Anna Potinus
Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC), inatarajia kushiriki kwenye maonesho ya 43 ya biashara ya kimataifa yatakayoanza Juni 23 hadi Julai 13 katika uwanja wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es salaam.
Mkuu wa kitengo cha mawasiliano TAEC, Peter Ngamilo, amesema kupitia maenesho hayo wataweza kuonesha shuguli mbalimbali zinazofanyika katika tume ikiwemo utoaji wa elimu kwa wananchi na wadau mbalimbali juu ya udhibiti na matumizi salama ya mionzi.
“Elimu kwa wananchi juu ya matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia kwenye sekta ya afya, kilimo, viwanda, mifugo, maji, lishe pamoja na ujenzi inatolewa,” amesema Ngamilo.
Aidha amesema kuwa wanafunzi na wananchi wote wanakaribishwa kwenye banda la TAEC kujipatia elimu bure kupitia maelezo, video fupi, vipeperushi na majarida ili waweze kujiongezea ujuzi juu ya majukumu yanayotekelezwa kisheria na TAEC katika nyanja za udhibiti wa mionzi na uhamasishaji wa matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia.