Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Shirika la Viwango nchini (TBS), zimetoa ufafanuzi kuhusu vidonge vinavyodaiwa kuwapo kwenye chupa ya chai ambavyo vinadaiwa kuwa na madhara kwamba si sumu na havina madhara kama inavyodaiwa.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na taasisi hizo, vidonge hivyo si sumu bali ni vitu vilivyotengenezwa kwa kutumia karatasi ambavyo ni teknolojia ya kisasa inayotumika kutenganisha kuta mbili za chupa ili kutunza joto la kimiminika kilichowekwa kwenye chupa husika.
“Hivi karibuni kumekuwepo na video inayosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu vidonge vilivyomo kwenye baadhi ya chupa za chai kuwa vidonge vyenye dawa yenye madhara kwa watumiaji na video nyingine ya lugha ya kiarabu ikieleza vidonge hivyo vina madini ya asbestos.
“Tunawahakikishia wananchi kuwa bidhaa hizo ni salama kwa matumizi ya kutunza joto la kimiminika kama vile chai,” imesema taarifa hiyo.
Pamoja na mambo mengine, taasisi hizo zimeonya wananchi kuepuka kusambaza taarifa kupitia mitandao ya kijamii zisizohakikiwa na taasisi hizo ili kuondoa taharuki zisizo za lazima.