Na MOHAMED KASSARA -DAR ES SALAAM
KIKOSI cha timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’, leo kitakuwa na kibarua kizito cha kusaka ushindi dhidi ya Benin katika mchezo wa kimataifa wa kalenda ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa).
Stars itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 na Malawi katika mchezo kama huo uliochezwa Oktoba 7 kwenye Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Matokeo ya mchezo huo yaliifanya Stars kushuka kwa nafasi tano katika viwango vya ubora vilivyotolewa na Fifa Oktoba, ikitoka nafasi ya 120 hadi 125.
Mchezo huo utakuwa wa kwanza wa kirafiki kwa Stars kucheza ugenini, tangu kocha Salum Mayanga alipokabidhiwa jukumu la kuinoa timu hiyo Januari 2, mwaka huu, akirithi mikoba ya mtangulizi wake, Boniface Mkwasa.
Mayanga ameiongoza Stars kucheza michezo minne ya kirafiki nyumbani bila kupoteza, dhidi ya timu za Botswana (mara mbili), Burundi na Malawi, akishinda mitatu na kutoka sare moja.
Kocha huyo pia ameweka rekodi ya kuiongoza Stars kucheza jumla ya michezo 13 tangu achukue jukumu hilo, akishinda mitano, sare sita, huku akipoteza mmoja dhidi ya Zambia.
Stars ilisafiri usiku wa kuamkia Alhamisi kwenda Benin na kikosi cha wachezaji 21.
Kuelekea mchezo huo, Mayanga alifanya mabadiliko madogo ndani ya kikosi chake, akiwaacha beki Erasto Nyoni na kiungo Mzamiru Yassin ambao walilimwa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Malawi na kuwajumuisha na Jonas Mkude na Mudathir Yahya.
Katika mchezo huo, Stars itamkosa nahodha wake, Mbwana Samatta ambaye ameshindwa kujiunga na kikosi hicho kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya goti aliyoyapata wakati akitumikia klabu yake ya KRC Genk katika mchezo wa Ligi Kuu ya Ubelgiji.
Kukosekana kwa Samatta ambaye ndiye kiongozi wa safu ya ushambuliaji, kuna maana jukumu hilo sasa litaongozwa na Simon Msuva anayecheza soka la kulipwa katika klabu ya Diffa El Jadid inayoshiriki Ligi Kuu nchini Morocco.
Kwa upande wa Benin, itaingia katika mchezo huo ikiwa na kumbukumbu ya kulazimisha bao 1-1 dhidi ya Congo Brazzaville katika mchezo wao uliopita.
Leo Benin itashuka dimbani ikihitaji ushindi ili kulipa kisasi cha kupokea kipigo cha mabao 4-1 kutoka kwa Stars  katika mchezo wa kirafiki uliochezwa Oktoba 12, 2014 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Mabao ya Stars siku hiyo yalifungwa na Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyekuwa nahodha, huku mengine yakiwekwa kambani na Amri Kiemba, Thomas Ulimwengu na Juma Luizio, bao la kufutia machozi la Benin likifungwa na Suanon Fadel.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mayanga alisema anaamini wachezaji waliopo kwenye kikosi hicho watajituma na kushinda mchezo huo bila ya uwepo wa Samatta.
Mayanga alisema wamepanga kucheza kwa nguvu ili kupata ushindi ambao ndiyo kiu ya Watanzania, lakini pia kumfariji Samatta ambaye ripoti ya  daktari wa Genk inadai atakuwa nje ya uwanja kwa wiki sita.
“Lazima nikiri kuwa Samatta ni mchezaji muhimu kwenye kikosi changu na kukosekana kwake kuna vitu tutavikosa, lakini nina matumaini ya kupata ushindi kupitia wachezaji waliopo,” alisema Mayanga.