WASHINGTON, Marekani
DONALD Trump ameapishwa kuwa rais wa 45 wa Marekani. Alivalia suti nyeusi na kufunga tai nyekundu, huku Rais Mstaafu Barack Obama, akiwa amevalia suti nyeusi na tai ya rangi ya bluu. Waling’ara. Ilikuwa siku ya kupewa heshima zaidi kwa bilionea huyo wa biashara za majengo na nyinginezo.
Kabla ya kuapishwa Capitol Hall, Rais mteule, Donald Trump, alikwenda kuhudhuria ibada katika Kanisa la Mtakatifu John mjini Washington. Maelfu ya wananchi waliungana na kiongozi huyo, huku wengine wakiandamana kupinga urais wake kitendo ambacho kiliwafanya askari kutumia muda wa ziada kuwazuia.
Marais wastaafu walihudhuria sherehe hizo ikiwa ni ishara ya umoja wa kitaifa bila kujali itikadi za vyama vyao. Miongoni mwa waliokuwepo, George W. Bush, Bill Clinton, Jimmy Carter pamoja na waziri Dick Cheney na wengineo.
Katika hotuba yake, Trump alisema huu si wakati wa maneno bali vitendo na kwamba Marekani inatakiwa kufaidi matunda ya kazi zao na kufufua viwanda vilivyofilisiwa. Tafsiri iliyopo kwenye hotuba hiyo inaonyesha wazi kuwa dunia inakwenda katika mwelekeo mpya.
Katika tafsiri ya Kiswahili isiyo rasmi, Trump alianza kwa kusifu utamaduni wa kisiasa uliowekwa nchini mwao pamoja na kummwagia sifa Rais Obama. “Tutakabiliana na changamoto. Tutakabiliana na nyakati ngumu. Lakini tutafanikiwa malengo yetu. Kila baada ya miaka minne, tunakutana hapa, tunatekeleza wajibu na kukabidhiana madaraka kwa mujibu wa katiba na kwa amani, tunamshukuru Rais Obama na mkewe Michelle kwa juhudi zao ili kufanikisha tukio hili.”
Akizungumzia juu ya msimamo wake katika utawala wa miaka minne ya kwanza, Trump alisema: “Kimsingi suala si chama gani kinachoongoza Serikali kwa sasa, bila kujali Serikali yetu inaongozwa na watu. Januari 20, 2017 itakumbukwa kama siku ambayo wananchi walichukua madaraka ya kuongoza nchi yao tena. Wanaume na wanawake waliosahaulika katika nchi yetu, hawatasahaulika tena.
“Kwa miongo mingi tumevinufaisha viwanda vya nje kwa gharama za kuua viwanda vyetu. Tumetuma majeshi yetu kwenye nchi mbalimbali na kuyadhoofisha; tumetetea mipaka ya mataifa mengine wakati tumeshindwa kutetea kwetu. Tumetumia trilioni ya dola kwa masuala ya nje ya Marekani, wakati miundombinu yetu nchini imeharibiwa na kupoteza mvuto wake,
“Kuanzia siku ya leo na zijazo, mtazamo mpya wa Serikali ni kujali mambo yetu. Toka wakati huu, tutaanza na Marekani kwanza. Kila uamuzi utakaofanywa katika masuala ya biashara, kodi, uhamiaji, sera za nje, utakuwa kwa manufaa ya wafanyakazi na familia za wananchi wa Marekani.
“Tunapaswa kulinda mipaka yetu inayotumiwa na nchi nyingi kutengeneza bidhaa zetu, kuibia kampuni zetu na kupora ajira zetu. Kuyalinda hayo kutakuwa na manufaa na kuibua nguvu mpya,” alisema Trump.
Katika hotuba hiyo, Trump alidhihirisha uzalendo wa hali ya juu baada ya kutamka wazi kuwa kila taifa litapewa nafasi katika majadiliano na Marekani lakini kitakachopewa kipaumbele ni utaifa wa Marekani kwanza kuliko chochote.
Hata hivyo, kabla ya sherehe hizo mamia ya watu walibeba mabango tangu saa mbili asubuhi wakitaka kuelekea kwenye eneo la tukio la Capitol Hall. Miongoni mwa mabango hayo yalisema: “Make racist, Afraid Again”. Pia walibomoa majengo mbalimbali na kuwashambulia waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti na kupiga picha kwenye matukio ya kabla, wakati na baada ya kuapishwa.
Atoa amri ya kwanza akiwa Rais
Ikiwa ni saa chache tangu kuapishwa kuwa Rais wa Marekani, Trump ametia saini amri za Serikali mojawapo ikiwa ni agizo linalolenga kuifuta bima ya afya iliyoanzishwa na mtangulizi wake, Barack Obama maarufu kama Obamacare.
Agizo hilo lenye lengo la kuipunguzia Serikali mzigo wa kiuchumi, linaziamuru taasisi za kiserikali kukomesha hatua zitakazoendeleza bima hiyo inayofadhiliwa na Serikali. Badala yake linataka taasisi hizo kupunguza, kuchelewesha au kufutilia mbali gharama za matibabu ambazo zilishughulikiwa na bima hiyo.
Hatua ambayo itaweka gharama hiyo kwa Serikali za majimbo na watu binafsi. Bima hiyo huwawezesha mamilioni ya Wamarekani wasiojiweza kupata huduma ya afya kwa gharama nafuu. Kuiondoa kabisa bima hiyo kutahitaji muswada kupitishwa katika Bunge la Marekani.
Wasiwasi wa mataifa ya kigeni
Wakati Trump akijinasibu kama bingwa wa Wamarekani wafanyakazi, kituo cha sera za kodi ambacho ni kituo kinachotoa ushauri bila kujali chama, kinakadiria kwamba mapendekezo yake ya kodi hayataongeza deni la kiasi cha dola trilioni 7.2 la Serikali ya Marekani katika kipindi cha miaka 10 ya mwanzo, lakini mapendekezo hayo yanatarajiwa kuwasaidia tu Wamarekani matajiri.
Kuchaguliwa kwake kulipokelewa kwa wasiwasi na wengi duniani kote, kutokana na sera za kujitenga za mambo ya kigeni.
Katika mahojiano baada ya Trump kuapishwa, Makamu Kansela wa Ujerumani, Sigmar Gabriel, alisema: “Kile tulichokisikia leo ni matamshi mazito ya siasa za kizalendo.”
Rais wa Mexico, Enrique Pena Nieto, alimpongeza Trump kwa kuampishwa, lakini alitahadharisha kwamba utaifa, masilahi ya kitaifa na ulinzi wa Mexico ni masuala ya juu kabisa.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis, alimtaka Trump kuongozwa na mfumo wa maadili akisema ni lazima kuwaangalia masikini na waliotengwa.
Putin amsubiri Trump
Siku moja baada ya kuapishwa Trump, Rais wa Urusi, Vladimir Putin, yupo tayari kukutana na kiongozi huyo mpya wa Marekani.
Msemaji wa Serikali ya Urusi, Dmitry Peskov, amenukuliwa na shirika la habari la nchi hiyo, TASS akisema hayo siku moja tu baada ya kuapishwa kwa Trump.
Uhusiano kati ya Marekani na Urusi haujawa mzuri katika miaka ya hivi karibuni, huku Marekani chini ya utawala wa rais aliyemaliza hatamu yake juzi, Barack Obama, ikiilaumu Urusi kwa kuingilia uchaguzi wake wa Novemba mwaka jana.