Na Ramadhan Hassan, Dodoma
NAIBU Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Deogratius Ndejembi ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kufuatilia na kuwa wakali katika fedha Sh Trilioni 1.3 zilizotolewa na Rais Samia Suluhu Hassan katika miradi mbalimbali.
Hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan wakati akizindua Mpango wa Serikali kuinua uchumi kwa kutumia mkopo wa fedha wa Sh Trilioni 1.3 uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa(IMF) alitoa onyo kwa watendaji na kuelekeza kuondoa urasimu katika usimamizi wa fedha za umma.
Akizungumza jana jijini Dodoma wakati akifunga mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi wa Takukuru ambao pia ulihusisha Makamanda wa Takukuru Mikoa yote nchini, Naibu Waziri huyo amesema kuna viashiria vya rushwa katika fedha hizo
Ndejembi amesema kuna maeneo tofali linafuatwa umbali wa kilomita 150 na bei ikiwa ni ya juu sana Sh 1,700 ambapo amedai hivyo ni viashiria vya rushwa nakwamba viongozi hao wanatakiwa kulisimamia jambo hilo.
Aidha, Naibu waziri huyo ameitaka TAKUKURU kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya rushwa ikiwa ni pamoja na kuwa na mipango ya katika kuzuia zaidi ili kuleta faida.
“Tusimame imara tuwadhibiti watumishi wanaofanya kazi kwa mazoea simamieni rushwa na mmomonyoko wa maadili huku mkizingatia utoaji wa haki,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi Salumu Rashid Hamduni, amesema kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla ya Sh billioni 29.3 ziliokolewa kati ya hizo Sh billion 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslim na utaifishaji mali na kiasi cha Sh bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.
Ameeleza miradi ya kimaendeleo 1,188 yenye thamani ya Sh billion 714.17 katika sekta ya afya, maji, elimu ziliweza kufatiliwa na kubaini makosa ambayo wameyachukulia hatua.
“Tumeelimisha katika ngazi ya Makao Makuu pamoja na wakuu wa TAKUKURU, kuzuia vitendo vya rushwa kuelimisha, kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watuhumiwa Mahakami kwa kushirikiana na ofisi ya Taifa ya mashtaka ambapo majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa na majalada 339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakani ambapo kesi mpya zilipatikana 542 na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345,”amesema Hamduni.
Amesema wao wakiwa na dhamana ya kupinga masuala ya rushwa nchini wataendeleza juhudi kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kuzuia mianya ya rushwa.
“Tunatambua wapo wananchi ambao hawajafikiwa,tunaendeleza jitihada za kuwafikia wananchi na hasa waliopo vijijini n kuendelea kutoa kipaumbele zaidi katika kuzuia vitendo vya Rushwa ikiwemo kuwaelimisha wananchi ili wafahamu haki zao katika upatikanaji wa huduma, madhara ya rushwa na jinsi ya kutoa taarifa za rushwa,”amefafanua Hamduni.