30.3 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

TAWLA yawawezasha Wanawake 373 waishio Magu kumiliki ardhi

Na Clara Matimo, Mwanza

Katika  jitihada za kuhakikisha mwanamke anamiliki ardhi kama nyenzo ya maendeleo na kushiriki kwenye uchumi wa nchi, zaidi ya wanawake 300 wilayani Magu Mkoa wa Mwanza wamekabidhiwa hati miliki za ardhi za kimila.

Hati hizo zimekabidhiwa leo kwa wanawake 300 wa vijiji vya Kitongosima na Shinembo na Mkuu wa wilaya hiyo, Salumu  Kalli, kati ya hati 373 zilizolipiwa  na Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania(TAWLA) zikigharimu Sh milioni 13,055,000.

Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salumu Kalli(kulia), akimkabidhi hati miliki ya kimila leo mmoja wa wanufaika wa  mradi wa kuwawezesha wanawake kumiliki  ardhi uliokuwa ukitekelezwa na TAWLA.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika katika Kijiji cha Kitongosima, Mkurugenzi  Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile,amesema  waliamua kuwalipia gaharama za upimaji  wanawake hao ambao wana ardhi  lakini hawakuwa na uwezo wa kulipia kwa sababu chama chake kinaamini  moja ya nyenzo ya ulinzi wa haki ya mwanamke kwenye ardhi ni kuwa na nyaraka ambayo inaonyesha umiliki.

“Kama tunavyofahamu hadi hati ikamilike ni hatua na sisi mwaka 2018 wakati tunatekeleza mradi wa kuwawezesha wanawake kumiliki  ardhi  kwa kuwa tunashirikiana na viongozi wa serikali kuanzia ngazi ya mtaa tukakuta kuna wanawake hawa wenye mashamba  ambao maeneo yao yametambuliwa na wamepimiwa lakini changamoto ikawa ni ukosefu wa fedha za kulipia ili wapewe hati, kila mmoja tumemlipia kiasi cha sh 35,000 leo tunafuraha maana wanakabidhiwa hati zao.

“Mradi huo tumeutekeleza kwa awamu mbili, awamu ya kwanza ilianza mwaka 2017/18 ya pili 2018/19 lengo lilikuwa ni kuwawezesha wanawake kumiliki ardhi na kufikia haki mbalimbali za umiliki mali maana tunafahamu ardhi ni mali,”alisema Mwambipile.

Naye Mratibu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini  kutoka TAWLA, Barnabas Kaniki, alisema jamii nyingi zimejengeka kwenye misingi ya mifumo dume ambayo kwa kiasi kikubwa mwanamke hamiliki ardhi hivyo waliamua kutekeleza mradi huo ili kutoa fursa kwa wanawake kumiliki rasilimali hiyo muhimu kwa ustawi wa maisha yao.

“Ardhi ni nyenzo muhimu sana ya maendeleo hasa kwa wanawake wanaoishi vijijini kwa hiyo kutokuwapa fursa ya kumiliki ardhi  ni kama umekatisha maisha yao hiyo ndiyo sababu  iliyotusukuma kutekeleza mradi huu kwenye maeneo haya ya pembezoni,”alisema.

Kaniki amebainisha kwamba kupitia mradi huo wametekeleza shughuli mbalimbali ikiwemo kuwajengea uwezo wasimamizi wa sheria kwenye  mabaraza ya kata na vijiji ambayo yanahusika na usuluhishi wa migogoro ya ardhi.

 “Lengo ni kutengeneza mazingira wezeshi  maana tunaamini kwamba  wajumbe wanaokaa kwenye vyombo hivyo vya maamuzi wakiwa na uelewa wa sheria za nchi na haki za binadamu wataweza kufanya maamuzi sahihi ambayo yana malengo ya kulinda haki za wanawake kwenye masuala ya ardhi.

Pia tumekuwa na mijadala mbalimbali kwenye jamii lengo ni kuongeza uelewa ili jamii ifahamu kwamba mwanamke kama ambavyo ilivyo kwa mwanaume anahaki ya kumiliki ardhi,”alisema Kaniki.

Akikabidhi hati hizo, Mkuu wa Wilaya ya Magu, Salumu Kalli, alizitaka taasisi za fedha kuzitambua kwa kuwapa mikopo wanawake hao endapo watahitaji maana ni rasmi na zinatambulika na serikali ili nao waweze kujikwamua kiuchumi.

Kalli amefafanua kwamba wanawake 73 ambao hawajakabidhiwa hati zao leo wasiwe na mashaka  watakabidhiwa muda wowote baada ya taratibu za kuziandaa kukamilika.

Nao baadhi ya wanufaika wa mradi huo wakizungumza na MTANZANIA Digital baada ya kukabidhiwa hati zao akiwemo Nyamarwa Malugu, Magreth Magashi na Paschazia Lukona, waliishukuru TAWLA na Serikali kwa kuwawezesha kumiliki rasilimali hiyo muhimu maana  hati hizo zinawapa maamuzi juu ya matumizi ya ardhi zao.

“Ninaishukuru sana TAWLA kwa kunilipia gharama  za kupata hati hii pia serikali  kwa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi, upimaji na utoaji wa hati miliki za kimila kwa sisi wananchi tunaoishi na kumiliki ardhi vijijini,”amesema  Magreth huku akionyesha hati yake kwa furaha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles