Na Damian Masyenene, Mwanza
MAMLAKA ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) imewatoa wasiwasi wananchi kwa kuelezea kuwa dawa zote za njia za uzazi za kisasa zinazotolewa katika vituo, zahanati na hospitali zimesajiliwa na ni salama kwa matumizi hivyo hazina madhara kama ambavyo baadhi ya watu wamekuwa wakipotosha na kuzua hofu kwa wananchi.
Hilo limeelezwa na Meneja wa Mawasiliano na Elimu kwa Umma wa Mamlaka hiyo, Gaudensia Simwanza katika mazungumzo yake Septemba 26, 2022 na mwandishi wa makala hii Jijini Mwanza huku akitoa tahadhari kwa wananchi kutotumia kiholela baadhi ya dawa ambazo hazijasajiliwa zikiwamo dawa za dharura za kupanga uzazi ambazo zimekuwa na madhara.
“Dawa za uzazi wa mpango ambazo zinatolewa katika hospitali zetu ni salama na zimesajiliwa na mamlaka yetu baada ya kutathminiwa na kuthibitisha ubora wake. Lakini watu wamekuwa wakitumia kwa usiri dawa za dharura (emergency) ambazo hazijasajiliwa wala kuruhusiwa kutumika na hizi ndizo zimekuwa zikiwaletea madhara mbalimbali,” alisema Gaudensia.
Akizungumzia umuhimu wa TMDA kulinda afya ya jamii, Mbunge wa jimbo la Mtambwe, Khalifa Mohamed Issa alisema Mamlaka hiyo ina dhima kubwa kwenye jamii ikiwa imebeba mustakabali wa taifa hivyo watumishi wake wasikubali kurubunika na kuliangamiza taifa kwa kuruhusu dawa zisizokidhi vigezo huku wakitakiwa kuwasaidia wananchi kutoa elimu na kuwaepusha na kadhaa ya kutembea na mafurushi ya dawa.
“TMDA wasilegee kwenye uhakiki na kutoruhusu bidhaa feki kuingia kwenye soko na kuharibu afya ya jamii kwakuwa taasisi hii ni msingi kwenye afya ya Watanzania,” alisema.
Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo ya Bunge, Aloyce Kamamba alitoa wito kwa TMDA kutoa elimu ya kutoa kwa jamii juu ya matumizi sahihi ya dawa hususan kwa maeneo ya pembezoni na hatua za kuchukua wanapobaini kuna utofauti kwenye dawa wanazopewa.
“Taasisi hii imeshikilia uhai wa Watanzania mkitaetereka kiuwajibikaji mtawaumiza wananchi. Jamii yetu haina elimu ya kutosha juu ya matumizi sahihi ya dawa tuombe mfike maeneo ya pembeni yasiyofikika kwa urahisi ili tusaidie matumizi bora na sahihi ya dawa,” alisema Kamamba ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Buyugu, Kigoma.
Kwa mujibu wa taarifa ya bajeti ya wizara ya afya mwaka wa fedha 2022/2023 iliyosomwa bungeni Mei mwaka huu na Waziri Ummy Mwalimu, katika katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 2022 vidonge vya uzazi wa mpango dozi 1,755,349 sawa na asilimia 82 ya lengo, sindano za uzazi wa mpango aina ya depo-provera dozi 2,125,625 sawa na asilimia 93 ya lengo na vipandikizi 206,000 20 sawa na asilimia 78 ya lengo vilisambazwa katika halmshauri zote nchini.
Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo akizungumza na kamati ya bunge ya huduma na maendeleo ya jamii iliyotembelea ofisi ya Kanda ya Ziwa Mashariki iliyopo Buzuruga, Mwanza alisema Mamlaka hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwamo uwepo wa njia nyingi za panya zinazotumika na wafanyabiashara wasio waaminifu kuingiza bidhaa zinazodhibitiwa, upungufu wa watumishi na uwepo wa majengo yanayofanya biashara ya rejareja ambayo hayajasajiliwa na bodi ya wafamasia.
Kwa mujibu wa taarifa ya utendaji kazi ya TMDA kwa mwaka 2020/2021 iliyotolewa Septemba, 2021, Katika kuimarisha udhibiti wa ubora usalama na ufanisi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi, jumla ya maombi 1,302 ya usajili wa dawa za binadamu yalipokelewa na 1,214 (94%) kutathminiwa ambapo 1,111 (85%) yaliidhinishwa baada ya kukidhi vigezo.