25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

TAEC kupima maji ya visima kubaini viasili vya mionzi

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Tume ya Nguvu za Atomu Tanzania (TAEC) imeanza kupima maji ya visima kuhakikisha wananchi wanaendelea kubaki salama dhidi ya madhara ya mionzi.

Tume hiyo ina jukumu la kudhibiti na kusimamia matumizi salama ya mionzi ili kulinda mazingira, wananchi, wagonjwa na wafanyakazi, kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya mionzi katika sekta za afya, kilimo, mifugo, viwanda, nishati, migodi, ujenzi pamoja na kufanya tafiti na kuishauri serikali juu ya mikataba mbalimbali inayohusiana na nyuklia.

Akizungumza Julai 5,2024 kwenye Maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa maarufu Sabasaba, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano TAEC, Peter Ngamilo, amesema zoezi hilo lililoanza Aprili mwaka huu linafanyika nchi nzima na linatekelezwa kupitia Sheria ya Nguvu za Atomu namba 7 ya mwaka 2003.

“Chini ya ardhi pia kuna madini ya Uranium hivyo, maji yanaweza kuchimbwa na kukutana na madini ya mionzi, mwananchi anaweza asijue kwahiyo tunaomba wananchi watoe ushirikiano kwa wakaguzi wanaopita katika maeneo mbalimbali kuhakikisha zoezi hili linafanikiwa vizuri,” amesema.

Amesema wamekuwa wakitoa vibali vya uingizaji, usafirishaji, umiliki wa vyanzo vya mionzi nchini, kufanya kaguzi mbalimbali katika maeneo yanayotumia vyanzo vya mionzi na kupima viasili vya mionzi kwenye mnyororo wa bidhaa ili kulinda wananchi dhidi ya madhara yanayoweza kusababishwa na mionzi.

Amesema pia tume hiyo inafanya kazi ya kupima viwango vya mionzi kwenye minara ya simu na rada za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanaokaa karibu waendelee kubaki salama dhidi ya madhara ambayo yanaweza kusababishwa na mionzi.

“Tunawalinda wafanyakazi ambao wanafanya kazi kwa kutumia vyanzo vya mionzi katika shughuli zao za kila siku, kwenye vituo vya afya, migodi, bandari, viwanja vya ndege kuna wafanyakazi wanatumia vyanzo vya mionzi katika shughuli zao za kila siku…moja ya kazi yetu ni kuhakikisha kwamba tunawaangalia wale wafanyakazi ili waendelee kubaki salama dhidi ya madhara ya mionzi.

Naye Ofisa Tafiti wa tume hiyo, Dk. Lazaro Meza, amesema mionzi inasababisha magonjwa ya saratani na mengine na kushauri wanaochimba visima kupeleka sampuli za maji katika tume hiyo ili zipimwe kujua kama maji yako salama au yana viasili vya mionzi.

“Ikitokea umechimba maji katika eneo lenye viasili vya mionzi kama mwananchi wa kawaida utajua kwa kuchuku sampuli ya maji na kuleta kwetu ili tupime tuangalie kama yako salama au yana viasili vya mionzi…kama maji yana uchafuzi wa mionzi kuna uwezekano mkubwa hata vyakula vikapata ndiyo maana kuna umuhimu wa kupima maji,” amesema Dk. Meza.

Tume hiyo inatumia maonesho hayo kutoa elimu kwa umma ili kuongeza uelewa kwa wananchi kuhusu matumizi salama ya teknolojia ya mionzi na madhara yanayoweza kupatikana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles