Na FERDNANDA MBAMILA-
DAR ES SALAAM
WAKALA wa Majengo nchini (TBA), wamedhamiria kutoa kipaumbele cha kuwauzia nyumba watumishi wa umma waliokaribia kustaafu kwa lengo la kuwapunguzia gharama ya maisha pindi watakapostaafu kazi.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea mradi wa nyumba za wananchi Bunju, Mtendaji Mkuu wa wakala hao, Elius Mwakalinga, alisema dhamira kuu ya mradi huo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini ili waweze kunufaika na nyumba za gharama nafuu.
Alisema licha ya kutoa kipaumbele kwa wananchi wa kipato cha chini katika kiwango cha uuzaji wa nyumba, pia wakala hao wanasimamia na kuiendeleza miradi mbalimbali, ikiwamo ya Serikali na taasisi zake.
“Mwakalinga aliongeza kuwa, kutokana na ongezeko la miradi mingi, hadi sasa mamlaka hiyo imeongeza wataalamu zaidi ya 200 ambao wana uwezo mkubwa wa kujenga na kusimamia miradi ya majengo mbalimbali,” alisema Mwakalinga.
Alisema katika mradi wa Bunju ambao unajenga nyumba zaidi ya 1,000, kutakuwa na huduma zote za kijamii.
“Ndani ya miaka mitano TBA huwa inajenga nyumba zipatazo 10,000, ambapo kwa kila mwaka hujenga nyumba 2000 kwa Tanzania nzima,” alisema Mwakalinga.
Naye mjumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Japheth Asunga, aliipongeza Serikali na Wakala wa Majengo nchini, TBA, kwa kubuni mradi wa aina hiyo ambao umekuwa ukiwaletea manufaa wananchi wa kipato cha chini.
Alisema kutokana na jitihada za ujenzi wa majengo za TBA, Serikali ina jukumu la kusogeza huduma za kijamii kwa haraka ili wananchi watakaokuwa na uwezo wa kuishi maeneo hayo waweze kunufaika.