Na Mwandishi Wetu, Dodoma
KUTOKANA na hamasa kubwa ya kilimo cha Mkonge iliyofanywa na Serikali, imechochea kuongezeka kwa mashamba ya kulima Mkonge hasa kwa wakulima wadogo.
Hayo yameelezwa Jumatano Agosti 16,2023 na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Mkonge Tanzania (TSB), Saddy Kambona wakati akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa Taasisi hiyo na mwelekeo kwa mwaka 2023-2024.
Mkurugenzi huyo amesema Serikali imegawa mashamba kwa wakulima 983 wilayani Korogwe na wakulima wengine zaidi ya 3,000 wamegawiwa mashamba wilayani Kilosa na zoezi bado linaendelea.
Pia, imepelekea kushusha riba kwenye mabenki ya biashara kwa mikopo inayoelekezwa kwenye kilimo, kununua mitambo mipya ya kuchakata Mkonge na kufufua mitambo ya kuchakata Mkonge ya Mashamba ya Kibaranga wilayani Muheza, Tanga.
Pia na shamba la Serikali la TPL lililopo Kata ya Bwawani wilayani Arumeru, Arusha ambalo linasimamiwa na kuendeshwa na TSB.
Amesema katika mkonge hatua za kimageuzi zimefanyika ikiwemo kuongezeka kwa uzalishaji kutoka tani 36,379 kwa mwaka 2020 hadi kufikia tani 48,351.49 mwaka 2022.
Pia, kuongezeka kwa fedha za maendeleo kutoka Sh milioni 100 mwaka 2019/2020 hadi kufikia Sh bilioni 2, mwaka 2022/2023.
Vilevile, kuongezeka kwa fedha za makusanyo ya ndani kutoka Sh 0.00 mwaka 2019/2020 hadi Sh milioni 507 mwaka 2022/2023.
Pia, kuweza kukusanya na kusambaza miche 6,991,200 ya mbegu za Mkonge bure kwa wakulima wadogo katika Wilaya 16.
Amesema hadi mwaka 2020, TSB iliweza kusajili wakulima wadogo 6,887. Mwaka 2022, idadi ya wakulima wadogo walikuwa 8,972.
Hata hivyo, wakulima wadogo wa Mkonge ambao hawajafikiwa na kusajiliwa na TSB wanakadiriwa kufikia 22,000.