Nyemo Malecela-Bukoba
WATOTO 301 wenye umri chini ya siku nane na mama 22 wamepoteza maisha katika kipindi cha Januari hadi Mei mwaka huu mkoani Kagera.
Takwimu hizo zimetolewa na Mratibu wa Huduma za Afya za Mama na Mtoto mkoani Kagera, Neema Kyamba alipokuwa akizungumza na MTANZANIA katika mahojiano maalumu mjini hapa.
Alisema takwimu hizo zinaonekana kuwa kubwa zaidi katika Manispaa ya Bukoba kwani katika kipindi hicho cha Januari hadi Mei mwaka huu watoto 39 wenye umri chini ya siku nane na mama watatu wamepoteza maisha.
Amezitaja sababu za kutokea kwa vifo hivyo kuwa ni kupoteza damu nyingi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, upungufu mkubwa wa damu kwa mjamzito.
Sababu nyingine ni kifafa cha mimba, maambukizi mbalimbali wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua kama vile malaria ambayo pia usababisha upungufu wa damu, lishe duni na minyoo.
Neema alisema kuwa vifo hivyo havitabiriki kwani ni hali inayotokea ghafla ambapo muhudumu anaweza kushindwa kugundua kama mama atapoteza maisha.
Kwa upande wa watoto, idadi hiyo pia inajumuisha waliozaliwa wafu.
Akizungumzia sababu ya vifo hivyo vya watoto, Neema alisema; “chochote kibaya kinachomtokea mama mjamzito kinaathiri uhai wa mtoto.”
Neema alisema kwa Januari hadi Mei mwaka huu asilimia 79 ya wajawazito mkoani Kagera wamejifungua katika vituo vya afya wakati asilimia zilizobakia walijifungulia njiani na nyumbani.
“Katika asilimia 21 za wanawake waliojifungulia nyumbani na njiani, kulitokea vifo vya mama watatu ambao walijifungulia nyumbani.
“Kwa mwaka 2016 vimetokea vifo 61, mwaka 2017 vimetokea vifo 73, mwaka 2018 vimetokea vifo 65 kwa akina mama wakati kwa watoto mwaka 2016 vimetokea vifo 1,043, mwaka 2017 vimetokea vifo 1,007 na mwaka 2018 vimetokea vifo 979,” alisema.
Neema amewataka wajawazito kuhudhuria kliniki angalau mara nne katika kipindi cha ujauzito.
“Katika mahudhurio angalu manne mama huyu atasaidia wahudumu wa afya kubaini vidokezo hatarishi wakati wa kujifungua, lakini pia wataweza kumpa ushauri wa namna ya kuchukua tahadhari katika kipindi cha ujauzito,” alisema Neema.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kagera, Marco Mbata, alisema kuwa Manispaa ya Bukoba inaonekana kuwa na idadi kubwa ya vifo vya mama na watoto kutokana na uwepo wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa hasa kwa watoto wachanga.
“Ikumbukwe mama wanaoletwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa kwa matatizo ya ujauzito, pia watoto wanaokuwa tumboni mwao wanakuwa kwenye hatari ya kuchoka au kushindwa kupumua, hivyo matokeo yanaweza kusababisha kumwokoa mtoto au kushindwa kumwokoa.
“Pia watoto wanaoletwa katika hali isiyo nzuri kutokana na kuchelewa kwenye jamii au vituo vingine wakati huo manispaa hakuna kituo cha watoto wachanga, kwani kituo cha afya kinachotakiwa kuwahudumia watoto wachanga lazima kiwe kinatoa huduma ya upasuaji,” alifafanua Mbata.
Aliongeza kuwa manispaa inajenga kituo cha afya cha Zamzam ili kupunguza mzigo kwa Hospitali ya Rufaa kwani kitatoa huduma ya upasuaji kwa wajawazito pamoja na watoto wachanga.