23.6 C
Dar es Salaam
Friday, June 21, 2024

Contact us: [email protected]

THRDC yahamasisha majukwaa ya watoto watetezi shuleni

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) umeanza kuwajengea uwezo watoto waweze kupata ujuzi wa kutetea haki zao kwa sababu ndiyo njia pekee ya kujilinda.

Akizungumza Juni 14,2024 Mratibu Taifa wa THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema watoto wengi hawafundishwi haki za binadamu na hawajui haki zao hali inayochangia kwa kufanyiwa ukatili hasa ubakaji na ulawiti.

Olengurumwa alikuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Alpha yakiongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Elimu kwa kila mtoto wa Afrika muda ni sasa’.

Mratibu Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania THRDC, Onesmo Olengurumwa, akizungumza wakati wa maadhimisho ya Siku ya Mtoto wa Afrika yaliyofanyika katika Shule ya Sekondari Alpha, Dar es Salaam.

“Dhana ya haki za binadamu kwenye shule haijaeleweka vizuri lakini kuna ukiukwaji wa haki za binadamu, mtoto anapokuwa amefundishwa kujitetea ni rahisi sana kutetea haki zake, tunatamani shuleni tuwe na watetezi wa haki za binadamu. Katika ngazi ya kimataifa Umoja wa Mataifa wanatambua nafasi ya watoto katika utetezi wa haki za binadamu,” amesema Olengurumwa.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Haki za Watoto Tanzania (TCRF), Dk. Sylivia Ruambo, amesema jukumu la kulinda haki za binadamu ni la watu wote kwani bila haki za watoto kuzingatiwa hakutakuwa na kizazi bora.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi ya Bright Home, Bernadino Richard, amesema tayari wameanzisha klabu ya haki za binadamu ambapo watoto wamekuwa wakikutana kila siku ya Ijumaa na kujadiliana masuala mbalimbali yahusuyo haki za binadamu.

“Ni vizuri watoto wafahamu haki za binadamu ili wakiwa wakubwa wawe watu wenye manufaa kwenye jamii,” amesema Mwalimu Richard.

Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo Eunice Ishenda ambaye ni mwanafunzi wa darasa la sita katika Shule ya Msingi Jerusalem, amesisitiza kuwepo kwa dhamira ya pamoja kuhakikisha watoto wote wanapata fursa sawa ya elimu kwani ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu.

Amesema bado kuna watoto wengi ambao hawapati nafasi ya kwenda shule kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo umaskini, umbali mrefu, vifaa vya kujifunzia na kushauri uwepo uwekezaji katika miundombinu ya elimu kuhakikisha shule zina mazingira bora na walimu wenye ujuzi.

“Tupatiwe elimu bora inayotupa maarifa na ujuzi kukabiliana na changamoto za maisha, watoto walioelimika vyema wana uwezo wa kuleta uvumbuzi na kupambana na changamoto za umaskini. Ni wajibu wa kila mtu kuwalinda watoto na kulinda haki zao na kuhakikisha sera na mikakati ya elimu inatekelezwa ipasavyo…elimu wanayotupa ilingane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira,” amesema Ishenda.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles