NA SIASA

Na JANETH MUSHA-ARUSHA


SHIRIKISHO la Vyama Huru vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), limelaani vikali kauli ya Msemaji wa Serikali, Dk. Hassan Abbasi kulihusisha na siasa.

Limesema  halitaki malumbano na serikali na badala yake linataka kushirikiana katika kutatua changamoto za wafanyakazi nchini ikiwamo kulipwa malimbikizo ya wafanyakazi.

Hayo yalisemwa jana na Rais wa TUCTA,Tumaini Nyamhokya, alipozungumza na waandishi kuhusu kauli iliyotolewa na Dk.Abbas hivi karibuni.

Dk. Abbas aliwataka Watanzania kupuuza madai halali ya wafanyakazi yaliyowasilishwa kwa serikali katika kikao cha Kamati ya utendaji Oktoba 11 mwaka huu.

Nyamhokya alisema Shirikisho hilo halifanyi siasa na kwamba katiba za vyama vyote vya wafanyakazi nchini ikiwa ni pamoja na katiba ya TUCTA yenyewe hazifungamani na mlengo wowote wa vyama vya siasa nchini na kuwa wajibu wao ni kulinda ajira na maslahi ya wafanyakazi nchini.

“Msemaji huyo wa serikali anapaswa kufahamu kuwa katiba za vyama vyote vya wafanyakazi nchini ikiwa ni pamoja na ya TUCTA hazifungamani na mlengo wowote wa vyama vya siasa nchini kwa kuwa vinafanya kazi kwa kuzingatia miongozo mbalimbali nchini ikiwa ni pamoja na Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Tucta inalaani vikali kauli ya Msemaji wa Serikali kwa kutuhusisha na vyama vya siasa.

“Ifahamike kuwa vyama vya siasa vina lengo la msingi la kuundwa kwake ambalo ni kushika dola na vyama vya wafanyakazi vimelenga kulinda ajira na kuboresha maslahi bora ya wafanyakazi nchini,”alisema na kuongeza:

 

“Tumesikitishwa na kitendo cha msemaji huyo kutaka umma kupuuza madai halali ya wafanyakazi tuliyowasilisha na TUCTA tunaona kwamba msemaji huyo ama kwa makusudi na kutokuelewa taarifa yetu na hatuna uhakika kama anaelewa vilivyo majukumu ya msingi ya vyama vya wafanyakazi nchini,”

“Kutaka kupuuzwa madai yetu  ni kitendo kilichokosa busara na dhamira njema kwa taifa letu.

“Majibu ya Msemaji huyo kuwa sisi tunaokoteza hoja na hatuna takwimu na tunafanya siasa jambo hili limetutisha, ni wajibu wetu kusemea wafanyakazi, tukidharauliwa na kupuuzwa huko mbeleni madai yetu yataendelea kupuuzwa”.

Kwa mujibu wa kiongozi huyo wa TUCTA, watendaji wa serikali wanapaswa kutekeleza kwa vitendo ahadi za Rais Dk.John Magufuli, alizozitoa kwa wafanyakazi katika sherehe za Mei Mosi mwaka huu  kulinda hadhi na heshima ya kiongozi huyo na kuwa wataendelea kukumbushia madai ya wafanyakazi mpaka yatakapolipwa.

Nyamhokya alitaja baadhi ya madai hayo ya wafanyakazi kuwa kuwa ni pamoja na kupandishwa madaraja, nyongeza ya mishahara na madai mengine ya wafanyakazi ambayo wanadai kuanzia mwaka 2013 hadi 2016.

Alisema madeni ya mwaka 2016/2017 yamelipwa kidogo huku madeni ya nyuma yakiwa hayajalipwa.

“Tunaomba serikali iongeze kasi ya ulipaji wa madeni ya wafanyakazi, tutaendelea kupiga kelele kuhimiza madai hayo yalipwe na yasipolipwa tutaendelea kupiga kelele,”alisema Rais huyo.

Hivi karibuni Dk.Abbas alikanusha taarifa  zilizotolewa na TUCTA dhidi ya Rais Dk.Magufuli kuwa hatapandisha mishahara ya watumishi wa umma pamoja na kuongeza mishahara na kupandisha madaraja ambapo alilitaka Shikisho hilo kuacha kufanya siasa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles