27.2 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

TUACHE SIASA KWENYE ELIMU, TUTAMBUE HADHI YA WALIMU

HUSSEIN JUMA, SHINYANGA


PROF. Willy Komba, mwalimu wangu Chuo Kikuu cha Dodoma, aliwahi kusema, ‘Walimu wanashiriki kwenye uumbaji’. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, Mwalimu ndiye anayeumba taaluma zingine zote na akasisitiza kuwa, ‘Mungu huumba binadamu, Mwalimu anaumba profession ya binadamu’. Kwa maana nyepesi, Prof. Komba anaamini umuhimu wa Mwalimu kuwa ni mkubwa mno katika kutengeneza taaluma zingine na hakuna taaluma inayokamilika bila Mwalimu.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, akihutubia kwenye Chuo Cha Ualimu Morogoro Agosti  27, 1966, aliwahi kusema, ‘Shule zinatakiwa zizalishe raia wenye mwamko na wanaojitambua. Walimu wanao uwezo wa kutimilisha hili kwa namna ya tabia zao na wafundishavyo’. Mwalimu akaendelea kuona umuhimu wa walimu akisema, ‘…as a group, they have power which is second to none…’ akiwa na maana kwamba, walimu, kama kundi, wanao umuhimu mkubwa sana.

Ili tuweze kuwa na jamii ya watu huru nchini, kama Mwalimu Nyerere anavyosema, ni lazima kuwapo na watu wenye ‘mitazamo ya fikra watu ambao ndiyo huunda jamii hiyo. Mitazamo mizuri ya fikra hutengenezwa angali binadamu yu mdogo na hivyo mwenye dhamana ya kutengeneza mitazamo hii (Mwalimu), kwa kipindi hicho, ni mtu muhimu mno.

Mwalimu aingiapo darasani akiwa mnyonge, amechoka, kapauka, hana morali na wala hajivunii kuwa Mwalimu, basi mtoto atakuwa na ‘mtazamo’ kuwa, ualimu ni kazi ambayo inatakiwa kukwepwa kwa namna yoyote ile; kazi ambayo haifai. Sawia kabisa na maneno ya Prof. Komba kuwa, Mwalimu anaumba; anaumba kwa vitendo, maneno, tabia, maisha na namna ya ufundishaji wake.

Kwa muda mrefu, Tanzania inashindwa kuuona umuhimu huo. Utofauti wa mishahara ya walimu ukilinganisha na mishahara mingine, namna madai yao yanavyoshugulikiwa, heshima ya walimu na hata mazingira wanapofanyia kazi ni kielelezo tosha kusema kuwa, Taifa bado halijatambua umuhimu wa walimu kama vile anavyoutambua Prof. Komba na Mwalimu Nyerere.

Waraka wa Watumishi wa Serikali Namba moja wa mwaka 2013, kwa mfano, wenye kumbukumu namba CAC.205/228/01/C/14 wa Julai 2, 2013 uliosainiwa na Katibu Mkuu Utumishi, George Yambesi, kwa kiasi kikubwa, unaonesha ‘hadhi’ na ‘umuhimu’ wa walimu Tanzania kuwa ni mdogo sana ukilinganisha na kada zingine na ninashukuru kuwa, walimu pia walishawahi kulijadili hili kwenye baadhi ya mikoa ingawa hadi sasa majibu yaliyopo ni ya kisiasa sana.

Waraka ule unabainisha kiwango cha mishahara ambacho kinaonesha utofauti mkubwa sana na mshahara wa Mwalimu ni mdogo sana ukilinganisha na mishahara ya kada zingine. Kwa mfano, Mwalimu mwenye kiwango cha elimu cha Stashahada kwa mujibu wa waraka ule, analipwa Sh. 344,000 wakati mwenye kiwango kile kile cha elimu kwenye kada ya kilimo analipwaSh.milioni 1, 060,000 na kwenye kada ya afya analipwa Sh. 562, 000. Mwalimu mwenye kiwango cha elimu cha Stashada analipwa Sh. 432, 500, wakati mwenye kiwango kile kile kwenye kada ya kilimo analipwa Sh. milioni 1,252,000 na kwenye afya Sh. 821,000. Tofauti hii inaendelea kuwapo hata kwenye viwango vingine vya elimu; kada ya ualimu ikiwa na mshahara mdogo kwa kulinganisha na kada zingine.

Kikao cha walimu mkoani Mbeya cha Agosti 3, 2013, takribani mwezi mmoja baada ya waraka wa Watumishi wa Serikali, walikaa na kujadili tofauti ya mishahara ile, wakirejea Sheria ya Ujira, yaani ‘Right to just remuneration Act No. 15 of 1984, hasa ibara ya 23 (1) isemayo, ‘kila mtu, bila ya kuwapo ubaguzi wa aina yoyote, anayo haki ya kupata ujira unaolingana na kazi yake  na watu wote wanaofanya kazi kulingana na uwezo na kiasi na sifa za kazi wanazozifanya’

Walimu walikuwa na hoja nne nzito kabisa kwamba, Je (i) Uwezo wa walimu wa kufanya kazi haufanani na kada hizo? (ii) umuhimu wa kada ya ualimu ni mdogo tofauti na kada zingine? (iii) Sifa walizonazo walimu ni tofauti kabisa na kada hizo? (iv) Umuhimu wa walimu na elimu ni mdogo nchini?

Ukiangalila karibu hoja zote zipo katika kuangalia ‘hadhi’ na ‘umuhimu wa walimu’ nchini, ambao kwa ushahidi huo aghalabu umekuwa hautiliwi maanani, wakati walimu ndiyo ‘creators of other professions’; kwa nini walimu hawapewi hadhi yao nchini? Je, ni kweli Taifa halioni umuhimu wao?

Ufini ni nchi yenye mfumo bora wa elimu duniani kwa mujibu wa taarifa za OECD za mwaka 2012. Ubora wa elimu yao umetokana na vitu vitatu, kimojawapo ni ‘kuthamini walimu’. Pamoja na mambo mengine kwenye kuangalia thamani ya walimu nchi Ufini, mshahara wa mwalimu wa shule ya msingi (pamoja na kuwa mahitaji ya kiwango cha elimu kuwa kikubwa) kwa mwaka ni takribani  Dola za Marekani 37, 500 sawa na Sh. milioni 82) Hawaishii hapo tu, heshima kwa walimu ni ya juu mno ukilinganisha na kada zingine, na kila Mfini hutamani kuwa Mwalimu kuliko kada yoyote ile na nafasi za ualimu ni za ushindani mkubwa mno. Mwalimu nchini Ufini anapewa mamlaka yote kama Mwalimu bila kuingiliwa hovyo hovyo kwenye kazi zake. Kazi yake ni ‘uumbaji’ wa taaluma zingine kwa uhuru mkubwa kabisa na kwenye mazingira safi, wezeshi na rafiki.

Mfumo wa elimu nchini Uchina pia umetambua hadhi ya Mwalimu kitaifa na wao kupitia mfumo wao wa Tai Pei, kila tarehe Septemba 10 ya kila mwaka ni  siku ya Walimu nchini.

Wanachokifanya ni kuboresha hadhi ya Mwalimu kijamii, kiuchumi na kitaaluma. Wanahakikisha wanakuwa na takwimu sahihi za walimu wasio na makazi na kisha kuwajengea. Wanahakikisha Mwalimu anafanya kazi kwenye mazingira mazuri. Wanahakikisha Mwalimu anakuwa na uwanda mpana na huru wa kujiendeleza kitaaluma. Inasadikika pia Uchina ni kati ya nchi zinazolipa walimu vizuri na kuthamini umuhimu wao.

Ukiachilia mbali suala la mishahara kama nilivyotanabaisha awali kwa rejea ya waraka wa elimu wa 2013, bado pia thamani ya Mwalimu nchini ni ndogo sana ukilinganisha na kada zingine. Nitolee mfano, Shule ya Sekondari Mazinge, mkoani Shinyanga hadi sasa walimu hawana ofisi. Kinachofanyika, jengo la darasa na chumba kimoja cha maabara ndivyo vinatumika kama ofisi hadi sasa. Tuseme hilo ni tatizo dogo. Sakafu ya jengo hilo linalotumika kama ofisi halina sakafu ya maana, kiatu cha Mwalimu kinapigwa vumbi muda wote. Hali hiyo hiyo Mwalimu wa Mazinge anakutana nayo darasani, madarasa yote hayana sakafu, hivyo yanategemea umwagiliaji maji sakafu kana kwamba Mwalimu huyo anaingia bustanini. Na hii ni shule ambayo ipo katikati ya mji. Hakuna hata nyumba moja ya walimu, hakuna na wala msingi tu haupo. Vyoo vinavyotumiwa na walimu havina tofauti na vile wanavyotumia wanafunzi. Hii ni aibu kubwa sana kwa Taifa, aibu ya kushindwa kutambua thamani ya Mwalimu.

Wilaya ya Siha nako, toka walimu wasimamie mtihani mwaka 2015, hadi sasa hawajalipwa stahiki zao, yaani fedha zao za usimamizi na wala hawajui tatizo ni nini. Mwalimu mmoja wilayani humo ananidokeza, anadai zaidi ya Sh. milioni moja, toka mwaka huo hajalipwa na hajui atalipwa lini. Iko wapi heshima ya walimu nchini!

Kule Hai, tulisikia Mwalimu katupwa ‘Lock up’ kwa amri ya Mkuu wa Wilaya, kisa kashindwa kujibu maswali yake. Siku ya Wafanyakazi Duniani mwaka jana, walimu walipoandika mabango yao kudai haki zao za msingi, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam siku moja tu baadaye alinukuliwa akisema alitamani sana angekuwapo karibu, angewacharaza bakora.

Matokeo mabaya mkoani Dar es Salaam, Afisa Elimu, ambaye bila shaka ni Mwalimu, anaandikiwa barua na Mkuu wa Mkoa akihojiwa kwa nini matokeo ni mabaya. Tambo zote hizi, bado Taifa halijaona kabisa kuwa ni ipi ‘hadhi’ halisi ya Mwalimu kwenye jamii. Mwalimu amekuwa mtu wa kunyanyaswa kila sehemu. Kila siku Taifa linashuhudia askari wameboreshewa mazingira ya kufanyia kazi, wamepewa usafiri na juu ya yote, wana posho nje ya mshahara. Mwalimu hana chochote zaidi ya mshahara wake, labda aamue kufundisha masomo ya ziada, ambapo inabidi apunguze ufanisi wa kufundisha darasani ili avutie soko lake la masomo ya ziada.

Malalamiko ya walimu nchini yamekuwa ni malalamiko yasiyofaa na sana yamekuwa ni malalamiko yasiyo na maana na ndiyo maana yoyote yule anaweza kujitokeza na kujibu malalamiko hayo bila kujali yeye ni nani, ili mradi tu awe mwanasiasa na ana mamlaka; yote ni kumkandamiza tu Mwalimu.

Pamoja na kuwa usimamizi wa walimu kwa sasa hauna mipaka tengefu baina ya vyombo vitatu; Wizara ya Elimu, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) na Tume ya Utumishi wa Umma Idara ya Utumishi wa Ualimu, bado haitoshi kabisa madai ya walimu, wala maadili yao kusimamiwa na mtu yeyote anayejisikia kufanya hivyo. Bado haitoshi kabisa Mkuu wa Mkoa au Wilaya kutamani ‘kucharaza bakora’ walimu ama kuwaandikisha barua hovyo hovyo juu ya maadili yao, mienendo yao au hata kitu chochote kuwahusu.

Ushiriki duni wa walimu kwenye kuandaa Mitaala ya Elimu ni kielelezo kingine namna ambavyo Taifa kupitia mfumo wa elimu, halimthamini kabisa Mwalimu. Kwa mfano, ukisoma Sera ya Elimu ya mwaka 2014 ukurasa wa 27 kwenye utangulizi, wizara inakiri kabisa kuwa, mabadiliko ya Mtaala wa kutoka kwenye msingi wa maudhui na ufahamu (Content and comprehension based curriculum) kwenda kwenye mtaala wa ujuzi haukushirikisha, kati ya wengine, walimu na hivyo, walimu hawafundishi vile mitaala inawafanya wafundishe.

Maana yake ni kwamba, kuna mambo ambayo walimu wanayaona yanafaa kuwamo kwenye mitaala na hawakuyawasilisha kwenye uandaaji mitaala hiyo, hivyo hayamo kabisa kwenye mtaala elekezi. Hii ni hatari na ni mwendelezo wa kudharau walimu ambao ndiyo wadau wakubwa wa elimu kwani ndiyo wanoutekeleza mtaala, wanautathmini na kuupima.

Kwa maoni yangu, ipo haja kubwa sana kwa Taifa liangalie upya na kutambua ‘umuhimu’ na ‘hadhi’ ya walimu ili kulipatia Taifa wananchi wenye mitazamo mizuri ya fikra, kwa manufaa mapana ya nchi na wananchi, hasa kipindi hiki cha Elimu Bure. Kama anavyosoma daktari, mtaalamu wa kilimo, mwanasheria na kadhalika, mwalimu pia anakaa chuoni kupatiwa mafunzo ya ualimu, wala hajaokotwa mtaani.

Juu ya yote, Mwalimu anarudi shule kuendeleza taaluma hizo ambazo leo hii zinaonekana kuwa na thamani kuliko Mwalimu. Nikubaliane na Prof. Komba kuwa, ‘Mwalimu anashiriki kwenye uumbaji’ na Mwalimu Nyerere kuwa, walimu, kama kikundi, wanayo nguvu kubwa mno kwenye jamii. Walimu wanao uwezo wa kujenga ama kubomoa jamii kutokana na nafasi  waliyonayo.

Tukilalamika kuwa, tuna taifa la ‘Vilaza’, lazima turejee ni nani huyu anayezalisha Taifa la vilaza? Hadhi yake nchini ikoje? Anathaminiwaje? Kama anapewa stahiki zote bila utofauti na kada zingine, Je ni kweli anaendelea kuzalisha vilaza?

Kama Taifa, ni lazima lione kuwa, kuna sehemu limeshindwa kabisa kuwatendea haki walimu na sasa ni wakati wa kurekebisha kasoro hizo hasa Awamu hii ya Tano ili sasa tuwe na Taifa la watu wenye mitazamo ya fikra yenye tija.

Serikali iboreshe mshahara wa Mwalimu sawia na kazi na umuhimu wake. Iunde chombo kimoja cha kushughulikia madai yao na zaidi waachwe wenyewe waseme, siyo kusemewa na wanasiasa wanaotumia takwimu feki kama zile za Kiufunza teachers survey ambazo hazina uhalisia. Mwalimu aheshimike zaidi ya mwanasiasa.

Inatia kinyaa mno kuona Mkuu wa Wilaya au Mkoa anapata shauku ya kutia Mwalimu ndani kwa matakwa yake binafsi, ama kucharaza Mwalimu bakora kwa kudai stahiki zake na kama kuna sheria inayowapa mamlaka hayo, basi Serikali ione haja ya kuurejesha bungeni, kama muswaada, kwa ajili ya marekebisho.

Inasikitisha mno kuona Mwalimu anaandikiwa barua kujibu kwa nini matokeo ni mabaya wakati ana njaa, anadaiwa hela ya pango na kama haitoshi, anafanya kazi kwenye mazingira magumu, ofisi hazilingani kabisa na hadhi yake. Inatia uchungu mno Mwalimu anayetumia muda mwingi kuandaa cha kumfundisha mtoto anakaa kilomita kadhaa kutoka anakoishi hadi kituo cha kazi. Na kama haitoshi, Mwalimu anahamishwa, hapewi stahiki zake za uhamisho.

Taifa sasa lifikie ukomo wa kuwatumia walimu kama makarani wa Mitaala kuliko waandaaji wa Mitaala. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa na elimu itakayomuwezesha mwananchi kuhimili kwenye ushindani wa soko la ajira. Kupuuza hadhi na umuhimu wa walimu ni kupuuza elimu, hivyo kufanya mwanya wa kuwa na Taifa la watu mambumbumbu.

255 759 947 397

Barua pepe: [email protected]

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles