Na Prisca Libaga -Arusha.
MAMLAKA ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) imezifutia usajili dawa mbalimbali za kutibu magonjwa ya binadamu.
Vilevile imeziondoa kwenye soko na kusimamisha matumizi yake kutokana na kuwa na madhara makubwa kwa wagonjwa.
Hayo yalielezwa Arusha jana na Mkurugenzi Mkuu wa TFDA, Hiiti Sillo, alipofungua mafunzo ya wakufunzi wa kufuatilia kufundisha na kuhamasisha masuala ya udhibiti wa madhara yanayotokana na matumizi ya dawa zisizosalama kwa watendaji wa afya kutoka wilaya zote za mkoa wa Arusha.
Alisema katika kudhibiti matumizi ya dawa zisizofaa, TFDA imeondoa dawa ya sindano ya Chloramphenical kwenye soko baada ya Shirika la Afya Duniani (WHO) kubaini ina madhara kwa watumiaji.
Mamlaka pia imefuta usajili wa dawa nyingine ambazo ni Ketoconazole (vidonge) Phenylpropanalamine, Dextropropoxyphene, Nimesulide, stavudine 40, Gatifloxacin, Rofecoxib na Celecoxib baada ya kuthibitika zina madhara kwa watumiaji.
Alisema matumizi ya dawa kama Kanamycin, Amikacin na Levofloxacin yamebadilishwa ziweze kutumika kutibu ugonjwa wa kifua kikuu pekee.
Mkurugenzi huyo wa TFDA alisema mafunzo hayo yanashirikisha wakufunzi 60 nchini kote na yanafanyika katika mikoa mbalimbali yakiwashirikisha madaktari, wauguzi na wafamasia walioko kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Alisema lengo la mafunzo hayo ni kuongeza idadi ya wakufunzi wa masuala ya usalama wa dawa kutoka 73 hadi 133.
Alisema katika kipindi cha miaka mitatu 2014/ 15 hadi 2017/18, TFDA imehamasisha watendaji wa afya wapatao 2000 nchini kote na sasa uhamasishaji unaendelea katika Mkoa wa Katavi.