NA MWANDISHI WETU
WAOGELEAJI wa Tanzania wameendelea kung’ara katika mashindano ya Cana ya Kanda ya Tatu ya Afrika, baada ya kuendelea kukusanya medali mbalimbali kwa siku mbili mfululizo.
Kutokana na kutawala mashindano hayo, matumaini ya timu hiyo ya Taifa kulitetea kombe hilo yameongezeka na wanatarajia kuweka historia ya pili kwa kutwaa ubingwa wa jumla wa mashindano hayo.
Siku ya kwanza, Tanzania ilitwaa medali zaidi ya 21, huku ikishinda medali tisa za dhahabu, tano za shaba na saba za fedha katika mashindano hayo yanayoshirikisha jumla ya nchi sita ambazo ni Kenya, Uganda, Zambia, Afrika Kusini, Sudan na wenyeji Tanzania.
Mwogeleaji wa kwanza wa Tanzania kutwaa medali ya dhahabu ni Natalie Sanford ambaye alishinda mita 800 kwa staili ya freestyle kwa waogeleaji walio chini ya miaka 14 na baadaye mwogeleaji nyota wa Tanzania wa kike, Sonia Tumiotto, akishinda kwa waogeleaji wa kike wenye umri zaidi ya miaka 15.
Waogeleaji wengine waliotamba na kutwaa medali za dhahabu ni Elia Imhoff, Natalie, Emma Imhoff, Tara Behnsen, Marin De Villard na kwenye ‘relay’ kupitia kwa Sonia Tumitto, Collins Saliboko, Hilal Hilal na Emma Imhoff.
Kocha wa timu hiyo, Michael Livingstone, alisema wana matumaini makubwa ya kutetea ubingwa huo pamoja na upinzani mkali kutoka kwa nchi shiriki hasa Zambia.